-

Waathirika wa vita Yemen wachangiwa

TV Imaan yaonesha tukio ‘live’

Zaidi ya shilingi milioni 15 zimekusanywa kwa ajili ya waathirika wa vita ya Yemen katika matembezi ya hisani, kati ya hizo zikiwemo ahadi na fedha taslimu. Katika harakati hiyo ya kukusanya fedha, taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) ikichangia shilingi milioni mbili huku vyombo vyake vya habari vya Imaan ikishiriki kikamilifu kwa siyo tu kuhamasisha uchangiaji bali pia kurusha tukio moja mubashara. Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi akiongea kandoni mwa hafla hiyo amesema ameguswa na hali ya wananchi wa Yemen na kuwa TIF itaendelea kuchangia zaidi.

Pia Nahdi amesema kuwa kuna kila haja ya watu binafsi na taasisi hapa nchini kuchangia wananchi hao wa Yemen wanaoishi kwenye madhila. Naye Mwenyekiti wa TYPF, Ally Abdallah amesema uchangiaji huo utaendelea mpaka Mwezi wa Ramadhan huku akiishukuru TIF kwa kurusha mubashara hafla hiyo ya uchangiaji.

Kauli ya mgeni rasmi
Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi, Balozi wa Yemen hapa nchini, Dkt. Fikry Talib Al-Saggaf amewapongeza waandaaji wa shughuli hiyo na kusema wamefanya jambo la kiutu kwani litawapa faraja waathirika wa vita hivyo. Aidha, Balozi huyo ameiomba jamii ya kimataifa kutoa misaada zaidi kwa Yemen ili kuwanusuru wananchi wakiwemo wanawake, wazee na watoto ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaoathirika zaidi.

Hafla hiyo ya uchangiaji iliyoratibiwa na kikundi cha watoto na wanawake cha Happy Hands kilichopo chini ya taasisi ya TYPF Foundation, iliambatana na matembezi katika eneo la Upanga jijini Dar es Salaam na kurushwa mubashara na vyombo vya habari vya Imaan. Akiongelea zaidi hafla hiyo, Kiongozi wa Happy Hands, Bi Yusra amesema kuwa, wameguswa na matatizo yanayowakumba wananchi wa Yemen na hivyo wakaamua kuendesha michango hiyo.

Kule Yemen kuna vita na wananchi wengi wanateseka, wana shida ya dawa, vyakula, ndio maana sisi tumeona tuchangishe ili kuwasaidia ndugu zetu wale,” alisema Bi Yusra na na kisha akatoa wito kwa Waislamu na Watanzania wengine kwa ujumla kujitokeza ili kuwasaidia waathirika hao wa Yemen kwa vitu mbalimbali kama nguo, dawa na vifaa vingine.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Dhi Nureyn Foundation ya mjini Iringa, Sheikh Said Abri amesema watu walio kwenye amani hawana budi kuwasaidia walioko kwenye matatizo. “Sisi tulioko kwenye amani tunapaswa kuwasaidia waliko kwenye vita, Yemen kule watoto na wanawake wanateseka mno, tunalazimika kuwachangia,” alisema Sheikh Abri.

Hali ya Yemen
Mwaka 2011 Yemen ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na hali ilizidi kuwa ngumu mwaka 2015. Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonesha kuwa tangu kuanza kwa vita hiyo zaidi ya watu 10,000 wameuawa na watu milioni tatu wamekimbia nchi hiyo.

Kuhusu njaa, UN inasema zaidi ya watu milioni nane wanakabiliwa na baa hilo huku kiasi cha dola milioni 50 kikiwa kimetolewa kukabili hali hiyo. Shirika la Umoja wa Kimataifa la Watoto Duniani (UNICEF) linasema kuwa zaidi ya watoto 10 wanakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa tiba, maji safi, elimu na chakula.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close