2. Aliyeslimu

Kijana aliyevutiwa na Nguzo Tano za Uislam

Miaka 28 iliyopita mzee Mikidadi William Shilunga pamoja na mkewe walifanikiwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, kumleta duniani Yona Shilunga ambaye wiki hii nilifanikiwa kukutana na kuzungumzo naye.

Shilunga ambaye sasa hivi anaitwa Ustadh Juma Shilunga, alizaliwa katika kambi ya Jeshi la Wananchi Sangasanga iliyoko Ngerengere katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, wakati huo baba yake akiwa afisa wa jeshi.

Mwaka 1997, umri wa kwenda shule ulipotimu, Shilunga alianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Sangasanga hadi mwaka 2003 alipomaliza na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza mwaka uliofuata.

“Nilianza kidato cha kwanza kwenye Shule ya Sekondari ya Kutwa Ngerengere lakini nilipofika kidato cha pili nikahamishiwa Dodoma katika Shule ya Sekondari Bihawana,”alisema. Hata hivyo, alipofika kidato cha tatu Shilunga alirejea tena katika Shule ya Sekondari ya kutwa Ngerengere na kufanikiwa kumaliza kidato cha nne mwaka 2007.

Maisha yake kiroho

Tangu alipozaliwa hadi anapata akili, maisha ya Shilunga kiroho yalifungamana mno na mafundisho ya dini ya Kikristo hasa katika dhehebu la Roman Katholiki.

“Mimi nimepata mambo yote ya muhimu anayotakiwa kupata kijana wa Kanisa Katoliki kuanzia ubatizo, hekaristi na kipaimara,”

alibainisha Yona. Hata hivyo, Shilunga alisema pamoja na mafundisho ya Kikristo aliyokuwa akiyapata Kanisani, alitamani mara kwa mara alitamani ajifunze Uislamu.

Kusilimu kwake

Shauku yangu kubwa ilikuwa ni kujua sababu ya Shilunga kutoka katika Ukristo na kuwa Muislamu, kwa hiyo nilitaka ufafanuzi zaidi kuhusu hamu aliyokuwa nayo ya kuujua Uislamu miaka hiyo akiwa shuleni.

“Kiukweli sijui ilikuwaje, lakini ninachoweza kukuambia ni kwamba, nilipokuwa Shule ya Msingi Sangasanga nilianza kushawishika kuupenda Uislamu. “Ninachokumbuka ni kuwa ukiachilia mbali kuzungukwa na marafiki Waislamu, pia nilivutiwa na mambo waliyokuwa wakiyafanya”, alisema huku akiniangalia kwa makini. Miongoni mwa mambo ambayo yalimvutia Shilunga ni kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuswali mara tano kwa siku. Katika funga ambayo ni nguzo ya nne baada ya Zakka, kijana huyo alivutiwa na Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye ameeleza kwa kina faida anazopata mfungaji,.

Nilikuwa naangalia Waislamu inapofika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wanafunga, wanaswali sana na ndani ya mwezi huo huongeza mapenzi baina yao na kuhurumiana kiasi nikatamani ifike siku nami niwe Muislamu”, alifahamisha. Aidha Shilunga alitamani pia kuingia msikitini lakini hakujua angewezaje wakati hakuwa Muislamu na umri wake haukuruhusu kujichukulia maamuzi makubwa ya kujichagulia dini aitakayo. Alipotimiza miaka 18, Yona Shilunga bado alikuwa na dhamira yake moyoni, kwamba siku moja awe Muislamu.

Siku moja sikumbuki mwaka gani, niliwahi kumwambia rafiki yangu Paulo kwamba siku moja nitakuwa Muislamu. Aliniuliza kwanini, nikamjibu ndiyo dini ambayo moyo wangu unaipenda,”alisimulia. Kwa kuwa suala hilo lilikuwa moyoni mwake siku nyingi, ilipofika mwezi wa Ramadhani wa mwaka 2014 Yona alijiambia mwenyewe kwamba ulikuwa muda muwafaka wa kutimiza azma yake.

“Nikawaambia baadhi ya rafiki zangu akiwemo na yule Paulo kwamba, Ramadhan ikiisha tu, nami naingia moja kwa moja katika Uislamu, hawakuamini kwa kweli. “Baada ya kupita mwezi huo mtukufu, Ustadh wangu mmoja, aitwaye Dahela alinambia suala la kusilimu halifai kulichelewesha. Kwa hiyo kijana Shilunga alitoa matamshi ya Shahada mbili na kuchagua jina la Juma.

Baada ya kusilimu

Baada ya kusilimu kijana Juma Shilunga alianza kujifunza misingi ya Uislamu katika madrasa moja iliyopo katika msikiti mkuu wa Ijumaa wa Ngerengere na kwa baadhi ya Masheikh anaofahamiana nao. Kutokana na elimu chache ya dini aliyokuwa akiipata kwa kuhudhuria madrasa, Shilunga aliona mapenzi yake kwa Mola wake na Uislamu wake yakizidi kila uchao sambamba na kujiepusha na magenge ya vijana wasio na maadili.

“Zamani kaka ilikuwa hakuna muziki unaonipita, hata upigwe wapi nitaufuata, kulala kwangu ilikuwa sio chini ya saa saba usiku. Hayo ndiyo maisha yangu kabla sijasilimu. Lakini tangu niingie katika Uislamu kwa hakika namshukuru Mungu sijui kitu gani kimefanya ule muziki niliokuwa nikiusumbukia mbali, leo hata ukipigwa nyumba ya pili sina habari nao,” alisema akionekana mwenye furaha tele.

Alisema ukiacha mabadiliko hayo ya kuachana na muziki, yapo maasi mengi aliyokuwa akiyafanya lakini saa amefanikiwa. Shilunga anasema kutokana na mabadiliko yaliyomotokea katika maisha yake, ndugu na rafiki zake wanashindwa kuamini kuwa ni Uislamu uliombadilisha, wakidhani kuwa huenda kuna dawa alitumia.

Wito kwa umma

Ustadh Juma Shilunga aliwaasa Waislamu kuendelea kuwa wamoja, kushikamana na kuhusiana kutenda mambo mema na kukatazana kutenda mambo mabaya. Kwa wale ambao bado hawajabahatika kuwa Waislamu, Shilunga aliwataka kutohofia kuingia kwenye dini hiyo ambayo kwa maelezo yake ni nzuri inayokwenda sanjari na maumbile ya mwanadamu, ukilinganisha na dini nyingine.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close