-

Waislamu tumeridhia walimu kudhalilika?

Wiki iliyopita nilihudhuria ibada ya sala ya Ijumaa katika moja ya misikiti iliyo jirani na eneo ninaloishi. Baada ya kumalizika sala, Imam alisimama na kuwahamasisha Waumini kuchangisha fedha shilingi laki moja kwa ajili ya kumlipia pango ya nyumba mwalimu wa madrasa iliyopo msikitini hapo.

Hii si mara ya kwanza kwa Waumini wa msikiti huo kuombwa kuchanga fedha kwa ajili ya mwalimu. Mara kwa mara Khaatib wa sala ya Ijumaa amekuwa akitoa rai ya kumchangia mwalimu sanjari na kumpa mtaji wa kuanza biashara ili aweze kuepukana na changamoto ya kifedha inayomuathiri vibaya kisaikolojia.

Changamoto inayomkabili mwalimu huyu wa madrasa inawakabili walimu wengi huku baadhi yao wakikosa ajira, na hivyo kuishi kwa kutegemea ada za wanafunzi na sadaka za wafadhili ambazo hata hivyo hazikidhi mahitaji yao hata kidogo.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, ni vigumu kwa walimu hawa kupata taasisi za Kiislamu zinazoweza kuwapatia mikopo au mitaji kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, jambo linalofanya umasikini kubaki kuwa changamoto kubwa katika harakati zao za kujikomboa kiuchumi.

Wengi wa walimu hasa wale ambao hawakosekani madrasa wanaishi kwa kubangaiza, kuanzia kula yao, vaa yao na hata kulala hasa kwa wale wanaoishi katika nyumba za kupanga. Walimu na familia zao wanavyopata shida ni kana kwamba hawapaswi kuwa na maisha mazuri kama ilivyo kwa watu wengine.

Wengi wanawaona walimu hawa kama watu madhalili wanaopaswa kuwafundisha vijana masuala ya dini lakini hawapaswi kuthaminiwa muda wao wanaoutumia. Ni aibu kuwaona walimu wa madrasa pamoja na familia zao wakiishi kiudhalili, wakati kuna matajiri wengi wa Kiislamu ambao hutumia neema ya mali waliyopewa na Mwenyezi Mungu katika mambo yasiyo na manufaa na dini huku wengine wakiishia kufadhili mashindano ya muziki, ulimbwende (umiss), soka na mambo mengine ya kishetani.

Wakati watu hawa wanatumia neema ya mali kusaidia mambo yaliyoharamishwa, inaonekana hakuna wa kuthubutu ama kudiriki kuwaonya wasifanye hivyo. Ukweli ni kwamba mtu hawezi kuacha maovu bila ya kumhofu Allah kama alivyosema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Hawi mtu ni katika wenye kumcha Allah mpaka aache hata lisilokuwa na ubaya kwa kuogopa kufanya lenye ubaya.” [Tirmidhiy].

Hadithi hii inatufunza juu ya kuyawajibikia mambo ya kheri ikiwamo kuwaunga mkono na kuwasaidia walimu wa madrasa kwani wameacha shughuli zao mbalimbali kwa sababu tu ya kuihudumia dini ya Allah.

Hata tusiposema kwa vinywa, vitendo vinavyooneshwa na baadhi ya Waislamu na jamii kwa ujumla vinatafsiri namna walimu wa madrasa walivyowekwa katika kundi la watu wasiothaminiwa na kutazamwa kwa jicho makini. Hii ni dhana potofu ambayo inapaswa kupuuzwa.

Pamoja na juhudi kubwa za walimu wa madrasa za kuwalea vijana wa Kiislamu katika maadili ya dini, ni watu wachache mno wanaotambua kwa dhati mchango wao na hata kuwafariji kwa kuwatembelea na kuwasaidia, hali inayowafanya watu wengi kuendelea kuwapuuza walimu hawa wanaofundisha maadili katika jamii. Ni walimu wa jamii kwa sababu athari za mafunzo yao zinatumika katika maisha ya kila siku.

Inasikitisha kuona walimu wengi wa madrasa hawana malipo ya kweli ambayo yanaweza kuwainua kiuchumi. Wengi wao wanaishi maisha ya hohehahe licha ya kuwapo taasisi lukuki zenye uwezo wa kufanya ukombozi mkubwa wa kiuchumi katika maisha yao.

Ada tunazoaminishwa kuwa ndio malipo ya mwezi ya walimu, kiwango chake ni kidogo mno na bado wenye dhamana ya kulipa (wazazi na walezi) hawalipi na hata wanaolipa hawafanyi hivyo kwa wakati muafaka.

Kwa kuzingatia hayo yote, walimu kupitia jumuiya na taasisi zao wanapaswa siyo tu kujadili na kulalamika kuhusu kujikomboa kiuchumi bali waanze kuchukua hatua wenyewe kwa sababu wanaopaswa kuwatazama wamefunika macho yao kwa
vitambaa vyeusi.

Si kweli kwamba hakuna wadau wanaoweza kuwakomboa walimu wa madrasa kwani sote tunafahamu kuwa ndani ya nchi hii kuna idadi kubwa ya matajiri wa Kiislamu, kuna taasisi pamoja na jumuiya nyingi za Kiislamu na pia wapo wazazi, walezi na Waislamu mmoja mmoja wenye uwezo wa kusikiliza kilio cha walimu wa madrasa hapa nchini.

Ni ukweli usiofichika kuwa walimu wa madrasa wanatakiwa kuwezeshwa ili waweze kujikomboa kiuchumi na hatimaye waishi kwa kujiamini badala ya kutegemea kuombaomba au sadaka ambazo hazikidhi mahitaji yao ya kila
siku.

Hili haliwezi kushindikana kwa sababu walimu hawahitaji kufadhiliwa bali wanataka kukombolewa ili waweze kusimama wao wenyewe. Wao wanatambua fika kuwa ipo siku ufadhili utakwisha hivyo kama wataimarika kiuchumi hapatakuwa na adha ya kusaka wafadhili wa maisha yao.

Uwepo wa walimu wa madrasa ni hitaji tosha katika jamii kwani mbali na kuwapatia elimu ya dini vijana na watoto wa Kiislamu na pengine hata watu wazima, pia walimu hawa wanashiriki katika shughuli zao mbalimbali za kijamii kama vile mazishi, ndoa na kadhalika.

Suala kubwa linalokwamisha suala la kuwakomboa walimu hawa, ambao wanaonekana dhalili mbele ya jamii ni kukosekana watu wa kuwatazama. Walimu wengi kama siyo wote wa madrasa za mjini na vijijini wanaishi kinyonge kama si kiujanjaujanja. Wanajaribu kujichanganya kwenye kilimo, biashara na shughuli mbalimbali lakini kinachowagharimu ni hali zao za kiuchumi kuwabana kwani shughuli wanazozifanya haziwasaidii kujikomboa.

Laiti wangewezeshwa, bila shaka wangefanya shughuli zao kwa ufanisi huku wakitekeleza majukumu yao ya kuwapatia elimu ya dini watoto na vijana wetu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close