-

Wanazuoni: Wakfu mkombozi wa Waislamu

Imebainishwa kuwa uwekezaji na matumizi mazuri ya mali za Wakfu ni miongoni mambo yatakayosaidia kukabiliana na hali duni za kwa Waislamu wengi hapa nchini, kwa uapnde wa afya, elimu, uchumi na kadhalika.

Wakijadili suala la Wakfu na manufaa yake hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Delhi Darbar jijini Dar es Salaam, wadau wa masuala ya Wakfu wa Kiislamu wamesema kuwa mali za Wakfu zimesaidia sana kukabili changamoto za Waislamu katika nchi ambazo kuna utaratibu mzuri wa kusimamia na kuratibu mali hizo.

Huko Afrika Kusini wamefanikiwa sana katika kukabili changamoto zao kwa kuwa wana utaratibu mzuri wa Wakfu, alisema mmoja wa wachangiaji Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya SSC Capital, Salum Awadh wakati akichangia mada katika mkutano huo ulioandaliwa kwa pamoja na Kituo cha Usimamizi, Ushauri wa Masuala ya Kifedha ya Kiislamu (CIFCA) na Taasisi ya Expedition Foundation na wadau wengine kadhaa.

Wenzetu Afrika Kusini wana utaratibu mzuri wa mali za Wakfu. Mapato na matumizi huwekwa hadharani hata ukiingia mitandaoni unaona. Hakika, mali za wakfu zimekuwa na tija kwa Waislamu,” alisema Awadh.

Naye, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Dhi-Nnureyn, Sheikh Shamsi Elmi alisema kuwa, Waislamu hapa nchini bado wanakabiliwa na matatizo mengi na kwamba, mali za Wakfu ni tiba ya kukabili hiyo. “Hali za Waislamu bado si nzuri sana kama kwenye afya, elimu, uchumi, hivyo kuna haja ya kuhakikisha mali hizo zinaratibiwa vema ili kusaidia kukabili changamoto zetu,” alisema Sheikh Elmi. Kwa mujibu wa Sheikh Elmi, Wakfu ina manufaa zaidi kuliko hata zaka katika maendeleo ya Waislamu.

“Wakfu ni madhubuti kuliko zaka kwani Wakfu haina kiwango maalum kama zaka na pia hakuna mipaka ya wanufaika kama ilivyo kwa Zakka,” alisema Sheikh Elmi. Pia aliongeza kuwa, mali za Wakfu zina uwezo wa kuwekezwa na pia ni mali ya umma tofauti na zaka ambayo husalia kuwa mali ya aliyepewa.

Naye mjumbe wa CIFCA, Dkt Kassim Hussein alibainisha kuwa kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa mali za Wakfuu kwani zimekuwa haziwanufaishi Waislamu badala yake zinawanufaisha wachache wanaozisimamia mali hizo. “Mali hizi za Wakfu ambazo zipo mikononi mwa baadhi ya taasisi na misikiti zimekuwa zikiwanufaisha wachache, tena wale waliokabidhiwa kuzisimamia,” alisema Dkt. Hussein.

Aidha, Dkt. Hussein alidai kuwa baadhi ya mali hizo zimeuzwa huku baadhi yake zikinunuliwa na watu waliokabidhiwa kuzisimamia kwa bei karibu na bure jambo ambalo alisema linatia aibu. Kwa upande wake Sheikh Muhammad Issa ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Sunna Tanzania(BASUTA), amesema ipo haja ya elimu ya Wakfu kutolewa kwa Waislamu wengi hapa nchini ili wajue umuhimu wa kutoa Wakfu, masharti yake na faida zake.

Mali za Wakfu
Mali za Wakfu huhusisha vitu kama ardhi, mashamba, majengo, viwanja. Wakfu inaweza kufaidisha makundi watu wote kwa ujumla au makundi maalum kama wanyama (kulishia), walemavu na pia katika masuala ya ndoa (kuwezesha vijana kuoa).

Akidadavua zaidi kuhusu mali hizo za Wakfu, Katibu Mkuu wa BASUTA, Sheikh Shaaban Mussa alibainisha kuwa ni pamoja na kupanda miti ya matunda iliwasaidie watu na wanyama. “Waislamu tunapaswa tufahamu kuwa Wakfu ni pamoja na kupanda miti, kwani hii inasaidia watu na hata wanyama, lakini siku hizi watu tunapanda zaidi miarobaini,” alisema Sheikh Shaaban Mussa.

