2. Aliyeslimu

Richard ‘Mac’ McKinney: Nilitaka kuua Waislamu, sasa nimekuwa Muislamu!

Wakati dunia ikiendelea kupona majeraha ya matukio ya kutisha yaliyotokea nchini New Zealand wiki chache zilizopita, kuna kisa kingine tofauti chenye mazingira kama hayo, ambacho kinaambatana na swali la msingi, “Sijui ingekuwaje”?

Visa vyote hivyo viwili vinamuonesha mtu aliyejaa chuki nzito dhidi ya Waislamu na anataka kuiweka chuki hiyo katika vitendo, au kuwa sahihi zaidi, anataka kuifanyia kazi. Hata hivyo, matokeo ya chuki hiyo, ndiyo yanayowaweka mbali watu hawa wawili wanaofanana kihisia. Richard Mací McKinney ni Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha ‘Ball State University’, Indiana, nchini Marekani, na Makamu wa Rais wa Kituo cha Kiislamu cha Muncie nchini humo.

Kabla ya majukumu yake kama mwanaharakati wa kijamii, McKinney alitumika eneo lingine, akiwa Sajenti wa Jeshi la Marekani. Akisukumwa zaidi na hamasa ya filamu za ‘Rambo’ McKinney alijiunga na jeshi la Marekani, akiwa na lengo la kwenda mstari wa mbele kupigana vita kama askari.

Akitumikia Jeshi la Marekani kwa miaka mingi katika Ukanda wa Mashariki ya Kati na maeneo mengine ya dunia, katika nchi kama za Somalia, Ufilipino na Amerika ya Kusini, McKinney amedai kwamba muda wake wa kuitumikia nchi yake, umechangia kwa kiasi kikubwa chuki aliyokuwa nayo dhidi ya Uislamu na Waislamu, kama anavyoeleza mwenyewe:”Sikuwa nikiuchukia Uislamu kabla, lakini mambo mengi nilioyaona ndiyo yaliyokuwa sababu ya kujihisi namna ile baadaye.”

Aliporudi nyumbani, alizongwa na mawazo ya kufanya kitendo kibaya cha kushambulia msikitiili kuua au kujeruhi mamia ya Waislamu. Alipanga kutengeneza bomu la kienyeji (homemade bomb) au IED kama linavyojulikana kitaalamu, na kisha kulitega katika Kituo cha Kiislamu cha Muncie, kwenye eneo lake la kuugesha magari, na kulilipua huku ‘akitazama shoo hiyo’ kwa mbali. Richard McKinney. anasema: “Hakuna aliyejua nilikuwa napanga kufanya nini. Nilitaka kufanya hivyo peke yangu.Nilifanya upelelezi wa eneo hilo na hata sikujali kama ningekamatwa. Nilitarajia kukamatwa ingekuwa ni sehemu ya kile ambacho kingetokea.”

Kwa bahati mbaya, mke wake aligundua mipango yake hiyo na aliwaambia FBI wachunguze nyendo zake. Unajua askari wengi wanaorudi nyumbani kutoka vitani huwa wanaathirika kisaikolojia na wanaweza kufanya mambo ya ajabu wasipopewa ushauri nasaha. Licha ya mipango yake kugunduliwa, McKinney hakuonesha kutubu wala kuacha mipango hiyo miovu. “Kama nitaishia gerezani na sindano ya sumu mkononi mwangu, hilo halina shida kwangu.” alisema Mckinney: “Nilifikiri kwa kulipua msikiti, ningekuwa naifanyia nchi yangu jambo jema sana…Nilikuwa nimevurugwa sana wakati ule.”

Binti achochea mabadiliko ya McKinney
Ni binti yake aliyekuwa darasa la pili ndiye aliyechochea mabadiliko kwa McKinney. Siku moja aliporudi nyumbani kutoka shuleni alimzungumzia mama wa mvulana mmoja anayesoma naye, ambaye alikaa karibu yake, akiwa amevaa mavazi ya stara ya mwanamke wa Kiislamu. Aliposikia habari hiyo, McKinney hakuweza kuzuia ghadhabu zake, jambo ambalo lilimkera mwanawe. Hali ya kukerwa na hasira za baba yake kwa mtoto huyu mdogo ilimsukuma McKinney kufikiria upya msimamo wake.

Alitafuta majawabu kutoka Kituo cha Kiislamu kilichopo jirani yake kuhusu vazi la mwanamke wa Kiislamu na mambo mengine kadhaa ya Kiislamu, na kituo kile kilimpatia nakala ya Qur’an Tukufu. Wiki nane tu baada ya kuingia msikitini, McKinney aliukumbatia Uislamu yeye mwenyewe.

