-1. Habari1. TIF News

TIF Yasaidia Kituo Cha Kutibu Waathirika wa ‘Unga’

Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi (mwenye kanzu nyeupe) alipotembelea kituo cha kutibu waathirika wa ‘unga’ akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Ibrahim Twaha.

Kassim Lyimo, Moro

VIONGOZI wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) wameahidi kusaidia kituo cha kuwahudumia walioathirika na dawa za kulevya kiitwacho Free at Last Sober House kilichopo maeneo ya Kihonda Mkoani Morogoro. Ahadi hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Aref Nahdi alipotembelea kituo hicho akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Ibrahim Twaha. Akizungumza na waathirika wa dawa za kulevya katika kituo hicho, Mwenyekiti Nahdi aliwapongeza kwa kuweka nia ya kubadilika na kuachana na matumizi ya madawa hayo. “Nawapongeza kwa kuweka nia na mkaweza kubadilika. Mmefanya jambo muhimu sana na jambo la msingi naomba hiyo nia mliyoweka iwe ya kweli, na wala msirudi nyuma na kutumia tena dawa za kulevya,” alisema Nahdi. “Tumekuwa tukiwasaidia baadhi ya watu wanaotoa huduma kama hii Zanzibar, na Mombasa nchini Kenya lakini kwa sasa tunashukuru kituo hichi kimejengwa Morogoro. Leo ndiyo siku yetu ya kwanza kukitembelea, lakini tulishaanza kutoa misaada siku za nyuma,” alisema Mwenyekiti huyo wa TIF. Ikumbukwe kuwa Mwenyekiti Nahdi alikuwa ni miongoni mwa watu wa kwanza kujitokeza kuunga mkono vita dhidi ya madawa ya kulevya mapema mwezi uliopita zilizoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kuungwa mkono na Rais John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Naye Mkurugenzi Mkuu wa TIF, Sheikh Ibrahim Twaha, alisema kuwa taifa bado linawategemea vijana hao na kuwataka kuwa karibu na mafundisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. “Kwanza tumefarijika kufika katika kituo hiki ambacho tulikuwa tunakisikia tu. Jambo la muhimu kwenu ni kutorudia kutumia dawa hizo na badala yake kuwa karibu na mafundisho Allah Subhanallah wa Ta’ala, naye Allah atawafanya kuwa ni watu wema katika jamii,” alisema Sheikh Twaha. “Familia zenu bado zinawategemea, jamii pia inawategemea, na taifa pia linawategemea ili baadaye muwe viongozi bora ambao mtakuwa ni mfano mzuri wa kuigwa na watu wengine,” alisema Mkurugenzi huyo wa TIF. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Free and Last Sober House, Juned Mbaraka amewashukuru viongozi hao wa TIF kwa kuwatembelea vijana hao. Hali kadhalika, Meneja wa Kituo hicho Suleimani Nasoro, amefurahishwa na ujio wa viongozi hao wa TIF na kukiri kuwa hakuna taasisi yeyote ambayo imewahi kuwatembelea na kujua changamoto zinazowakabili. Nao waathirika wa dawa hizo ambao wanapewa huduma katika kituo hicho cha Free and Last Sober House, wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo upungufu wa vitanda, chakula, ukosefu wa maji pamoja na huduma nyingine. Akijibu baadhi ya changamoto hizo, Mwenyekiti wa TIF alisema taasisi yake itawasaidia na pia itaendelea kuwasaidia kwa mambo mengine baadaye. “Kwa kuanzia tutafanya utaratibu wa kuwatengenezea vitanda, kuwaletea magodoro na mashuka mapya ili kituo kiweze kuwavutia watu wengine kuwaleta ndugu zao, lakini pia kesho Inshaallah tutawaletea mbuzi wawili kwa ajili ya kituo,” alisema Mwenyekiti huyo wa taasisi ya TIF. Kituo cha kuwahudumia walioathirika na dawa za kulevya cha Free at Last Sober House, kilichopo maeneo ya Kihonda Mkoani Morogoro kinamilikiwa na watu binfsi na sasa kina vijana 14 ambao wameacha kutumia dawa hizo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close