-1. Habari2. Taifa

Wazanzibar wasaka tiba, matokeo ya kidato cha sita

Mfululizo wa matokeo mabaya ya mitihani ya kitaifa huko Zanzibar umezua maswali na mjadala mkubwa, ambapo mbunge wa jimbo la Malindi Zanzibar Ally Saleh amesema anataka kuitisha mjadala wa kitaifa kujadili hali ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Ally Saleh ambaye alikuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba ya Warioba, amesema kuwa, ni fedheha kwa Zanzibar kuendelea kufanya vibaya katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.

Maneno ya mbunge huyo yanakuja kufuatia Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita 2019 ambapo shule nne za Zanzibar zimetajwa kuwa miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya zaidi kitaifa.

Shule hizo ni Kiembesamaki A, Islamic, Mpendae, Tumekuja na Haile Selassie -zote zikiwa za mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar. “Ni aibu kwa mara nyengine tena shule nne za Zanzibar zimo katika kapu la shule 10 za mwisho kwenye mtihani wa kidato cha sita mwaka huu,” alisema Ally Saleh na kuongeza: “Mimi nitaanzisha move (hatua) ya mjadala.”

Huo ni muendelezo wa matokeo mabaya huko visiwani kwani takwimu za NECTA kwa miaka mitatu nyuma zinaonesha kuwa kwa takribani miaka minne mfululizo shule za huko zimekuwa zikifanya vibaya katika mitahani ya kitaifa, hususan ile ya kidato cha sita.

Mathalani, takwimu zinaonesha katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2016 shule saba katika shule 10 zilizofanya vibaya zilitoka Zanzibar, mwaka 2017 ziliingia shule nne, mwaka 2018 shule mbili na mwaka huu shule nne. Wakati shule hizo zikijitokeza mkiani, haijawahi kutokea shule ya Zanzibar kutokea katika shule 10 bora za kitaifa.

Pia kwa mujibu wa matokeo ya kidato cha nne, mwaka 2017 shule sita za Zanzibar zilikuwa miongoni mwa 10 zilizofanya vibaya zaidi kitaifa, huku nne kati ya hizo zikiwa mkiani kabisa. Mwaka 2018, idadi hiyo ilipungua kwa nusu, yaani tatu ziliingia katika shule 10 dhaifu zaidi.

Utafiti wa LHRC
Wakati Ally Saleh akiazimia kuitisha mjadala huo, tayari sababu mbalimbali zimekuwa zikitajwa kupelekea ufaulu duni. Mathalani, ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2017 ilinukuu majibu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar (MoEVT) yakiorodhesha sababu kadhaa za matokeo mabaya visiwani humo.

Miongoni mwa sababu hizo ni ukosefu wa walimu mahiri wa masomo ya sayansi na hisabati, ukosefu wa nyenzo za kufundishia zikiwemo maabara, mazingira yasiyo rafiki ya kufundishia ambapo darasa moja huchukua wanafunzi wengi. Kwenye suala hili la msongamano darasani, gazeti la The Citizen la Desemba 25 mwaka jana linasema, darasa moja katika baadhi ya shule Zanzibar, linaweza kuchukua wanafunzi hadi 150. Sababu hizi zote zinatajwa kusababisha changamoto kubwa katika utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi Zanzibar.

Utafiti wa Oxford Policy Management
Utafiti uliofanywa na Oxford Policy Management kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Idara ya Sera, Mipango na Utafiti (DPPR) ya Wizara ya Elimu na Amali Zanzibar (MoEVT), chini ya anuani: “Zanzibar Education Situational Analysis” uliotolewa January, 2016, unautaja udhaifu mwingine wa elimu ya Zanzibar kuwa ni msingi mbovu wa elimu katika ngazi za chini.

“Kiwango cha elimu hasa kwa ngazi za shule za msingi na sekondari za kati (O’level) kipo chini. Wanafunzi wengi hawapati ujuzi na maarifa kama inavyoelezwa na mitaala ya elimu, kiasi kwamba zaidi ya asimilia 20 ya wanafunzi huingia kidato cha kwanza wakiwa wamefeli darasa la saba,” utafiti huo unaonesha.

