2. Aliyeslimu

Kupigania hali za wasioona Waislamu ni lengo letu – Benedicto

Wakati ukiendelea kuvuta pumzi aliyokujalia Mwenyezi Mungu na hauilipii hata senti, jiulize nini umefanya kwa ajili ya dini yako na umma wa Kiislamu kwa ujumla? Jamii ya Kiislamu inahitaji kuwa imara kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata kielimu (zote, ya mazingira na muongozo). Nguvu na uimara huu hauwezi kupatikana bila Waislamu wenyewe kufanya kazi.

Leo, katika makala hii tunamuangalia mlemavu wa macho, Luis Benedicto (38), ambaye alisilimu kutoka Ukristo mwaka 2010. Akiwa na miaka nane tu tangu asilimu, Benedicto tayari ameweka alama kwani yeye ni muasisi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walemavu wa macho Waislamu Tanzania (TAIBU).

Luis Benedicto ambaye ni mzaliwa wa mkoa wa Kigoma, alikuwa akiabudu katika dhehebu la Roman Katoliki (RC), na baada ya kusilimu aliitwa Salim Benedicto. Licha ya kuwa ni Mwenyekiti wa TAIBU), Benedikto pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) na pia ni Afisa Elimu katika Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Bila shaka hapo ushajua kuwa, kitaaluma, Benedicto ni mwalimu aliyehitimu Shahada ya Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Sekomu kilichopo Tanga.

Akiwa katika Ukristo, Benedicto alipata Kommunio na Kipaimara, na vilevile alikuwa ni muimbaji wa muziki wa injili katika Shule ya Msingi Furaha iliyoko Tabora alikosoma kuanzia mwaka 1991 hadi1996.

Kusilimu

Safari ya Benedicto hadi kusilimu ilitokana na kukosa amani na utulivu wa kweli alioutarajia katika ndoa ya kwanza aliyofunga akiwa muamini wa dhehebu la Kiroma mwaka 2004 huko Tabora katika Parokia ya Mtakatifu Theresia. Benedicto alisema, katika ndoa hiyo, badala ya kupata raha alionja karaha kutokana na kile anachosema yule aliyefunga naye ndoa kuonekana kutomkubali kwa dhati kutokana na hali aliyokuwa nayo ya ulemavu wa macho.

Waswahili wanasema, “Uzito wa mzigo anaujua alieubeba.” Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Benedicto kwani baada ya kuona matatizo yanakuwa mengi alienda kwa viongozi wake wa kiroho ili kuivunja ndoa lakini alikataliwa kwa sababu sheria Ukristo haziruhusu kuvunja ndoa. “Nililazimika kwenda kinyume na sheria za kidini nikavunja ndoa ili kupata amani ya roho, jambo ambalo kwa RC haliruhusiwi. Nisingeweza kuishi na mtu ambaye hakunikubali kwa dhati hali ya kuwa mi nateseka eti kisa sheria za dini haziruhusu kuivunja ndoa! Sikuona mantiki yake” alisema Benedicto.

Kutokana na hilo, alijiuliza maswali mengi, huku akijifunza zaidi baadhi ya misimamo ya dini yake ambayo kwake ilikosa matinki ikiwemo hili la kuzuiwa kuvunja ndoa licha ya kuwa ilikuwa wazi kuwa salama yake (Benedicto) ingetokana na kuachana na yule mwanamke tu. Baadaye, Benedicto alihama kutoka dhehebu la Roman Katoliki na kuingia katika makanisa ya kipentekoste, akidhani huenda akawa sawa nao kwani madhehebu hayo yanatofautiana kwenye masuala kadhaa na RC.

Licha ya kubadili dhehebu, maswali yaliyokosa majibu yalizidi, ikiwemo suala la madai ya uungu wa Yesu (Nabii Isa). Lakini walau alijisikia vema kuwahama RC ambao “wana hadi masanamu!” alisema. Mwishoni mwa mwaka 2010, akiwa katika harakati za kutafuta mke ambaye atakuwa mchamungu na ambaye angemkubali kwa hali aliyonayo, Mwenyezi Mungu alimkutanisha na bint wa Kiislamu kutoka Zanzibar aitwaye Mariam Abdallah Bakari.

Licha ya mashaka aliyokuwa nayo juu ya dini yake, Benedicto hakuwahi kufikiria kubadili dini na kuwa Muislamu. Lakini bint huyo, alipokutana na binti huyo aliyejitoa kwa moyo wote kumpenda; Benedicto akajikuta anaukubali Uislamu. Hatimaye, Benedicto alitamka shahada kuwa; “hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ni Mtume wake.”

Kusoma Uislamu

Hadi hivi leo, tunapozungumza, Benedicto ana uwezo wa kusoma Qur’an Tukufu kwa kutumia alama za nukta – nundu ambazo msingi wake alikuwa nao tangu Shule ya Msingi Furaha. Nukta -nundu za upande wa Kiarabu alijifunza katika Madrasatul Nuur mwaka 2012 huko Afrika Kusini ambako alikwenda kusoma kozi ya utawala kama kiongozi wa Chama cha Wasioona Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora (TLB). Akihudhuria mafunzo hayo, Benedicto aliweka kambi katika Madrasatul Nuur maalumu kwa ajili ya wasioona ili kujifunza dini yake pia.

Harakati katika Uislamu

Kumbuka, kwa sasa Luis Benedicto ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), kilichoanzishwa mwaka 1964 na kupata usajili rasmi mwaka 1972 kikiwa kinajihusisha na kupigania haki maalumu za wenye ulemavu huo hususan katika elimu, afya nk. Baada ya kutambua changamoto zinazowakumba wasioona Waislamu ambazo kwa namna moja au nyingine si changamoto kwa wasioona wasio Waislamu, ndio wakalazimika kuasisi chama cha Wasioona Waislamu (TAIBU) akiwa pia ni Mwenyekiti.

TAIBU ina malengo mengi ikiwemo kuunganisha wasioona Waislamu, kuwapa elimu wasioona Waislamu kwa kuanzisha shule na vyuo vitakavyofundisha sio tu elimu ya mazingira bali pia ya muongozo kwa kutumia vifaa muafaka, ikiwemo nukta-nundu. TAIBU pia inakusudia kuinua uchumi miongoni mwa wasioona ili kuokoa watu wasioona kutoka kwenye hali ya utegemezi na hivyo kuwa ombaomba.

Mafanikio
Mafanikio ya TAIBU mpaka sasa ni mengi. Kwanza, licha ya upya wake, TAIBU imepokelewa vyema na jamii. Hilo linathibitika kutokana na ukweli kuwa, wamepokea michango mingi kutoka kwa jamii ya hali na mali. Tayari TAIBU imekabidhiwa kiwanja na Muislamu ili taasisi hiyo ijenge madrasa ya wasioona. Pia, TAIBU imetengeneza muundo wa uongozi wenye idara mbalimbali, na sasa wako katika hatua za mwisho za kutengeneza katiba, zoezi ambalo linashughulikiwa na wanasheria.Allah azidi Benedicto kumjalia hekima katika kuhudumia jamii.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close