2. Aliyeslimu

Kombola: Nilianza kwenda Msikitini na Madrasa kabla ya kusilimu

Kisa chake cha kusilimu kina matukio mengi lakini jambo kubwa linalodhihirika ni kuwa Mwenyezi Mungu akitaka kumuongoza mtu katika haki, hutokea hivyo bila mtu mwenyewe kujitegemea.

Hilo linathibitika katik kisa cha Hassani Hassani Kombola (23) aliyekuwa anasoma Shule ya Seminari kwa ufadhili wa Kiongozi wa Kanisa akiandaliwa aandaliwe kuwa Mtawa. Hata hivyo, hakumaliza. Aliishia kufukuzwa yeye na wenzake kadhaa na hatimaye Allah akamjaalia kusilimu.

Wenzake walioendelae na masomo sasa ni wanasomea Upadri ila yeye anafurahi kuingia katika nuru ya dini tukufu ya Uislamu.

Ni nani Kombola?

Kombola ni mzaliwa wa Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Ulanga, Kata ya Mahenge akiwa ni mtoto wa pili kati ya watatu wa Hassan Kombola. Pia yeye ni mtoto wa kwanza kati ya wanne wa Bi. Faustine Ferdinarnd.

Kipindi cha Ukristo hadi sasa

Kombola anasema baba yake alikuwa Muislamu na mama yake Mkristo, kisha alifariki angali yeye mtoto mdogo na hivyo kulazimika kukulia katika mazingira ya Kikristo nyumbani kwa mama yake.

Tangu akiwa mdogo, Kombala aliabudu katika Kanisa la Dhehebu la Roman Katoliki (RC). Alipata ubatizo katika Kanisa la Kosita lililopo Mahenge. Mwaka 2007 alipata Komunio katika Kanisa la Sali lililopo Ruaha.

Baadaye, Kombola alichukuliwa baba yake mkubwa, Salimu Kamando ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa msikiti huko Mwaya mjini. Mazingira hayo kwa baab yake mkubwa, kwa mujibu wa Kombola, yalimmshawishi kusilimu, uamzui ambao anasema hajawahi kuujutia.

Kombola anaamini Uislamu ni dini ya haki, pasipo shaka. Akiwa kwa baba yake mkubwa, kila siku ya Ijumaa familia nzima ilienda msikitini huku yeye akibaki nyumbani peke yake. Naye alienda kanisani peke yake kila Jumapili.

Mazingira yote aliyoishi kwa baba yake yalikuwa ni ya Kiislamu, siyo tu nyumbani bali hata kwa majirani na jami nzima. Watoto wenzake walikuwa wakimshangaa waliposikia kuwa ni Mkristo.

Baadaye kidogo, Kombola alianza kupata athari na kuanza kubadilika. Akaanza kwenda msikitini siku ya Ijumaa na kusoma madrasa, hata kabla hajasilimu.

Mwaka 2010 alipata pigo jingine kwa kumpoteza mama yake mzazi aliyetangulia mbele ya haki. Kombola aliendelea kukaa kwa baba yake mkubwa.

Mwaka 2010 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alipelekwa na kiongozi wa kanisa katika Shule ya Seminari ya Sali kuusoma masomo ya kujiandaa kuingia kidato cha kwanza (pre-form one) ili baadaye aandaliwe
kuwa mtumishi wa kanisa.

Lakini Kombola alifukuzwa na wenzake baada ya wenzake kupigana na wote kukataa kuwataja waliohusika. Hii ilikuwa ni mipango ya Mungu kwani wenzake waliobaki wanaendelea na masomo ya Upadri.

Baada ya kufukuzwa, mmoja wa baba zake wadogo alimpeleka Shule ya Sekondari ya Kata iitwayo Celina Kombani ambapo alisoma hadi kuhitimu kidato cha nne mwaka 2014.

Mwanzoni mwa mwaka 2016 Kombola alisilimu akiongozwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, marehemu Abdallah Mkang’ambe aliyeenda Mahenge kwa ziara ya kidini.

Kombola anakumbuka kuwa, kabla hajasilimishwa, Sheikh Mkang’ambe alimuuliza sababu iliyompelekea. Alimueleza na alipojiridhisha alimtamkisha maneno ya Tauhid kuwa: “Hapana Mola wa haki isipokuwa Allah na Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ni Mtume wake.

Baada ya kumsilimisha, Sheikh Mkang’ambe alimuahidi kumsomesha masomo ya Chuo katika ngazi ya Astashahada ila bahati mbaya Sheikh huyo alifariki kabla muda haujafika. Hata hivyo, kwa sasa Kombola ni Mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) akichukua Stashada ya Sayansi na Teknolojia ya Maabara.

Nasaha

Kwa Waislamu, Kombola anawashauri kwanza kuanzisha na kulea familia katika misingi ya dini tukufu ya Uislamu, jambo ambalo anaamini yeye alilikosa na hivyo kusababisha mdogo wake kubaki katika Ukristo. Alisema, huenda zipo familia nyingi za Kiislamu zenye mseto kama huo.

Pili, anawashauri Waislamu kuwekeza katika elimu zote mbili ya mazingira na Muongozo. Anaamini binadamu Waislamu tukipata elimu hizo tutafikia daraja la kweli la Ukhalifa katika hii dunia.

Ama kwa upande wa wasiokuwa Waislamu, anawashauri kutafuta ukweli kote katika Ukristo na kwa Uislamu, na InshaAllah Mwenyezi Mungu atawaongoza. Alisema, Uislamu ni dini isiyo na kasumba za kuficha mambo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close