-

Tuna mengi ya kujifunza kwa waislamu wa nchi nyingine, Aref Nahdi

Waislamu nchini wana mengi ya kujifunza kutoka kwa Waislamu wa nchi nyingine duniani katika masuala anuai ili waweze kupiga hatua katika dini yao na maendeleo kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi, mara baada ya kurejea nchini kutoka katika ziara yake ya Ufaransa, Thailand na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Akiwa katika nchi hizo, Mwenyekiti Nahdi alifanya mambo matatu makubwa.

Mambo hayo matatu ni, kwanza alitembelea maeneo mbalimbali muhimu katika nchi zote tatu kwa ajili ya kubadilishana uzoefu. Pili, alisaini mkataba na kampuni ya Eutelsat uliolenga kuboreresha matangazo ya vyombo vya habari vya Imaa. Tatu, alitembelea taasisi za UAE ambazo TIF inashirikiana nazo katika miradi mbalimbali nchini Tanzania.

Mwenyekiti Nahdi alibainisha kuwa akiwa katika nchi zote mbili, Ufaransa na kisha Thailand, alijifunza namna mbalimbali Waislamu wa huko wanavyoendesha mambo yao ya Kiislamu, hususan katika uendeshaji wa vyombo vya habari.

“Kiukweli kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa wenzetu. Binafsi nikiwa mdau mkubwa wa katika mambo ya vyombo vya habar vya Kiislamu nimejifunza jinsi wenzetu wanavyotumia vyombo hivyo kiweledi katika kuutangaza Uislamu na kutetea Sunna,” alisema Nahdi.


Mwenyekiti Nahdi aliongeza kuwa aliyoyaona huko yamempa changamoto ya kuzidi kuviboresha vyombo vya habari vya Imaan ili vizidi kuwa na tija zaidi katika kuwahudumia Waislamu na jamii kwa ujumla. Mwenyekiti huyo wa taasisi ya TIF inayosimamia miradi mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari – TV Imaan, Redio Imaan na Gazeti Imaan – alisema, Waislamu wanaomiliki vyombo vya habari hapa nchini ili kupata uzoefu na kujua mbinu wanazotumia ili kugikia malengo hususan da’awa.

Pia Nahdi amebainisha kuwa Waislamu wa nchi za huko wanapenda kuchangia katika masuala ya dini yao, na hivyo amewaomba Waislamu hapa nchini kuiga na kujenga tabia ya kuchangia vyombo ya Kiislamu kama wafanyavyo Waislamu wa Thailand na Ufaransa.

“Waislamu wa Ufaransa na Thailand ni wachache ila Ma shaa Allah wana moyo wa kuchangia mambo yao ya kidini, huu ndio moyo ambao Waislamu Watanzania tunapaswa kuwa nao. Hapa nchini ipo miradi mingi ya Kiislamu ila baadhi inakwama kwa kukosa fedha,” alisema Nahdi.


Ziara ya White Channel, Thailand
Akiwa nchini Thailand, Mwenyekiti Nahdi alitembelea Kituo cha Runinga cha Kiislamu cha Ahlu Sunnah kijulikanacho kama White Channel kilichopo jijini Bangkok, ambako alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Sumate Momin. Wakuu hao wawili wa vituo vikubwa vya Kiislamu nchini mwao walifanya mazungumzo na kubadilishana uzoefu.

Akitolea mfano wa kituo cha White Channel, Nahdi alisema ni kituo kinachoendeshwa kisasa, huku akikisifu zaidi katika namna wana-vyoendesha kampeni ya uchangiaji wa kituo hicho.


“Nimetembelea kituo cha White Channel, huwezi amini kiko katika nchi ya Waislamu wachache ila kinaendeshwa kiueledi na Waislamu wa huku wana moyo wa kujitolea haswa,” alisema Nahdi na kuongeza. “Hali hiyo natamani iwe kubwa hapa nchini ili Waislamu wazidi kuvichangia vyombo vya habari vya Imaan na vingine ili vizidi kujiimarisha na kuusemea Uislamu.”

Katika nchi ya Thailand iliyoko bara la Asia, takwimu za mwaka 2015 zinaonesha kuwa, idadi ya Waislamu ni asilimia nne, huku Mabudha wakishikilia awamu ya kwanza kwa kuwa asilimia 95.


Mkataba na Eutelsat jijini Paris
Akiwa huko Ufaransa, Mwenyekiti Nahdi alisaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya zaidi ya shilingi million 830 na kampuni ya Eutelsat ya nchini humo utakaosaidia kuboresha urushaji wa matangazo ya Radio na TV Imaan ili kuyafikisha mbali zaidi.

Mwenyekiti huyo wa TIF alisaini mkataba huo katika ofisi za makao makuu ya Eutelsat huko jijni Paris. Aliyesaini kwa niaba ya Eutelsat ni Makamu wa Rais (Mauzo), Francesco Cataldo, ambaye pia ni Makamu Afisa Mkuu upande wa biashara (CCO) wa kampuni hiyo kubwa ya kimataifa.

Vyombo vya habari vya Imaan vinarusha matangazo yake kupitia Satelite ya E7B inayomilikiwa na Eutelsat ya Ufaransa hali inayoifanya vyombo hivyo kuenea dunia nzima huku ikitoa elimu bora kwa Waislamu na ikiwa katika muonekano mzuri.

Mwenyekiti Nahdi alisema, Redio na Televisheni Imaan zitafaidika na mkataba huo, ambapo sasa matangazo yatawafikia Waislamu na wananchi kwa ujumla katika hali ya ubora zaidi kuliko awali. Mwenyekiti Nahdi pia aliwaomba Waislamu hapa nchini kuzidi kuviunga mkono vyombo hivyo katika namna mbalimbali ili viendeleze kuwa sauti ya Waislamu na kutetea maslahi ya jamii kwa ujumla.

Taasisi washirika UAE
Ziara ya Mwenyekiti Aref Nahdi pia ilimfikisha Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambako alitembelea taasisi kadhaa rafiki zinazoshirikiana na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) katika miradi mbalimbali nchini Tanzania.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Dar Al Ber Society, Sharjah Charity International, Dubai Charity Association na pia Mohammed bin Rashid Al Maktoum Humanitarian & Charity Est. Akiwa katika taasisi hizo, Mwenyekiti huyo alifanya mazungumzo na viongozi wa taasisi hizo wenyeji juu ya namna ya kuboresha ushirikiano wa taasisi zao.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close