-

Tujikinge na maafa ya ulimi

Kusengenya [kuteta]

Kusengenya ni moja kati ya maafa makubwa ya ulimi. Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] aliwauliza Maswahaba wake: “Je mnajua kusengenya ni nini?” Wakasema: “Allah na Mjumbe wake wanajua zaidi.” Akasema: “Kusengenya ni kumtaja ndugu yako kwa jambo lenye kumchukiza.” Pakasemwa: “Unaonaje kama atakuwa nalo huyo ndugu yangu hilo ninalolisema?” Akasema: “Ikiwa lipo kwake, utakuwa umemsengenya; na kama halipo utakuwa umemzulia.”[Muslim].

Hadithi inabainisha kuwa kusengenya au kuteta ni kutaja kasoro za mtu au ila ya ndugu yake asiyekuwepo, ambayo kama angekuwepo angechukia. Iwapo ila au kasoro uliyotaja hana, basi umemzulia na huo ni utesi mkubwa mno.

Mifano ya kusengenya

Hutokea mtu akasengenywa kwa sababu ya mwili wake, kama vile kumsema kwa hali yake ya upofu, uziwi, chongo, urefu, ufupi, rangi kama vile weusi weupe na mfano wa hayo, na iwe kwa sura itakayokuwa inamchukiza mlengwa. Pia, hutokea mtu kusengenywa kwa kumsema vibaya sababu ya nasaba au kabila lake kwa njia ya kumdharau. Kusengenya kunapatikana pia katika kumsema mtu vibaya kwa kudharau kazi yake anayoifanya; au pia kwa tabia zake mbaya kama vile kiburi, uoga na mfano wa hizo.

Hutokea pia kusengenyana kukafungamana na mambo ya kisheria kwa mtu kusemwa kuwa ni mwizi, muongo, mlevi, dhalimu au kutotekeleza majukumu yake ya kisheria kama vile swala, funga, kuwafanyia wema wazazi wawili au mengineo. Akisemwa mtu katika hali zote hizi juu ya mambo haya, kama kinachozungumzwa ni kweli, huesabika kuwa amesengenywa, na hivyo mwenyemtu huyo anahesabiwa kuwa anamuasi Allah Aliyetukuka.

Hata hivyo, msemaji anaweza asihesabike kuwa amesengenya akizungumza kwa njia inayomvua katika usengenyaji. Maana yake kwa namna ya utesi unaokubalika.

Utesi unaokubalika

Yapo mazingira yanayokubalika kisheria kumsema mtu,na msemaji asibebe lawama za kusengenya.

Kulalamikia dhuluma: Miongoni mwa hali hizo ni pamoja na kulalamikia dhulma kwa kumtajia hakimu au kadhi dhulma, khiyana au ufisadi anaofanyiwa na mtu mwingine. Mtu anaweza kufanya hivi ili kutaka msaada wa kuondosha uovu kwa anayeweza kuuondosha au kusaidiana ili kumrejesha yule muovu, aliyeasi katika njia iliyonyooka. Mfano wa hili, ni kumsemea mtu anayekunywa pombe au kuacha swala kwa kiongozi au mlezi wake ili kuondosha uovu huo.

Kutaka fat-wa: Pia inakubalika kuitaja hali ya mtu na uhalisia wa maisha yake kwa ajili ya kutaka fat-wa. Mfano ni mwanamke kumwelezea mufti kuwa mumewe ni bakhili kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kupata mahitaji yake kiukamilifu kutoka kwa mumewe.

Kumtahadharisha mtu: Pia mtu anasameheka kwa kusengenya iwapo alifanya hivyo kumtahadharisha Muislamu juu ya shari anayoweza kukumbana nayo. Mfano, ni mtu kumuelezea mtu ambaye anasuhubiana naye kuwa ni muovu au mzushi, na hivyo akamnasihi na kumtahadharisha wengine wawe makini naye. Mfano wa hili ni wanazuoni walivyobainisha hali za watu miongoni mwa wapokezi wa hadithi ili kubainisha kama wanaaminika katika kutoa habari au la.

Sambamba na hili, anasameheka pia mtu anayemsema mtu anayefanya maasi kwa dhahiri kama vile mlevi, mzushi, dhalimu ili watu waweze kumtambua na kuwa na tahadhari naye.

Kutumia majina maarufu: Pia mtu anasameheka kusengenya katika kutumia majina maarufu yanayotokana na muonekano wa mtu anayemtaja ili kutaka mtu anayemtaja afahamike kwa anaoongea nao. Huenda majina hayo si mazuri lakini ndiyo yanayowafanya watambulike. Mfano wa majina haya ni mtu kuitwa chongo, bonge na kadhalika, naye akaridhia.

Aina za utesi

Utesi hauishii katika maneno tu bali kitu chochote kinachoashiria maasi hayo kinaingia katika uovu huu. Mfano wa hayo ni ishara, maandishi, tamthilia, igizo, vichekesho na mengine mengi  yanayooonesha kuwa ni utesi kwa namna yoyote.

Kushiriki katika utesi

Miongoni mwa watu wanaoingia katika hukumu ya wenye kusengenya ni yule anayesikiliza utesi huo kwa njia ya kufurahia na kuridhia kinachozungumzwa, hali ambayo inamzidishia hamasa yule anayesengenya kwasababu amepata watu wa kumshajiisha na kumuunga mkono katika jambo hilo.

Pindi mtu anapomsadikisha msengenyaji katika yale anayoyasema na akayaridhia, atakuwa ameshiriki katika dhambi hiyo, hivyo ni wajibu kwa kila mtu kutetea na kulinda heshima ya ndugu yake katika Imani kwa kumnasihi na kumkemea yule anayemsengenya. Haifai kufurahia na kuridhia mazungumzo ya namna ya hiyo.

Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] amesema: “Atakayetetea heshima ya ndugu yake akiwa mwenyewe hayupo ni haki juu ya Allah kumwacha huru na moto.” [Ahmad].

Yanayopelekea katika utesi

Kuna mambo mengi yanayopelekea watu kusengenyana mara kwa mara, miongoni mwa mambo hayo ni chuki iliyojificha inayowezakubadilika kuwa uadui wa dhahiri. Husda inayouchoma moyo wa mtesi dhidi ya mwenzake humfanya ahahe kumteta ili amvunjie heshima yake na kudogesha hadhi yake katika jamii, huku mtesi huyo akificha aibu na maovu yake mwenyewe.

Jambo jingine linalopelekea utesi ni kupenda kuwaridhisha wanabaraza unaokaa nao mara kwa mara na kuwaunga mkono na kulifurahisha baraza.

Hukumu ya kusengenya [kuteta]

Kusengenya ni katika tabia mbaya kijamii ambazo Muislamu hastahiki kuwa nazo. Kusengenya kumeharamishwa lina kukemewa kwa nguvu katika mafundisho ya Uislamu, kutokana na madhara makubwa yanayotokana na tabia hii yakiwemo kuharibu udugu, kuvunja heshima za watu, kupandikiza uadui na kueneza aibu za wengine.

Allah Aliyetukuka amemfananisha msengenyaji na mtu ambaye anakula nyama ya ndugu yake akiwa amekufa, pale aliposema:

“Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anayependa kuila nyama ya nduguye aliye kufa Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu [42:19].

Tags
Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close