-1. Habari1. TIF News

TIF yapeleka mahujaji 16 kwa ufadhili wa falme za Kiarabu

Taasisi ya The Islamic Foundation  (TIF) yenye makao yake makuu  mkoani Morogoro inatarajiwa kupeleka mahujaji 16 Makka, Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hijja kwa ufadhili wa taasisi mbalimbali za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kupitia Ubalozi wake hapa nchini.

Katika mahujaji hao, 6 kati yao wamefadhiliwa na taasisi ya The Zayed Bin Sultan Al Nahyan Charitable and Humanitarian Foundation ya Falme za Kiarabu (UAE) na watano wamefadhiliwa na Jumuiya ya Dubai Charity Association (DCA). Hawa wote wamelipiwa gharama kamili.

Mahujaji wengine watano wamefadhiliwa na Sharjah Charity International wakiwa wamelipiwa nusu gharama na gharama nyingine kutakiwa kujilipia wenyewe. Akiongea na gazeti Imaan, Mkurugenzi Mtendaji wa TIF, Sheikh Ibrahim Twaha, amesema maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya safari hiyo.

“Mahujaji wetu wanakwenda na taasisi ya kupeleka mahujaji ya Khidmat na tayari wameshapata chanjo, visa na tiketi za safari pamoja na mavazi ya kuvaa wakiwa Hijja, yaani Ihraam na wameshahudhuria semina za maandalizi. Kilichobaki ni kuondoka tu kuelekea viwanja takatifu,” aliongeza Sheikh Ibrahim.

Safari ya mahujaji hawa ilianza siku ya Jumanne Julai 30, 2019 katika uwanja wa ndege wa JNIA jijini Dar es Salaam kuelekea Dubai na ndege ya Shirika la ndege la Emirates na kubadili ndege kutoka Dubai kuelekea Jeddah nchini Saudia Arabia ambapo wanatarajiwa kuwasili Makka siku hiyo hiyo majira ya saa 2 usiku in Shaa Allah.

Kwa miaka kadhaa sasa TIF imekuwa ikipeleka mahujaji katika mradi wa taasisi hiyo kutoka Imarati wa kufadhili mahujaji kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwamo Tanzania. Mahujaji wa TIF na wenzao wanaokwenda na taasisi ya Khidmat, wanatarajiwa kurejea Agosti 25, 2019 baada ya kuhiji na kutembelea mji wa Madina na maeneo mbalimbali ya kihistoria.

Sheikh Haruna Kapama, mmoja wa Masheikh anayeongoza mahujaji hao alitaja baadhi ya maeneo ya kihistoria watakayoyatembelea mjini Makka na Madina kuwa ni pamoja na nyumba aliyozaliwa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) pamoja na nyumbani kwa Bi. Khadija bint Khuwaylid (Allah amridhie).

Watakapokuwa Madina, licha ya kuzuru kaburi la Mtume na Makhalifa Abubakar na Umar (Allah awaridhie), mahujaji hao wanatarajiwa pia kuzuru makaburi ya Maswahaba katika makaburi ya Albaqii na maeneo mengine matakatifu katika mji wa Madina.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close