Utafiti huo unabainisha kuwa hali hiyo imesababisha wanafunzi wengi kutofaulu kidato cha pili na hata cha nne na hivyo kuzalisha matokeo mabaya katika ngazi za juu za elimu. Pia utafiti huo kama ulivyo wa LHRC, nao unagusia suala la msongamano darasani na hivyo kuathiri maendeleo ya wanafunzi kitaaluma.

Wadadisi wa mambo
Nayo maoni ya baadhi ya wachambuzi na wadau mbalimbali, kwa upande mmoja yanakubaliana na utafiti wa LHRC na huo wa Oxford Development, lakini mengine yanaenda mbali kwa kuwanyooshea kidole cha lawama wanafunzi.

“Baadhi ya wanafunzi visiwani Wazanzibar wamekuwa hawayatilii maanani masomo huko skulini, wanafanya uzembe kiasi kwamba ndio tunapata matokeo hayo ambayo hayapendezi machoni mwetu,” alisema Mussa Makame mkazi wa Meya, Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwandishi na mhariri mkongwe, Jabir Idrissa amesema ukosefu wa ajira kwa walimu kumesababishia baadhi yao hasa wale wenye weledi kwenda sehemu nyingine kusaka ajira. “Walimu kadhaa hawajaajiriwa ndio maana siku hizi wakimaliza shahada vyuoni wanachupia fursa Tanganyika (Tanzania bara). Ninawajua vijana wawili watatu wakiwemo wa kike wameajiriwa huko,” alisema Idrissa.

Jabir alisema, suala la baadhi ya wahitimu wa kada ya ualimu kushindwa kurekebishiwa mishahara na stahiki zingine, limekuwa na mkono katika matokeo duni huko visiwani.

“Ninamjua kijana mmoja mwalimu na mwaka sasa tangu amalize masomo ya shahada ya pili (Masters Degree) hajarekebishiwa mshahara wala kupangiwa pa kwenda kuendelea na kazi. Ameamua kurudi skulini kwake kufuta na kuandika,” alisema Jabir Idrissa.

Naye mwanadishi habari na mwanaharakati wa haki za binadamu, Salma Said alitilia shaka sifa za walimu wengi wanaofundisha huko Zanzibar akisema wengi wao hawana uzoefu na maarifa ya kutosha kufundisha wanafunzi.

Maoni hayo ya Salma yanashabihiana kwa kiasi fulani na Ally Khamis ambaye alitupia jicho mfumo wa upatikanaji wa walimu huko Zanzibar akidai kuwa umejaa kasoro.

“Tukichimbue hata namna wanavyopatikana walimu ni tatizo kubwa kwa Zanzibar. Miaka ya nyuma kidogo wanafunzi wenye division (madaraja) mbaya ndio walikua wanaangukia vyuo vya ualimu. Sasa hivi universities (vyuo vikuu) zinatoa degree (shahada) za ualimu. Lakini baada ya kuhitimu wanafunzi ajira ni tatizo na hata zikitolewa hazina mfumo maalumu,” alidai Ally Khamis.

Suala lingine ambalo Salma Said alilibainisha ni uzembe kwa baadhi ya taasisi zenye wajibu wa kusimamia elimu na kwa kuwa hakuna anayewajibika basi ndio imekuwa chanzo cha mfululizo wa matokeo mabaya huko visiwani.

“Kiukweli kiwango cha elimu kimeshuka sana Zanzibar na hii ni kutokana na uzembe na kukosekana kwa uwajibikaji kwa wale wanaohusika, ndio maana tunaendelea kuyashuhudia haya matokeo mabaya. Tusipochukua hatua, hali inaweza kuzidi kuwa mbaya,” alisema Salma Said.

Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar (MoEVT) alipopigiwa simu kutolea maelezo suala hilo, alisema asingeweza kuongea kwenye simu na pia yupo katika kikao kwa muda huo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close