-

Tofauti za madhehebu kikwazo katika dini

Mudir wa Chuo cha Kiislamu, Baabil hudaa Islamiya kilichopo Mtae katika Halmashauri ya Lushoto mkoani Tanga, Sheikh Ramadhan Mohammed amewataka Waislamu wa madhehebu zote hapa nchini kuondoa tofauti zao ili kujiletea maendeleo katika dini yao na jamii nzima. Sheikh Ramadhan alisema Uislamu unasisitiza watu kupendana, kuishi kama ndugu na kuimarisha misingi ya umoja na mshikamano kama alivyofundisha Mtume Muhammad (Rehema za Allah na amani zimshukie).

Akizungumza na Waumini wa dini ya Kiislamu katika msikiti wa Muuminina uliopo kata ya Tuangoma, wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan aliwataka Waislamu kuepuka faraka zinazoweza kuwagawa na kuzusha vurugu miongoni mwao.

Alisema faraka zimesababisha Waislamu kukosa nguvu na umoja miongoni mwao na kujikuta wakipoteza fursa ya kupiga hatua za maendeleo kwa kujenga miundombinu ya kijamii kama vile shule, vyuo vikuu na hospitali.

“Ninawaasa Waislamu kuwa makini na baadhi ya watu wanaotaka kutugawa kwa maslahi yao binafsi. Tuepuke sana faraka baina yetu. Tujifunze kufanya mema ndani ya jamii yetu kwa faida ya taifa na Waislamu wenzetu,” alisema Sheikh Ramadhan na kuongeza: “Waislamu tumepoteza ule Uislamu tuliofundishwa na Mtume (Rehema za Allah na amani zimshukie), tumejigawa makundi makundi na kujengeana uadui sisi kwa sisi, tumesahau kabisa kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

“Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu.” (Qur’ an, 3:103).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close