3. Akisi Ya Aya

“Bila Ya Shaka Dini Mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu..”

Assalam Alaykum wapenzi wasomaji wa safu hii adhimu ya Akisi ya Ayah. Leo Insh’Allah tuakisi Aya hiyo mashuhuri kutoka Surat Ali Imran inayosomeka: “Bila ya shaka dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu..” Qur’an(3:15).

Mbele ya Mwenyezi Mungu, kuna mfumo mmoja tu wa maisha, ambao unalingana na uhalisia wa maumbile ya binadamu na maadili yake. Sehemu ya mfumo huo ni binadamu kumkiri Mwenyezi Mungu kama Mola wake na kwamba Yeye tu ndiye anayestahili kuabudiwa. Katika mfumo huu, binadamu anajisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu kwa kumtii na kumtumikia. Kwa kufanya hivyo, binadamu anapaswa kufuata kikamilifu muongozo kama ulivyowasilishwa na Mwenyezi Mungu kupitia Mitume wake, badala ya kujaribu kuvumbua njia za kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa akili zake. Utaratibu huu wa fikra na vitendo unajulikana kama Uislamu, na inafahamika vyema kwamba Mwenyezi Mungu Muumba wa ulimwengu hawezi kukubali mfumo mwingine kutoka kwa viumbe wake. Lakini kwa upumbavu wake, binadamu anafikiri ana haki ya kuamini na kufuata kila imani inayokuja mbele yake, iwe upagani au kuabudu masanamu. Tukiakisi Aya hiyo, tutaona kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake, tabia na mienendo kama hiyo ni uasi dhidi yake. Ndugu zangu katika imani, tukiakisi kwa kina zaidi Aya hiyo, tutaona kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuumba, akaumba dunia na vyote vilivyomo. Kwa ukweli huo, Yeye ndiye mwenye haki na anayepaswa kuweka utaratibu wa sisi kuishi hapa duniani. Binadamu kujibunia mfumo wa maisha au utaratibu wa kuishi ulio kinyume na ule uliowekwa na Mwenyezi Mungu ni kupora mamlaka ya Mwenyezi Mungu. Mfano wake ni kwamba wale wazalishaji wa magari aina ya ‘Hyundai’ ndiyo wenye haki ya kutoa kitabu cha maelekezo kuhusu utendaji wa gari hiyo. Yaani wakati gani ifanyiwe ‘service’, mafuta yamwage baada ya kilomita ngapi na kadhalika. Wenye haki na wajibu wa kutoa maelekezo hayo ni ‘Hyundai’ na siyo watu wengine. Dini hii ya Uislamu (kujisalimisha kwa Muumba) ndiyo dini ya Mitume wote wa Mwenyezi Mungu katike kila zama. Vilevile, kila kitabu kitakatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiwe katika lugha yoyote kilichoteremshiwa, kwa ajili ya watu wa zama zozote, kilikuwa na mafundisho ya Uislamu. Dini zilizobuniwa baadaye na kusambazwa miongoni mwa wanadamu kiuhalisia ni upotoshaji wa dini hii asili na ni matokeo ya kuchezea dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kutamani zaidi kuliko vile wanavyostahili, kumewafanya binadamu kubadili imani, misingi na maamrisho y a d i n i y a Mwenyezi Mungu ili kukidhi maslahi yao binafsi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close