Tangu wakati ule, amekuwa na ushawishi katika jamii. McKinney amekuwa mhamasishaji mkubwa na kiungo muhimu cha maisha ya watu. Miaka mitatu baada ya kusilimu, McKinney akawa Rais wa Kituo cha Kiislamu Muncie, kituo kile kile alichopanga kukilipua!

Mwenyewe McKinney anahadithia: “Nilianza kutumia masaa kwa masaa kule, na mambo yalikuwa yakiniingia akilini haswa. Nilijua nataka kutamka Shahada – Nilitaka kuwa Muislamu.” Tangu wakati ule, amekuwa na ushawishi katika jamii. McKinney amekuwa mhamasishaji mkubwa na kiungo muhimu cha maisha ya watu. Miaka mitatu baada ya kusilimu, McKinney akawa Rais wa Kituo cha Kiislamu Muncie, kituo kile kile alichopanga kukilipua!

Saleem Abufares, Rais mwingine wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha ‘Ball State University’, amemzungumzia McKinney: “Ni mhamasishaji mzuri sana na ni Muislamu aliyeiimarisha jamii na Jumuiya ya Waislamu pale Ball State. Amenihamasisha kufanyakazi kwa bidii katika kile ninachofanya, na ametufundisha sana kuwa marafiki wahamasishaji na Waislamu.”

McKinney hivi sasa anaendelea kufanyakazi ya kuutangaza Uislamu na akiwakilisha jamii ya Waislamu, huku pia akirekebisha fikra potofu kuhusu Uislamu na hisia mbaya ambazo watu wengi wanazo, kama mwenyewe anavyosema: “Uislamu siyo dini ya chuki wala vurugu, na nafikiri dhana nyingi potofu zinatokea kwa sababu tunachanganya tamaduni tofauti na dini.”

Ndugu zangu katika Imani, huyu ni mtu ambaye awali alipata kutamka wazi kwamba kitu pekee kinachomfanya awe hai ni chuki yake dhidi ya Uislamu, lakini sasa anahisi ana jukumu kwa jamii yake, kama anavyosema: “Nitafanya kila ninaloweza kuhakikisha kituo cha Kiislamu na watu wake wanalindwa. Nitasimama na jamii yangu kwa hali zote. Kama hiyo ina maana kukaa kituoni mchana kutwa na usiku kucha kama mlinzi, nitafanya hivyo. Sitaruhusu lolote litokee kwao – hawa ni kaka zangu na dada zangu – na hiyo ina maana kubwa kwangu.

Ndugu zangu katika Imani, moyo una rutuba nyingi mno kwa mbegu za Uislamu. Tunahitaji kupanda tu mbegu hizo ili Uislamu uchipue. Chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) inahitaji ujinga kama sharti la uwepo wake na ustawi. Wakati wowote hofu na chuki hiyo ya kijinga itakapoondolewa, na mtu akatafuta ukweli kwa uadilifu na moyo ulio wazi, bila shaka Allah ‘Azza wa Jalla’ atamuongoza.

Tujikumbushe tukio la miaka 1400 iliyopita, mtu mmoja aliyekuwa na chuki hatari moyoni mwake dhidi ya Uislamu alipoondoka nyumbani kwake akiwa na upanga mkononi ili kumuua Mtume wa Mwenyezi wa Mungu (rehema za Allah na amani zimshukie).

Mtu yule akiwa njiani kutekeleza uovu huu, ambao ungemfanya akae motoni milele, Allah ‘Azza wa Jalla’ aliufungua moyo wake kutokana na uadilifu ulio ndani yake. Alisikiliza Aya kutoka ‘Surah ya Twaha’ kwa moyo ulio wazi, hatua iliyomfanya kuukumbatia Uislamu na kumtii Mtume(rehema za Allah na amani zimshukie), katika safari yake ile ile ya ugomvi, huku akiwa bado amekamata upanga wake!

Mtu huyu baadaye akawa wa pili kwa umashuhuri katika Umma wa Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), baada ya Abubakr (Allah amridhie), mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi katika historia ya binadamu, anayeheshimiwa na Waislamu na wasio Waislamu. Huyo ni Seyyidna Umar Ibn al-Khattab (Allah amridhie).

Kuna visa vingi vya maadui waliokwenda kumdhuru Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na wakaoongozwa.Nani anayejua kuna nyoyo nyingi adilifu ambazo zimechafuliwa na ‘Islamophobia’, ambazo zinahitaji kupigwa msasa tu na kulinganiwa kidogo ili zitoke katika uovu na kuwa bora, kwa idhini yake Mwenyezi Mungu? Richard MacKinney sasa anaitwa Omar Said Ibn-Mac!

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close