10. Ramadhan

Tukiwa tunaelekea Ramadhan, tuijue Qur’an-2

Qur’an kukusanywa wakati wa Khalifa Abubakr

Baada ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kuondoka duniani, Maswahaba hawakuona haja ya kuiweka pamoja Qur’an kama kitabu kimoja mpaka yalipozidi mauaji ya Maswahaba waliyoihifadhi katika Vita vya Yamama au maarufu kwa jina la Vita vya Waasi.

Inasemekana kwamba, katika vita hivyo waliuawa Maquraa, wasomi wa Qur’an 70. Hilo lilimshtua Umar na akaogopa kupotea sehemu kubwa ya Qur’an, na ndipo alipoamua kwenda kumshauri Khalifa Abubakr atoe amri ya kukusanywa Qur’an.

Kadhia hii anaisimulia Zaid bin Thabit (Allah amridhie) aliposema aliitwa na Abubakr baada ya mauaji ya Alyamama. Alipofika, alimkuta pia Umar. Khalifa akamwambia Zaidi: “Umar amenijia na kuniambia, ‘Vita vya siku ya Yamama vimeua wengi na nachelea yasije yakaendelea mauaji ya wataalamu katika vita vijavyo ikajakupotea sehemu kubwa ya Qur’an. Kwa hiyo nashauri kuikusanya pamoja.’ Nikamwambia, ‘Kwa nini tufanye jambo ambalo Mtume hakulifanya?’ Umar akasema, ‘Sawa lakini Wallahi hili jambo la kheri (lina maslahi makubwa kwa umma).’”

Khalifa anazidi kunukuu alichosema Khalifa Abubakar siku hiyo mbele yake na Swahaba Mtukufu Umar: “Umar amekuwa akinikariri mpaka Allah amefungua kifua change, na nimeona kifanyike kile alichokiona Umar. Sasa wewe (Zaid) ni kijana mwenye akili nzuri ambaye hatuna mashaka nawe. Pia ulikwa ukiandika Wahyi zama za Mtume. Kwa hiyo ifatilie Qur’an na uikusanye pamoja.”

Zaid anasema: “Wallah, lau wangenipa jukumu la kuubeba mlima lisingelikuwa zito zaidi kwangu kuliko jukumu la kuikusanya Qur’an. (Licha ya hayo) basi nikaifatilia Qur’an nikiikusanya kutoka kwenye ngozi, makozi ya mtende na kwenye vifua vya watu, mpaka nikazikuta Aya za mwisho wa Sura ya Tauba (128-129) kwa Abuu Khuzaima al-Answaary. Sikuzikuta (Aya hizo) kwa mtu mwengine yoyote.” [Bukhari].

Namna ya ukusanyaji wa Zaid
Ukusanyaji wa Zaid ulikuwa kwa mitindo miwili kama ilivyoashiriwa katika simulizi yake mwenyewe: Kwanza ni kutoka kwenye vifua vya watu. Pili, ni ile iliyokuwa imeandikwa kwenye vifaa mbali mbali. Pia, Zaid hakuwa akiandika Aya ama sura kutoka kwa mtu yoyote ila kwa kushuhudia mashahidi wawili waadilifu.

Imamu Abuu Daud amepokea kutoka kwa Yahya bin AbdirRahman bin Hatib kwamba amesema: “Alikuja Umar mbele za watu akasema, ‘Mtu yoyote aliyewahi kupokea sehemu yoyote ya Qur’an kutoka kwa Mtume na ailete hapa.’ Watu wakaleta walichokihifadhi mpaka ikazingatiwa kwamba mtu wa kwanza kuikusanya Qur’an alikuwa Abubakr.” [Taz: ‘Albayan fii uluumil-Qur’an’ uk. 199-200].

Pia Hisham bin Urwa amepokea kutoka kwa baba yake kwamba alisema: “Abubakr alimuamrisha Umar na Zaid wakae kwenye mlango wa msikiti na kuwaambia (watu), ‘Atakayekujieni na mashahidi wawili watakaotoa ushahidi kwa chochote katika Qur’an basi iandikeni.’” (Abuu Daud).

Hii ndiyo namna ya ukusanyaji Qur’an uliofanywa na Abubakr.
Ilikuwa ni kuitoa sehemu tofauti ilikokuwa imehifadhiwa na kuiweka katika sura ya kitabu ama Msahafu. Msahafu ulipokamilika ulihifadhiwa nyumbani kwa Khalifa Abubakr (Allah amridhie).

