3. Akisi Ya Aya

Je! Wanadhani Watu Wataachwa Kwa Kuwa Wanasema, ‘Tumeamini’; nao wasijaribiwe?”

Assalam Alaykum wapenzi wasomaji wa safu hii ya Akisi ya Ayah. Kwa mara nyingine tena, Insh’Allah, leo tuakisi Aya zinazotoka Surah Ankabut ambazo zinasomeka namna hii: “Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: ‘Tumeamini’; nao wasijaribiwe” (Qur’an, 29:2).

Wakati Aya hiyo iliposhuka, hali ya mambo mjini Makka ilikuwa mtihani mkubwa. Kila aliyeukubali Uislamu basi alikuwa shabaha ya unyanyasaji, ukandamizaji na udhalilishaji. Kama alikuwa mtumwa au masikini, basi alipigwa na kupewa mateso yasiyovumilika. Kama alikuwa muuza duka au fundi, basi angepewa mateso ya kiuchumi ili afe njaa. Kama angekuwa mwanafamilia wa ukoo mashuhuri, basi watu wake wangempa mateso na manyanyaso mbalimbali, ili kufanya maisha yawe magumu kwake. Hali hii ilijenga mandhari ya hofu na kihoro mjini Makka, kiasi cha watu wengi kuogopa kumfuata Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie), ingawa ndani ya nyoyo zao walimkiri kuwa ni Mtume wa kweli kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuna wengine waliamini lakini baadaye wakavunjika moyo na kurejea walikokuwa awali baada ya kupata kibano na mateso makali. Ingawa mitihani hii ya kutisha haikutikisa hata chembe imani ya Maswahaba waliokuwa madhubuti, kuna baadhi ya nyakati ilijenga hofu kwenye nyoyo zao. Mfano wa hili ni kisa cha Khabbab bin Arat (Allah amuwie radhi) kilichosimuliwa na Bukhari, Abu Daud na Nasai. Khabbab anasema: “Katika kipindi ambacho tulichoka na manyanyaso ya washirikina, siku moja nilimuona Mtume akiwa amekaa kwenye kivuli cha ukuta wa Kaaba. “Nilikwenda na kumuambia atuombee kwa Mwenyezi Mungu ili atusaidie. Baada ya kusikia hivyo Mtume alikasirika sana na kusema, ‘Waumini waliopita kabla yenu walipata mateso zaidi. Baadhi yao walikatwa vipande viwili kwa msumeno kuanzia kichwani. Wengine waliteswa kwa machanuo ya chuma ili kuwafanya waitupe imani yao. Kwa haki ya Mungu kazi hii itakamilika na muda siyo mrefu, wakati mtu atakaposafiri bila bughudha kutoka San’aa mpaka Hadhramaut na hakuna atakayeogopewa isipokuwa Allah tu.’” Sasa ili kuondoa hali hii ya msukosuko na kuwa uvumilivu, Allah Ta’ala Aliyetukuka anawaambia waumini kwamba hakuna atakayeweza kustahili ahadi zake za mafanikio hapa duniani na akhera kwa kusema tu imani yake. Bali kila atakayedai kuwa na imani hii basi atapitia mitihani na misukosuko kadhaa, ili kuthibitisha ukweli wa madai yake. Ndugu zangu katika imani, tukiakisi kwa kina Aya hizo za Mwenyezi Mungu, tutaona kwamba Pepo yake siyo rahisi. Wala mafanikio yetu hapa duniani pia siyo rahisi. Hayapatikani kwa kusema tu kauli tupu. Lazima kuwe na mitihani mizito ya kupima imani. Waumi lazima waonje machungu, wapate hasara ya mali na maisha kwa sababu ya Mwenyezi Mungu. Kila Waislamu wanaopatwa na madhila, machungu, mateso, hofu na adha nyingine kutoka kwa makafiri na wanafiki, basi jambo la kuakisi na kutafakari ni maneno ya Mwenyezi Mungu yasemayo: “Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyowajia wale waliopita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walioamini pamoja naye wakasema, ‘Lini nusura ya Mwenyezi Mungu itakuja?’ Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu,” (Quran, 2:149). “Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali M w e n y e z i Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu waliopigana Jihadi, na hajawap a m b a n u a waliosubiri?” ( Q u r ’ a n , 3:142).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close