Ili kufanikiwa katika suala hilo la Wakfu, Mwenyekiti wa Taasisi ya kuhifadhisha Qur’an nchini, Sheikh Othman Kaporo amesema kuwa Ikhlas ni muhimu sana. “Waislamu tuwe na Ikhlas, tukiwa na Ikhlas ya kweli tunaweza kufanya miujiza kupitia mali za Wakfu” alisema Sheikh Kaporo.

Uzoefu wa nchi nyingine
Aidha, mifano mingine kuhusu manufaa ya mali za Wakfu imekuwa ikitajwa kuwa ni nchi za Uturuki, Morocco, Kenya, Malaysia na kadhalika. Akizungumzia uzoefu wa Kenya na Morocco, Mwenyekiti wa Tume ya Wakfu nchini Kenya Sheikh Zubeir noor Hussein, huko nyuma aliwahi kubainisha kuwa wao Kenya wanazaidi ya miaka 100 katika masuala ya Wakfu huku mali hizo zikisaidia Waislamu wengi.

Sisi kwetu Kenya hakika tuko mstari wa mbele katika mambo haya kwa muda wa zaidi ya miaka 100, tuna changamoto zetu lakini zaidi ya hayo tumepiga hatua kubwa na kwa sasa tunapitia upya sheria yetu ya Wakfu iendane na katiba ya sasa,” alisema Sheikh Hussein.

Kwa upande wa Morocco alisema: “Nchi kama Morocco ina misikiti zaidi ya elfu 70 ambayo iko chini ya Wakfu na wana ekari zaidi ya elfu 80 za ardhi ambazo ziko chini ya Wakfu ya kule. Income (mapato) yao sasa hivi ni takribani dola milioni 150 kwa mwezi (shilingi bilioni 344.25. Akiba ya fedha yao sasa hivi ni dola milioni 550 (shilingi trilioni 1.26).”

Na huko Uturuki, ambako mambo ya Wakfu yapo tangu enzi za dola ya Ottoman, yanatajwa kuwanufaisha Waislamu wengi kwenye kusaidia ajira, elimu, afya na masuala mengine ya kijamii. Pia, huko Uturuki kumekuwepo na utaratibu wa kuandika majina ya watu wanaotoa mali za Wakfu ili kuwatambua na kuwaenzi na Wakfu hizo ndizo zinazohudumia Masjid Aqsaa hadi leo.

Wakfu kwa kina! Wakfu ni neno la Kiarabu linalotokana na neno “Waqafa” kwa maana ya kuzuia, kusimamisha, kufanya kitu kisiende au kisiondoke. Wakfu ilianza tangu zama za Mitume na Manabii. Kwa mfano, Mama yake Maryam bint Imran, yaani bibi yake Nabii Isa (amani ya Allah ismhukie) aliweka nadhiri kumfanya mtoto wake awe Wakfu kwa Allah.

Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) alihimiza Maswahaba kutoa mali za Wakfu na ndipo Swahaba Uthman bin Affan alipoamua kununua kisima kutoka kwa Myahudi aliyekuwa akiwauzia maji wakazi wa Madina. Baada ya kukinunua, Uthman alitoa Wakfu kisima hicho ili watu wachote mai bure. Kisima baada ya kununuliwa kilikuja kujulikana kama Bi’r Uthman.

Umar bin Khattwaab naye alitoa kiunga chake cha mitende kule Khaybar kuwa Wakfu ambapo mazao yake yaliuzwa na fedha zilizopatikana kutumika kwa ajili ya Allah. Historia nzima ya Uislamu imejaa matukio ya watu wema kutoa mali zao Wakfu zama zote huku mali hizo zikifikia kilele chake zama za ukhalifa wa Waturuki ambapo ilifika hadi nusu ya mali katika baadhi ya miji ni mali za Wakfu tu.

Kupitia mali za Wakfu, Waislamu waliendesha huduma mbali mbali za jamii kama vile kusimamia misikiti, vyuo kama vile Khayrawan, Al Azhar na Cordoba nchini Hispania, na vilevile mali za Wakfu zilitumika kuhudumia hospitali, yatima, wajane na wazee wasiojiweza. Hapa nchini, Zanzibar kuna Kamisheni ya Mali za Wakfu na Amana ambayo husimamia mali za Wakfu Zanzibar. Lakini Tanzania bara hakuna chombo kama hiyo ingawa kuna taasisi mbalimbali zinazomiliki mali za Wakfu. Miongoni mwa mali za Wakfu zinazomilikiwa na taasisi

Show More

Related Articles

Back to top button
Close