Msahafu huo ulibaki huko mpaka alipofariki. Kisha ulihifadhiwa katika nyumba ya Amirl-Muuminin Umar katika kipindi chake chote hadi kufa kwake. Licha ya watu kuendelea kuisoma Qur’an kwa mujibu wa hifadhi walizokuwanazo, msahafu wa Abubakr ulibaki kuwa rejea yao hadi mwanzoni mwa ukhalifa wa Swahaba Mtukufu Uthman.

Ali (Allah amridhie) asifu juhudi za Abubakr
Khalifa wa nne katika Uislamu, Ali bin Abii Twalib, (Allah amridhie), alisema: “Abubakr amezitayarisha sahifa ambazo alikusanya ndani yake Qur’an baina ya magamba mawili.” [Fadhail alQur’an uk. 23].

Katika mahala pengine alisema Ali (Allah amridhie): “Mtu anayewazidi watu wote kwa ujira katika kushughulikia Msahafu ni Abubakr. MwenyezI Mungu amrehemu Abubakr. Yeye ndiye mtu wa kwanza aliyeikusanya Qur’an.” [Taz: Mabaahith fii uluum Alqr-n uk. 128].

Ni nani Zaid bin Thabit?
Baada ya Abubakr kuridhishwa na hoja za Umar zenye nia njema, tumeona kwamba jukumu la kuifatilia Qur’an na kuikusanya pamoja alikabidhiwa Swahaba Zaid bin Thabit. Labda msomaji angelitaka kujua nafasi ya Swahaba huyu mtukufu mpaka kufikia kuaminika kuyafuatilia maneno matakatifu ya Allah.

Zaid ni kijana wa Kianswari, msomi na mwelewa. Mtume alipofika Madina, Zaid bin Thabit alikuwa kijana wa miaka 13, hivyo alizuiliwa kushiriki katika Vita vya Badr. Mama yake ambaye aliitwa Nawwar binti Malik, alisikitika sana kwani alikuwa akitamani kumuona mwanawe amefauatana na Mtume katika vita hiyo ya Jihad.

Baada ya kuikosa nafasi hiyo, Zaid na familia yake waliitafuta nyanja nyengine tukufu nayo ni elimu. Alipenda ajipinde katika kuhifadhi Qur’an, hivyo alimuelezea mama yake fikra hiyo, naye (mama yake) aliwaeleza jamaa, wanaume, katika familia yao. Jamaa zake wakampeleka kwa Mtume na kumueleza nia ya mtoto wao.

Jamaa wa Zaid walimwambia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie: “Mtoto wetu huyu amehifadhi sura saba katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, na anajua kusoma na kuandika, basi angependa awe karibu nawe. Kama ukipenda, unaweza kumsikiliza. Mtume akamsikiliza Zaid akisoma baadhi ya sura alizozihifadhi, akamkuta ni mahiri wa kuitamka Qur’an na kwamba kisomo chake kinamuathiri (Mtume) kweli kweli.”

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alifumrahia sana kijana Zaid, akamtazama na kumwambia: “Zaid nataka ujifunze kwanza jinsi ya kuandika Kiyahudi…” Zaid akasema: “Labbayka Yaa Rasuulallah.” Zaid alijifunza na kukijua Kiyahudi kwa siku chache mno, kisha akajifunza lugha nyengine ya kigeni, akawa sasa ni mkalimani wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) [Taz: ‘Suwarun min hayat swahaba’ uk. 363-364].

Zaidu kuchaguliwa rasmi na Mtume kuwa muandishi wa Qur’an
Mtume alipogundua kuwa Zaid ana vipawa vya akili pevu, uwelewa (thaqafa) na uaminifu, alimteua kuwa miongoni mwa makarani wake. Basi kila ilipoteremka Aya ama Sura, alimuita na kumwambia: “Haya, andika ewe Zaid.” Akawa anaipokea Qur’an kutoka kwa mwenyewe Mtume mbichi mbichi ikiambatana na sababu za kushuka kwake.

Mara kijana akawa mahiri zaidi katika Qur’an na kuzama huko hadi akawa rejea ya kwanza ya umma wa Muhammad (rehema na amani za Allah na amani zimshukie) katika Qur’an baada ya kufa kwake. Nafasi hii kwa upande wa kitabu cha Allah ndiyo iliyowafanya Makhalifa kumuheshimu sana na kumchagua Zaid aifanye kazi ya kuikusanya Qur’an.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close