3. Akisi Ya Aya

Ufahamu undani wa ugonjwa wa bawasili

Bawassili ni moja ya magonjwa maarufu zaidi yanayoathiri mfumo wa chakula hususan njia ya haja kubwa. Kwa kitaalamu ugonjwa wa bawasili hujulikana kama ‘hemorrhoids’ jina ambalo limetokana na kuvimba na kuchomoza kwa mishipa ya damu inayopatikana katika puru (rectum) na mlango wa haja kubwa.

Mishipa hii hujulikana kama ‘hemorrhoidal veins’ na kazi yake kubwa ni kusafirisha damu kwenda kwenye moyo. Mishipa hii pia inaweza kuchomoza katika eneo lolote kati ya haya mawili na hapo ndipo tunapopata aina kuu mbili za ugonjwa huu.

Bawasili ya ndani (internal hemorrhoids)

Kwa kawaida, aina hii ya bawasili hutokea ndani katika puru. Aina hii ni mara chache kusababisha dalili, lakini kama itadumu kwa muda mrefu inaweza kuchubuka na kusababisha damu kidogo kuvuja wakati wa haja kubwa. Pia bawasili ya ndani inaweza kua kubwa na kuchomoza kama nya
ma kwenye mlango wa haja kubwa.

Bawasili ya nje (external hemorrhoids)

Aina hii ya bawasili ndiyo sumbufu zaidi kwa kua ndiyo imekua chanzo kikubwa cha uwasho na maumivu makali wakati wa haja kubwa. Mara nyingi bawasili hii huonekana kama vijivimbe pembezoni mwa mlango wa haja kubwa na kawaida huwa na maumivu endapo vitaguswa.

Visababishi vya bawasili

Kwa lugha rahisi tunaweza kusema kua bawasili ni mishipa ya damu iliyovimba na kuchomoza katika njia ya haja kubwa katika eneo la puru (rectum) au kuzunguka mlango wa haja kubwa.

Kuvimba huku na kuchomoza kunasababishwa na kuongezeka kwa shinikizo au msukumo katika maeneo tajwa hapo juu. Shinikizo hili mara nyingi husababishwa na kujikamua sana wakati wa haja kubwa, matumizi ya muda mrefu ya choo cha kukaa, kuhara au kukosa choo kwa muda mrefu, uzito mkubwa wa mwili, ujauzito, mapenzi kinyume na maumbile pamoja na ukosefu wa nyuzinyuzi (fibers) katika lishe. Vitu hivi vyote vinaweza kusababisha bawasili.

Kwa upande wa wanawake, bawasili ya muda mfupi inaweza kusababishwa na uchungu wakati wa kujifungua na pia bawasili nyengine huweza kujitokeza kwa mwanamke akiwa katika siku zake.

Kutegemea na ukubwa na aina ya bawasili, inakadiriwa kua ugonjwa huu unaweza kujitokeza na kuondoka bila ya kusababisha dalili yoyote hasa kwa watu wenye umri mkubwa. Ikiwa bawasili itakua kubwa au itavimbia kwa nje, hapo dalili mbalimbali zinaweza kuhisiwa na mgonjwa.

Dalili zake

Kwa kawaida dalili zote za bawasili zinahusisha mabadiliko katika njia ya haja kubwa ambayo huhisiwa zaidi wakati wa kwenda haja. Mabadiliko hayo ni pamoja na kuvuja damu wakati wa kwenda haja, uwasho na maumivu, uvimbe pembezoni mwa mlango wa haja kubwa na pia kutokeza kinyama kwenye njia ya haja kubwa.

Wakati wa kumuona daktari

Dalili za bawasili zinaweza kuwa hatari au zisiwe hatari. Kama una dalili hatari kama vile kuvuja damu au kupata maumivu makali wakati wa haja kubwa, ni vyema kwenda kumuona mtaalamu wa afya ili kuweza kujua nini sababu hasa ya dalili zako. Pia mtaalamu wa afya atakusaidia kujua maradhi mengine yaliyo na dalili sawa na maradhi yako sambamba na kupatiwa tiba na ushauzi wa namna ya kujikinga na maradhi hayo.

Dondoo za kujikinga Bawasili ni ugonjwa unaoepukika kirahisi ikiwa mambo yafuatayo yatazingatiwa. Kula mlo kamili unaohusisha vyakula na matunda yenye nyuzinyuzi kama vile maharage, viazi vitamu, machungwa, parachichi, peasi, ndizi, peasi n. k.

Pia ili kuepuka bawasili ni muhimu kunywa maji ya kutosha, kufanya mazoezi, kuepuka kufuga haja kwa muda mrefu, kuepuka kukaa kitako kwa muda mrefu pamoja na kutumia choo cha kuchuchumaa.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close