-

Utulivu wakati wa Swala ulinifanya niingie katika Uislamu- Chacha

 

Katika dini tukufu ya Uislamu kila ibada ina namna yake sahihi ya utekelezaji kutokana na mafundisho matukufu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wetu Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie). Uislamu ni mfumo wa maisha hivyo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka hajaacha kitu chochote bila kukielezea hukumu na namna ya utekelezaji wake.

Moja ya mafundisho ya Uislamu ni kutekeleza nguzo tano za Uislamu, ikiwemo ibada ya swala. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an: “Hakika wamefanikiwa waumini, ambao ni wanyenyekevu katika sala zao na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.” [Qur’an 23:1-3].

Leo katika makala ya aliyesilimu tunamzungumzia Emanuel Samwel Chacha (44), ambaye baada ya kusilimu anaitwa Abdulkarim Chacha. Chacha alisilimu miaka 20 iliyopita baada ya kuvutiwa na unyenyekevu aliouona kwa Waislamu wakati wa kufanya Ibada ya swala.

Chacha aliyezaliwa na kulelewa mkoani Singida ambapo mzazi wake alikuwa akifanya kazi, alikuwa akiabudu katika Dhehebu la Roman Catholic (RC). Akiwa katika imani yake ya zamani, alishapata mafundisho ya komunio na kipaimara miaka ya 1986 na 1987 Singida Mjini. Chacha anakumbuka hadi jina la askofu wake aliyeitwa Mabula. Kwa sasa, Chacha anaishi jijini Dar es Salaam akiwa ni baba wa watoto wawili.

Kusilimu kwake:

Kama tulivyodokeza, kilele cha uamuzi wa Chacha kusilimu ni utulivu na unyenyekevu aliouona kwa Waislamu wakati wa kufanya ibada, tofauti na hali aliyoiona alipokuwa katika imani yake ya awali.

Hata hivyo, Chacha anakumbuka kuwa, kabla hata ya kuvutiwa na unyenyekevu katika ibada za Waislamu, miaka miwili baada ya kupata Kipaimara, yaani mwaka 1989, alishaanza kujiuliza maswali kuhusu ibada aliyoifanya katika dini yake ya awali ya kuomba katika sehemu ambazo kuna sanamu.

Jambo hilo lilimsumbua sana kiasi kwamba akawa anamuuliza rafiki yake mmoja aliyeitwa Mohammed kuhusu namna ya kufanya ibada katika Uislamu, ili tu kulinganisha, ndipo rafiki yake alimueleza mengi kuhusu swala katika Uislamu, na kushangazwa na usafi wa eneo la ibada kiasi cha kutoingia na viatu eneo la msikitini.

Mwaka 1998 katika mwezi wa Ramadhani Chacha alisilimu, kwa tamko la shahada kuwa, “Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na Muhammad ni Mtume wake,” maneno ambayo alitamkishwa na mzee aliyefahamika kwa jina maarufu kama Mtengi.

Athari kwa ndugu zake:

Baada ya kusilimu, akiwa huko Singida, Chacha alianza kujifunza Uislamu na kutekeleza ibada za swala na funga. Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi Mlioamini jiokoeni nafsi zenu na watu wenu kutokana na moto ambao kuni zake ni watu na mawe, wanausimamia Malaika wakali wenye nguvu hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa amri zake na wanatenda wanayoamrishwa.  [Qur’an, 66:6].

Kusilimu tu kwa Chacha ilikuwa ni ulinganiaji tosha kwa wadogo zake wawili ambao nao walijiunga naye katika Uislamu. Hivyo, Chacha alitengeneza athari na kuwa sababu ya ndugu zake kuitambua haki na kuifuata. Allah azidi kuwaongoza.

Nasaha kwa Wasio Waislamu:

Alipoombwa kutoa nasaha zake kwa wasio Waislamu, Chacha alisema Mwenyezi Mungu ameridhia Uislamu kuwa dini ya kweli na haki, na Mtume wa mwisho kuwa ni Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), hivyo hamna sababu ya kupingana na hilo, zaidi ni kuukubali Uislamu na kufuata mafundisho aliyoshushiwa Mtume Muhammad.

Pia, Chacha alitoa rai kuwa, watu wafuate haki baada ya kuitambua.

Isiwe shida kwa mtu kuifuata haki baada ya kuitambua kwa sababu ya
kujali maslahi ya kidunia, iwe fedha au mali, anayoyapata kutoka katika
upande aliopo,” alishauri.

Hata hivyo, Chacha alisema mbadilishaji ni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Muumba wa mbingu na ardhi, na kwamba analotakiwa kufanya mwanadamu ni kutafuta ukweli na kumuomba Allah amuongoze katika kuifuata haki.

Ushauri kwa Waislamu:

Kwa upande wa Waislamu, Chacha alihimiza umoja, akitaja kuwa ni jambo muhimu. Alisema, licha tofauti za madhehebu, muongozo wa Waislamu wote ni Qur’an na Sunna za Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Kutokubaliana katika baadhi ya mambo kupo na hilo si suala geni katika Uislamu, lakini tunachotakiwa kufanya ni kuzungumza na sio kulumbana,” alisema na kuongeza kuwa, kwa kuzungumza tofauti zetu kistaarabu kwa nia ya kuitafuta haki, tutakuwa kweli tumemuiga Mtume.

“Tukionesha tabia njema tunaweza kuleta athari kubwa kwa watu kuingia katika Uislamu hata bila ya kumlingania kwa maneno,” alisema Chacha. Allah azidi kumuongoza Abdulkarim Chacha na amjaalie kizazi chema kitakachoutumikia Uislamu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close