10. Ramadhan

Watoto wako wanafunga Ramadhan hii?

Allah Ta’ala amewafundisha wazazi ndani ya Qur’an jinsi ya kuomba dua kwa ajili ya watoto wao: “Na wale wanaosema, ‘Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe viongozi kwa wachamungu.’” [Qur’an, 25:74].

Ibn Abbas (Allah amridhie) amefafanua kwamba maana ya ‘yaburudishayo macho’ ni kizazi au watoto watakaojipinda katika kumtii Mwenyezi Mungu na kuwaletea furaha katika hii dunia na Akhera.

Moja ya jambo lenye malipo makubwa na kuridhisha kwa mzazi ni kuona watoto wao wakibaleghe huku wakimtii Allah na kufuata dini yake. Mtoto akishika dini ya Allah katika maisha yake, mzazi anajua amepata chanzo cha ‘Sadaqatun Jariyah’ (sadaka yenye kuendelea) kwani mtoto mwema huendeleza mema.

Allah hakuwafundisha wazazi kuwaombea watoto wao kuwa wema tu, bali kuwa viongozi wa watu wema. Allah wakati wote anawahimiza wazazi kuwa na matarajio makubwa na kuwawekea watoto wao malengo ya juu.

Ibn Kathir (Allah amrehemu) amesema: “Wao (wazazi) walitaka ibada yao iunganishwe na ibada ya watoto wao na kizazi, na muongozo wao uende mbali zaidi na kuwanufaisha wengine.” [Tafsir Ibn Kathir].

Wasiwasi mkubwa wa Mitume ndani ya Qur’an wakati kifo kilipowakabili ulikuwa ni juu ya watoto wao:
Kweli watabaki kuwa wa kweli katika ibada na utii kwa Allah Ta’ala!? “Je! Mlikuwepo yalipomfikia Yaqub mauti, akawaambia wanawe, ‘Mtamuabudu nani baada yangu?’ Wakasema, ‘Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is’haq, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake.’” [Qur’an, 2:133].

Katika Ramadhan ya mwaka huu, bila shaka, wazazi wamekuwa na matarajio ya watoto wao kufunga kwa mara ya kwanza, au wakilazimika kufunga kwa mara ya kwanza.

Wakati mtoto anapofikia umri wa baleghe, anawajibika kutekeleza maamrisho ya Kiislamu, ikiwemo kufunga mwezi wa Ramadhan. Hii mara nyingi inaleta mgogoro ndani ya jamii inayowadekeza vijana na kuwaona hawana uwezo wa kufanya maamuzi, achilia mbali kushika nafasi za uongozi na kubeba majukumu mazito.

Uislamu una mtazamo tofauti kabisa kuhusu vijana na uwezo wao. Maisha ya Maswahaba yana mifano mingi ya vijana walioshika nafasi kubwa za uongozi na kupata mafanikio ya kupigiwa mfano.

Mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu alikuwa mtoto, Ali bin Abii Talib (Allah amridhie). Yeye aliukubali Uislamu akiwa na miaka 10 tu na aliandamana na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kusali kwa njia ya siri.

Ali alimkaribisha Abu Dhar al-Ghifariy Makka alipokwenda kumchunguza Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa siku tatu na kwa siri alimuongoza mpaka Dar ul Arqam ambako aliukubali Uislamu. Hata hivyo, kitendo chake cha kijasiri zaidi kilikuwa kulala kwenye kitanda cha Mtume wa Mwenyezi Mungu wakati wa usiku wa Hijra, akijua wazi kundi la wauaji liko nje, likiwa na silaha tayari kwa kushambulia.

Baada ya maumivu ya kifo cha Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), wakati wanafiki walipokuwa wanapanga njama Madina, na Mabedui wakifanya uasi katila eneo la Arabuni, Usama bin Zayd, aliongoza jeshi la Maswahaba waandamizi kupambana na Warumi, akiwa na umri wa miaka 17 tu. Si tu aliongoza msafara wa kivita bali pia aliibuka mshindi, akiwa Jenerali wa kwanza Muislamu kuwashinda Warumi, na hivyo kusafisha njia ya Waislamu kuelekea Syria na Misri. 

Tunakumbuka pia kisa cha vijana wa pangoni, ambao walikimbia mateso na udhalilishaji ili kuhifadhi dini yao. Allah Ta’ala amewaelezea kuwa walikuwa na Imani kwa Mwenyezi Mungu. Naye (Allah Ta’ala) aliwaongoza.

Hata hivyo, sifa ya kwanza watu wa
pangoni ni ‘ujana’:
Sisi tunakusimulia habari zao kwa haki. Hakika wao walikuwa ni vijana waliomuamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uongofu.” [Qur’an, 18:13]. Ujana unaweza kuwa hatua muhimu zaidi katika maisha ya mtu, ambapo hujengwa tabia na mitazamo itakayoweka mwelekeo wa mtu katika maisha yake yote. Ujana ni hatua yenye vishawishi na matamanio makubwa, ikichochewa zaidi na
‘hormones’ na kupungua kwa hali ya kutoogopa kufanya mambo ya hatari (risk).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close