-

Waislamu watakiwa kuwekeza sekta ya elimu

Wadau wa elimu hapa nchini wametakiwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu ili kuwawezesha vijana kupata elimu bora inayoendana na matakwa halisi ya ulimwengu wa leo. Wito huo umetolewa na Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Pazi Mwinyimvua wakati wa mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne na elimu ya awali katika shule za Yemen DYCCC, ziliopo eneo la Chang’ombe, manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam.

Dkt. Pazi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo alisema, elimu ndio msingi wa maisha ya mwanadamu hivyo Waislamu hawana budi kutumia uwezo wao wa kifikra na kimali kuwekeza katika sekta ya elimu.

Nabii Adam (amani iwe juu yake) alianza kufundishwa majina ya vitu vyote na baadae kupokea muongozo kutoka kwa Mola wake. Hii ina maana kuwa, ili mwanadamu aweze kukabiliana vema na changamoto za kimaisha hana budi kujifunza elimu ya dini na ile ya mazingira,” alisema
Dkt. Pazi na kuongeza:

Uislamu umehimiza elimu zote zenye manufaa bila ya kuchagua, hivyo vijana wanapaswa kujengewa misingi bora ya kujitafutia elimu.

Zaidi, Pazi aliwataka waasisi wa shule hiyo ya Yemen kuongeza juhudi sambamba na kumtegemea Mwenyezi Mungu katika jukumu la kuiongoza shule.

Kujitolea kwenu huduma ya elimu hakupotei bure, bali mnajiwekea akiba kwa Mwenyezi Mungu kwani huko ndiko kuipigania dini yenu,” alibainisha Pazi.

Dkt. Pazi alisema ili vijana wapate elimu bora na yenye manufaa, walimu na wazazi ni lazima wazingatie misingi ya elimu bora ikiwamo kuwa na majengo bora, vitendea kazi pamoja na walimu wenye moyo wa kujituma.

Ili kuyafanikisha hayo, Pazi aliwataka wamiliki wa shule hizo za Yemen kuwajali na kuwathamini walimu wao kwa kuwapa motisha ikiwa ni njia ya kuwahamasisha kufanya kazi kwa ufanisi.

Akizungumzia wajibu wa mwalimu wa kiislamu, Pazi alisema walimu wana wajibu wa kutumia vizuri taaluma wanazozipata, kuchunga kanuni na misingi ya kazi yao, na kuhakikisha yale wanachofundisha kinawafikia wanafunzi.

Aidha Pazi, alitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya DYCCC inayomiliki shule za Yemen kwa kuweka mazingira mazuri ya kusomea na hivyo kuwafanya watoto wawe na hamu ya kusoma. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya shule za Yemen, Hassan Akrabi aliwataka wahitimu kuzingatia yale waliyofundishwa na kuyafanyia kazi.

Akrabi alisema uongozi na walimu wa shule hiyo umejizatiti vya kutosha kutoa elimu bora na kuwalea wanafunzi katika maadili ya dini ili wawe viongozi bora wa baadae. Naye, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hamisi Togwa alisema, Yemen DYCCC ni miongoni mwa shule zenye wastani wa kati na zinazoendelea kufanya vizuri katika ngazi ya wilaya, mkoa, kanda na taifa tangu kuanzishwa kwake.

Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 95 wa elimu ya awali na 65 wa kidato cha nne walihitimu masomo yao kwa mwaka huu wa 2018.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close