-

Tushirikiane na walimu kuwaelimisha watoto

Ni ndoto ya kila mzazi kuona mtoto wake anafanya vizuri katika elimu, iwe ya dini au mazingira. Wazazi wengi hujinyima na kutumia rasilimali zao kufahakikisha watoto wao wanapata elimu bora. Hili ni jambo zuri na linalofaa kupongezwa. Hongereni sana wazazi. Endeleeni na moyo huohuo.

Lakini, wapo wazazi ambao wanaona suala la kumuelimisha mtoto ni kazi ya mwalimu. Mtoto anapofanya vibaya darasani, basi shutuma zote zinamwangukia mwalimu. Katika baadhi ya nyakati huwa kweli. Lakini, sio wakati wote mtoto anapofanya vibaya yafaa uwanyooshee vidole walimu.

Nimesikia na kusoma katika vyombo vya habari watu wakiwashutumu walimu. “Walimu wa siku hizi hawafundishi.” “Walimu hawana wito siku hizi.” Jamii inamhukumu mwalimu. Pengine wanazo hoja, lakini je, sisi kama jamii hasa wazazi, tunatekeleza wajibu wetu kufanikisha ufundishaji na ujifunzaji wa watoto wetu?

Nimeongea na walimu wengi kuhusu ushiriki wa wazazi katika taaluma za watoto. Walimu wengi wanakiri kuwa, hawapati ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wazazi. Baadhi walinieleza kuwa, ni jambo la kawaida mwaka mzima kupita bila mzazi kufika shuleni. Hii ni kusema kuwa hakuna mawasiliano wala ushirikiano wa karibu baina ya mzazi na shule. Wazazi wenzangu, je, hii ni sawa?

Ni wazazi hawahawa ambao kila wanapoitwa katika vikao vya shule hawafiki. Utasikia ‘nipo bize’ ‘Mtaniambia mtakachoamua nipo tayari.’ Jamani, unashindwaje kutenga saa 1 au 2 kwa mwaka ili kwenda kujadili maendeleo ya mwanao shuleni? Mzazi, kazi zipo na hazitaisha, ubize wako hautaisha. Suala la maendeleo ya mtoto wako ni jukumu lako wewe.

Tusiwatwishe walimu mzigo wasiostahiki. Ukaribu wako na mwalimu utampa nguvu mwalimu kumuelimisha mwanao. Umbali baina yenu utatengeneza mianya hatari kwa maendeleo ya mtoto wako. Ni hiyari yako kushirikiana na mwalimu au ubaki kunyoosha vidole huku watoto wetu wakifeli. Kabla ya kuhitimisha, ngoja tutaje mambo muhimu anayopaswa kufanya mzazi ili kuimarisha taaluma ya mtoto wake.

Mosi, tenga muda wa kwenda shuleni. Idadi ya siku itategemea na nafasi yako mwenyewe. Inaweza kuwa kila muhula mara moja au mbili. Hii itakupa fursa ya kujua changamoto za watoto wako mapema na pengine kwa kushirikiana na walimu mnaweza kubuni namna ya kuzikabila.

Pili, kagua madaftari ya watoto wako mara kwa mara. Kupitia ukaguzi huu, utabaini maendeleo ya mtoto na hata changamoto zake. Zaidi ya yote, utabaini kama mwanao anafika shuleni au laa. Baadhi ya watoto huwa hawafiki shuleni na wanaishia mitaani. Wazazi wengi huja kutanabahi hali hii baada ya muda kupita. Kama tutajijengea utaratibu wa kukagua madaftari yao tunaweza kubaini hali hii na kuitibu mapema.

Tatu, jenga mazoea ya kuwasaidia mazoezi za nyumbani [home work] kama zipo. Ni jambo la kusikitisha kuwa mazoezi ya nyumbani tumekuwa tukiwaachia wadada wa kazi wawasaidie watoto wetu. Hali hii inaondoa maana halisi ya kazi za nyumbani. Kazi hizi zilikusudia kujenga msingi baina ya mwalimu/shule na mzazi. Aidha, zililenga kumshirikisha mzazi katika mchakato wa elimu ya mtoto na kumuonesha mzazi fursa na changamoto za mtoto wake.

Nne, ongea na watoto wako kuhusu maisha ya shule. Waulize kuhusu walimu na namna wanavyowafundisha. Waulize kuhusu uhusiano wao na walimu [je, ni mzuri au mbaya]. Waulize kuhusu ushirikiano wao na wanafunzi wenzao. Pia, uliza kuhusu ubora wa chakula [kama kipo], upatikanaji wa maji safi na huduma ya vyoo.

Haya yote ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto shuleni. Shiriki katika vikao vya shule. Kupitia vikao hivi tujadili kero na changamoto zinazowakabili watoto wetu. Tushirikiane na walimu katika kutatua changamoto hizo. Tuepuke tabia ya kujadili mambo ya shule vijiweni  kwani haitusaidii chochote. Tuendelee kushirikiana na walimu kuwaelimisha watoto wetu. Tutambue kuwa maendeleo mazuri ya watoto ni kwa manufaa ya watoto wetu na wazazi.

Tags
Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close