-1. Habari1. TIF News

TIF Kuchangisha Shilingi Bilioni 6

Mikopo ya elimu bila riba

T aasisi ya The Islamic Foundation (TIF) inatarajia kuchangisha kiasi cha Shilingi bilioni 6 kutoka kwa wahisani na wadau ili kufanikisha mchakato wa utoaji mikopo bila riba kwa wanafunzi wa ngazi mbali mbali za elimu. Mwenyekiti wa TIF, yenye makao yake makuu mjini Morogoro, Aref Nahdi amesema hayo hivi karibuni alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 10 ya Shule ya Kiislamu Mivumoni yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam. Mpango huo unojulikana kama ‘TIFEducation Fund’ utawawezesha wanafunzi wa Kiislamu watakaokuwa wanasoma katika ngazi mbali mbali za elimu. “Nawaomba siku ikizinduliwa hii bodi muiunge mkono na InshaAlah tunatarajia itazinduliwa baada ya mwezi wa Ramadhani na bajeti yake inakadiriwa kuwa bilioni 6, zitatoka wapi, Mimi sijui ila Allah anajua,” alisema Nahdi. Pia Nahdi aliwataka Waislamu kuhakikisha wanafanya mambo kwa ajili ya Allah kwani yeye ndiye huleta mafanikio. “Waislamu wenzangu tufanye mambo kwa ajili ya Allah, natuamini kila kitu kinawezekana endapo tutafanya kwa ajili ya Allah, leo hii TIF kwa uwezo wa Allah ina redio, runinga, gazeti, na tumefanikiwa kuchimba visima zaidi ya 2,000 na misikiti zaidi ya 2,000,” alisema Nahdi. Kauli hizo za Nahdi zimekuja kufuatia tangazo alilolitoa Januari 29, mwaka huu wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa taasisi hiyo uliofanyika mjini Morogoro ambapo aliujulisha umma wa Watanzania juu ya mpango wa kuanzisha bodi ya mikopo ya elimu ya Kiislamu, isiyotoza riba. “Kutokana na wanafunzi wengi kukosa mikopo ya kujiendeleza na elimu ya juu, na pia mikopo mingi kuwa na riba, taasisi yetu ya The Islamic Foundation kwa kushirikiana na baadhi ya wadau itaanzisha Mfuko wa Elimu kwa ajili ya kutoa mikopo isiyokuwa na riba,” alisema Nahdi. Tayari baadhi ya viongozi wa mfuko huo wamechaguliwa, akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu Mstaafu wa Jumuiya wa Wanataaluma wa Kiislamu Tanzania (TAMPRO), Dkt. Pazi Mwinyimvua. Dkt. Pazi yeye ndiye Katibu wa Mfuko huo wa Mikopo ya Elimu. Akizungumza na gazeti hili, Katibu huyo wa Mfuko wa Elimu wa TIF alisema wataanza rasmi kutoa mikopo hiyo mwezi Novemba 2017. Aidha, Dkt Pazi alisema walengwa wa mfuko huo ni pamoja na wanafunzi wa Kiislamu wenye uwezo mkubwa kiakili, lakini wanaotoka katika familia masikini na wanaojiunga na kidato cha kwanza, cha tano au chuo kikuu. Aidha, Dkt. Pazi alisema mfuko huo hauishii Tanzania Bara tu, bali utafanya kazi zake hadi Zanzibar. Akijibu swali la ni kwa namna gani mikopo hiyo ni tofauti na mingine, Dkt. Pazi alisema mikopo ya TIF itatolewa bila kutoza riba wakati wa kurejesha. Dkt. Pazi alisema: “Hii ni mikopo inayotolewa kwa mujibu wa Sharia ya Kiislamu, ingawa mwanafunzi atakaa miaka mingi mpaka aweze kurejesha mikopo baada ya kumaliza elimu yake na kupata ajira, bado atalipa kiasi kilekile alichokopa.” “Matarajio yetu ni kuwa mikopo hii itatoa mchango mkubwa katika kuwakomboa Waislamu ambao hata Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliwataja kama moja kati ya makundi yaliyo nyuma kielimu na yanayohitaji kusaidiwa, ingawa mpaka sasa miaka 50 hali haijawa nzuri,”alisema Dkt Pazi.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close