-

Tuziunge mkono taasisi za dini kuwekeza sekta ya elimu

Miongoni mwa habari zilizowahi kuandikwa katika toleo la gazeti Imaan ni inayohusu taasisi ya Direct Aid yenye makao yake makuu nchini Kuwait ikisema kuwa itazidi kuwekeza kwenye sekta ya elimu hapa nchini na kwingineko duniani.

Zaidi, taasisi hiyo imesema kuwa, huwa inatumia asilimia 80 ya bajeti yake katika sekta hiyo, kama alivyobainisha Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dkt. Abdallah Al Subayt. Hii ni hatua muhimu sana kwa taasisi hiyo kwani inagusa miongoni mwa maeneo nyeti ya maendeleo ya jamii yoyote hapa duniani.

Hivyo tunaamini kwa dhati kuwa uwekezaji huo wa taasisi ya Direct Aid katika elimu pia ni faraja kwa Waislamu wengi hapa nchini ambao bado maendeleo yao ya elimu ni duni, wakijiuliza kila siku wataondoka kwenye hali hiyo.

Kadhalika, hizi ni jitihada nzuri za kusaidia maendeleo ya elimu kwa ujumla wake hapa nchini, kwani bado suala la elimu halijakaa sawa. Tukirejea kwa Waislamu, ni kweli Waislamu wengi wamewekeza katika elimu ila bado tunaona kuna changamoto kadhaa katika uwekezaji huo. Baadhi ya changamoto hizo hujitokeza pale yanaporudi matokeo ya mitihani ya kitaifa yakawa mabaya.

Pia, zipo changamoto katika uendeshaji. Hivyo tunaposikia taasisi ya Kiislamu inadhamiria kujikita kwenye elimu tunashawishika kusema hilo ni jambo la kutia faraja sana, tukiamini kwamba hatua hiyo itaongeza nguvu katika juhudi pana za Waislamu za kusukuma mbele elimu.

Na kutilia mkazo nukta hiyo, nasi tuzitolee wito taasisi zingine za Kiislamu zijitahidi katika kuhudumia masuala ya kielimu. Zifahamu kuwa kizazi bora cha Uislamu kitatokana pia na kupatia vijana wetu elimu. Wakati tukipongeza jitihada za Direct Aid na taasisi zingine za Kiislamu, pia tuwatolee wito wazazi na Waislamu kwa ujumla kushirikiana na taasisi hizo katika kupokea huduma hiyo.

Miongoni mwa jitihada hizo ziwe ni kupeleka watoto wao katika shule hizo ambazo zinatoa sio tu taaluma ya masomo ya mazingira bali pia maadili ya Kiislamu.Wazazi pia watoe ushirikiano kwa kulipa michango mbalimbali ili fedha itumike kuboresha uendeshaji.

Mara kadhaa zimesikika habari kutoka kwa baadhi ya walimu na wadau wa elimu nchini wakilalamikia hatua za baadhi ya wazazi wa Kiislamu kuzikimbia shule hizo kwa kigezo cha kutofaulisha vizuri. Aidha, walimu hao pia wamekuwa wakilalamikia wazazi kutolipa ada kwa wakati, na pia kutotoa ushirikiano wa kutosha pale wanapoitwa kujadili maendeleo ya watoto. Hilo sio jambo zuri kwani linakwamisha maendeleo ya elimu.

Mwisho tunapenda kutoa wito kwa wafadhili na wadau wengine kujitokeza katika kusaidia miradi ya elimu. Wenye kufanya hivyo watambue kuwa kujitolea kwao huko hakupotei bure, bali wanajiwekea akiba kwa Mwenyezi Mungu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close