2. Aliyeslimu

Nilisilimu kwa ukarimu wa familia ya Waislamu – John

Kumbe kumtendea mtu wema bila kujali ni nani, anatoka wapi au anaenda wapi kunaweza kuwa na matokeo chanya, ambayo hukuyategemea, hasa pale msaada husika unapotolewa kwa nia safi ya kupata ujira kwa Muumba wako.

Katika makala hii tutembee na Amoni John (27), kijana kutoka kijiji cha Msingisa, kata ya Sagara, wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma aliyesafiri kwenda jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya biashara ya kuuza mahindi na mtama.

Akiwa mtoto wa pili kati ya watoto nane kutoka katika familia ya Kikristo ya John Lembile na Janeth Mwega, kijana huyu aliamua kuingia katika Uislamu kutokana tu na ukarimu mkubwa aliofanyiwa na familia ya Kiislamu. Kusilimu kwa John kunamfanya kuwa Muislamu katika familia ya watu kumi, ndugu zake saba na wazazi wake.

Alivyosilimu

Kwa mujibu wa John, alianza kusikia kuhusu Uislamu kupitia kwa Mwalimu Adadi Msala katika shule ya Sekondari, Laikala iliyopo Msingisa. Ni Mwalimu huyu ndiye aliyeanza kumueleza uzuri wa Uislamu na kumlingania awe Muslamu.

Hata hivyo, wakati huo, John hakutilia maanani sana wito huo hadi ilipofika mwaka 2016 alipoenda Dar es Salaam. Ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya safari jijini humo, alipata pia hamu ya kufika visiwani Zanzibar, japokuwa hakuwa na mwenyeji huko.

Akiwa bado yupo Dar es Salaam, maeneo ya bandarini Kunduchi, alikutana na Sheame Mzee, ambaye ni mvuvi kutoka Pemba, Zanzibar. Ndio mara ya kwanza wanakutana bandarini hapo. John alimueleza Mzee kuwa anaenda Pemba. Mzee akamuelekeza John nyumbani kwao, na kumwambia aende akawaambie amemuagiza na watampokea. Angeweza kutoa maagizo hayo kupitia simu, lakini aliwakosa.

Kweli, John alipofika visiwani, alienda hadi katika familia hiyo iliyopo Pemba, Chakechake Mtaa wa Kangani akajieleza na wakampokea na akawa anaishi hapo akifanya harakati za kutafuta maisha. Siku mbili baadae yule rafiki yake, Sheame Mzee, anayeishi kwao, alimpigia simu, na katika mazungumzo, taratibu, akaanza kumlingania Uislamu. Kwa kweli, licha ya mengi mazuri aliyoambiwa, tayari John alishaanza kuwapenda Waislamu kutokana na ukarimu mkubwa aliofanyiwa. Na hapo pia akaanza kumkumbuka mwalimu wake wa sekondari aliyeanza kumlingania kabla.

Katika hili tunarejea maneno ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:

Hamtaweza kuufikia wema hasa mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda; na chochote mnachokitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua,” (Qur’an, 3:92).

Na kweli wema ulifikiwa, sio tu kwa watoaji ambao malipo yao makubwa, InshaAllah yanawasuburi huko Akhera, lakini pia kwa John ambaye wema aliofanyiwa ulimpelekea kusilimu.

John alitamka Shahada yake akiongozwa na Sheikh Hassani Haji wa huko Zanzibar, kwamba, “Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah; na Muhammad (rehema za Allah na amani zimwendee) ni Mjumbe wake. Baada ya kusilimu, John alichukua jina la Kiislamu la Omari badala ya Amoni John.

Baada ya kusilimu

John anasema, jamaa zake aliokuwa akiishi nao Zanzibar hawakuamini kuwa amesilimu kabisa. Walihisi labda alisilimu kwa kuwa tu yuko kule, lakini akirudi kijijini kwao atarejea katika Ukristo.

Hata hivyo, John tayari amethibitisha uamuzi wake wa kusilimu ni wa dhati na wa bila kulazimishwa kwani amepiga hatua kubwa katika kujielimisha kuhusu dini, ikiwemo kuisoma Qur’an. Kwa sasa ana uwezo wa kusoma Juzuu A’mma kwa wepesi.

Kadhalika, sasa hivi John ana furaha zaidi kwa sababu nuru ya Uislamu inazidi kung’ara huko kwao. Anasema, wakati anaondoka hakukuwa na Muislamu hata mmoja, miaka miwili baada ya kutoka na kwenda kuishi Zanzibar, aliporudi alikuta watu wengi wamesilimu.

Nasaha

John anawashauri Waislamu kuufuata Uislamu kwa vitendo, akisema kuwa, kufanya hivyo ni sehemu kubwa na nyepesi ya juhudi za ulinganiaji. John anasema, kutekeleza Uislamu kunashawishi zaidi kwa wasio Waislamu kuliko maneno maneno matupu. Bila shaka kusilimu kwake ni mfano hai.

Pia John anawashauri Waislamu kusimamisha Swala sambamba na kuisoma vema dini yao kuliko kujiita Waislamu hali ya kuwa hawaijui dini hii tukufu.

Ni changamoto mtu aonekane anasali hali ya kuwa hajui inatakiwa asali vipi,” John alisema.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close