2. Aliyeslimu2. Deen

Qur’an imeutaja Unasara kwa usahihi kuliko dini yoyote

“Pengine ningesilimu mapema zaidi ila nilihofia rafiki zangu Wakristo wangenichukuliaje, lakini baada ya kutafakari nilitambua kuwa siku ya hukumu nitakuwa pekee yangu bila rafiki, hapo ndipo nilipoamua kufanya hima kukiri hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake) ni Mtume wake.” Hayo ni maneno ya Agostino Lameck Nziho (24), kijana aliyelinganiwa na kaka na mjomba wake kuingia kwenye Uislamu.

Agostino ni mzaliwa wa Mkoa wa Songwe, Wilaya ya Mbozi kata ya Mlowo. Ni mtoto wa pili kati ya watoto wawili wa ndugu Lameck Nziho, na wa pili kati ya watoto wanne wa Bi. Christina Nzunda.

Katika safari yake ya kusilimu, Agostino anasema alishangaa kusikia kuwa Qur’an imetaja na kueleza vema vitabu vitakatifu vinavyoaminika kwa Wanasara na kumfanya aamini kuwa Unasara umeelezwa vizuri ndani ya Qur’an kuliko Biblia inayotumika sasa.

Agostino anasema alisoma sura ifuatayo ambayo ilimfanya ajue Uislamu umeuelezea vema Unasara. “Na tukawafuatisha Mitume hiyo, Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uongozi na nuru na isadikishayo yaliyokuwa yake katika Taurati na uongozi na Mawaidha kwa wamchao,” (Qur’an, 5:46).

Harakati za Kusilimu

Harakati za kusilimu kwa Agostino zilianzia kwa ndugu wake wa karibu, kaka na mjomba wake, ambao walikuwa ni Waislamu. Wao ndio walikuwa wakimlingania kuingia katika dini tukufu ya Uislamu licha ya kuwa mara zote aliwagomea.

Mara zote kama anavyo– simulia Agostino jibu lake lilikuwa kwamba hatasilimu kwa shinikizo la mtu isipokuwa kama atajiridhisha mwenyewe kuwa Uislamu ni dini inayomfaa basi ataufuata.

Kadri siku zilivyoenda mihula ya masomo ikapita mmoja baada ya mwingine huku akisoma masomo ya Kiislamu ikiwemo sira ya Mtume (rehema na amani ziwe juu yake). Agostino anasema kozi hizo hazikumuacha kuwa mtu wa namna ya uelewa ule ule kuhusu Uislamu.

Ni katika kusoma huko ndipo alikuja kujua kuwa Unasara umeelezwa vema ndani ya Qur’an bila namna ya kuchakachuliwa kama ilivyokuwa inatakiwa iwe katika vitabu vya mwanzo vya Unasara ambavyo kwa sasa vimechakachuliwa.

Miongoni mwa yaliyomvutia ni kujua kuwa Injili na Taurati vimetajwa ndani ya Qur’an kama ambavyo tumenukuu katika Aya ya mwanzo. “Na tukawafuatisha Mitume hiyo Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati na tukampa Injili iliyomo ndani yake uwongozi na nuru na isadikishayo yaliyokuwa yake katika Taurati na uwongozi na Mawaidha kwa wamchao,” (Qur’an, 5:46).

Baada ya kutambua ukweli huo, Agostino alianza kujenga mapenzi na dini tukufu ya Uislamu lakini hakusilimu kwa kuhofia rafiki zake Wanasara kumuona kama mtu aliyekosa msimamo.

Akiwa katika Mafunzo ya Ualimu kwa vitendo huko Makao Makuu ya nchi Dodoma, wilaya ya Kondoa ndipo anasema aliona kama anajidhulumu kwa kutosilimu akihofia rafiki zake ambao siku ya hukumu ataulizwa maswali akiwa pekee yake.

Siku mbili kabla ya Sikukuu ya Idil Adh’ha ambayo imesherehekewa hivi karibuni, Agostino alitamka shahada na aliyemsilimisha ni mwanafunzi mwenzake anayejulikana kwa jina la Nuhu Oday, ambaye wanafanya wote mafunzo kwa vitendo huko Kondoa.

Katika familia ni yeye tu na kaka yake mkubwa ambaye alimtangulia kusilimu ndio Waislamu, wengine katika familia yake ni Manasara, tunawaombea Allah ajalie kwa rehema zake Agostino awe ni saba– bu ya kuwaongoa.

Kabla ya kusilimu, Agostino amepitia madhehebu mbalimbali zote zikiwa ni jitihada za kuuta– futa ukweli ambapo amesali kanisa la Moravian, kisha “Tanzania Assemblies of God (TAG)” badaye akaenda Kanisa Katoliki Tanzania (KKT) kisha akarudi tena Moravian.

Kwa sasa Agostino ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM). Anasoma shahada ya Ualimu katika masomo ya Historia na Kiingereza.

Ruwaza wake

Agositino anasema ruwaza wake (role model) ni Sheikh Nurdin Kishk kwa ni anasema amekuwa akijifunza vitu vingi kutoka kwa Sheikh huyo.

Nasaha Agostino anatoa nasaha zake kwa ndugu zake katika imani kuwaeleza kuwa hana hakika kama hawatambui kuwa Uislamu ndio dini ya haki na mafunzo yake yamekamilika. Hivyo anawasihi kuishi kwa kufuata nguzo za Uislamu na zile za imani ili kufanikiwa.

Pili, anawanasihi kuishi kwa kufuata Sunna za Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake), Mtume ambaye ni kiigizo kwa Waislamu, na ili kutekeleza hilo amewasihi Waislamu kumsoma na kumuelewa Mtume Muhammad.

Kwa upande wa wasiokuwa waislamu, Agostino anawashauri wajikite katika kusoma historia na watafiti zaidi hususani namna ya kuenea kwa dini hiyo kama watakuwa ni wenye kuutafuta ukweli, na Mwenyezi Mungu akiwajalia huenda wakasilimu. Agostino anaeleza kuwa malengo yake ni kuisoma dini tukufu ya Uislamu ili aweze kuja kusahihisha mitazamo potofu kwa watu kuhusu dini hii.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close