3. Akisi Ya Aya

Hakika Allah Anakuamrisheni Kuzirudisha Amana Kwa Wenyewe…

Assalam Alaykum wapendwa wasomaji wa safu hii ya Akisi ya Aya. Leo Insh’Allah tuendelee pale tulipoishia wiki iliyopita. Tunaakisi Aya kutoka Surat Nisaa zinazosomeka namna hii:

“Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni kuzirudisha amana kwa wenyewe. Na mnapohukumu baina ya watu mhukumu kwa haki. Bila shaka mawaidha anayokutoleeni Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye asikiaye na aonaye” (Qur’an, 4:58). Kama tulivyosema awali, ukiakisi kwa kina, utaona amana ina maana pana zaidi kuliko tunavyoweza kufikiri. Amana ipo katika kila kipengele cha maisha yetu. Hebu tuangalie mifano ifuatayo ya amana na nafasi yake katika maisha yetu. Wafanyakazi uliowaajiri ni amana kwako na utaulizwa juu yao. Mtume wa Mwenyezi Mungu ameripotiwa akisema: “Mlipe mfanyakazi ujira wake kabla jasho lake halijakauka” – (Ibnu Majah). Familia yako ni amana ambayo utaulizwa juu yake. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an: “Enyi! Mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu na moto, ambao kuni zake ni watu na mawe” (Qur’an, 66.6). Mume wako ni amana ambayo utaulizwa juu yake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani ya Allah imshukie) amesema katika Hadithi: “Mwanamke yeyote ambaye atakufa huku mumewe akiwa amemridhia ataingia peponi”(Tirmidhi, Ummu Salamah). Faragha iliyopo kati ya mume na mke ni amana. Imeripotiwa mchamungu mmoja aliyetangulia alitaka kumuacha mke wake. Aliulizwa: “Kwanini unataka kufanya hivyo?” Alijibu: “Mtu mwenye busara hatoi siri za mkewe.” Baada ya kumuacha alifuatwa tena na kuulizwa, “Kwa nini umemuacha mwanamke yule?” Alijibu, “Kwa nini unaniuliza kuhusu habari za mke wa watu?” Muda wako ni amana ambayo utaulizwa juu yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaambia watu wa motoni wakati watakapoomba kupewa nafasi ya pili: “Hatukukupeni umri wa (kuweza) kukumbuka mwenye kukumbuka” (Qur’an, 35:37). Matamanio yako na sehemu zako za siri ni amana ambayo utaulizwa juu yake. Abdullahi Ibn Umar (Allah amuwie radhi) amesema: “Mwenyezi Mungu Mtukufu ameumba sehemu za siri za mwanaume na kusema, ‘Hii ni amana ambayo nimeificha kwako, kwa hiyo itunze isipokuwa pale inaporuhusiwa’” (Razi, Tafsir Kabir). Nafasi uliyonayo katika jamii, iwe uimamu, uongozi, mlinganiaji, mwanaharakati ni amana ambayo utaulizwa juu yake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani ya Allah imshukie) alipoulizwa: “Amana inapoteaje?”, alijibu: “Pale madaraka au mamlaka yanapoingia mikononi mwa wasiostahili, basi subirini ile saa”. Mifano tuliyoitaja hapo juu ni michache tu. Lakini kuwa hakika zaidi, hata Qur’an uliyoifungia kabatini, Swala unazoswali msikitini, Hijab ya Kiislamu unayovaa, na mwili ambao Allah Ta’ala ametuazima ni amana. Ndugu zangu katika imani, tukiakisi kwa kina zaidi, tutaona Dini yetu yote hii n i a m a n a . Insh’Allah tutamalizia sehemu iliyobaki ya akisi hii wiki ijayo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close