-

Thamani ya maisha ya dunia

Imepokewa Hadithi kutoka kwa Abdullah bin Masoud (Allah amridhie) kuwa siku moja Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alilala juu ya mkeka kisha akainuka hali ya kuwa  ule mkeka umeweka alama katika ubavu wake. Maswahaba wakamwambia: “Ewe Mjumbe wa  Allah, kwa nini tusingekutengenezea tandiko?” Akasema: “Ni na nini mimi na dunia? Sikuwa mimi katika dunia isipokuwa ni kama msafiri  ambaye amepumzika kutaka kivuli chini ya mti kisha akaondoka na kuuacha,” [Tirmidhiy].

Katika tukio hili tunapata mazingatio yafuatayo: 

Mwili una haki yake ya kupumzikana hupata mapumziko mazuri pale mtu anapolala katika tandiko (godoro) zuri na laini. Binadamu anahitaji mapumziko kutokana na uchovu wa mwili na tabu za kazi za kutwa nzima kisha akusanye nguvu zake kwa ajili ya siku mpya, ikiwa Allah atampa uhai nguvu na afya njema, aweze kukabiliana na harakati za siku hiyo kwa uchangamfu.

Ikiwa tandiko ni gumu, huweza kusababisha uchovu zaidi na kumfanya mtu kukosa raha ya  kupumzika hata kufikia kupoteza lengo la kuupumzisha mwili, bado Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) hakujitafutia tandiko la kifahari lililo laini kwa ajili ya kupumzika bali  alijiwekea tandiko la mkeka na mto wa ngozi uliojazwa kamba hadi kiasi ule mkeka ukaweka athari katika mwili wake.

Jambo hili lilikuwa linawaumiza sana Maswahaba wake hasa walipokuwa wakiyashuhudia au kusikia maisha ya kifahari ya viongozi na wafalme mbalimbali wa zama hizo. Anas bin Malik (Allah amridhie) amesema, aliingia kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akiwa juu ya kitanda cha kamba, chini ya kichwa chake kukiwa na mto wa ngozi ulijazwa kambakamba ndani yake.

Swahaba Umar bin Khattab akaingia akiambatana watu wengine miongoni mwa Maswahaba (Allah awaridhie). Mtume akajigeuza kidogo, Umar akaona athari ya mkeka katika ubavu wa Mtume, akalia. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akamuuliza: “Ni kitu gani kinakuliza ewe Umar?” Umar (Allah amridhie) akasema: “Kwanini nisilie wakati Kisra (Mfalme wa Fursi) na Kaisari (Mfalme wa Roma) wanaishi katika maisha wanayoishi kwenye dunia (maisha ya kifahari) na wewe unaishi katika hali hii ninayoiona!”

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasema: “Ewe Umar hivi huridhiki dunia iwe ni ya kwao na Akhera iwe ni ya kwetu?” Akasema: “Ndio ninaridhia.” Mtume akasema: “Basi ndio hivyo,” [Bayhaqiy]. Watu wengi wanapitia hali ngumu ya maisha. Jambo hili halipasi kumfanya mtu avuke mipaka, bali yumpasa avumilie. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ni kipenzi cha Allah na angeweza kuishi katika maisha ya kifahari kwa namna anayotaka, lakini amepitia ngazi na hali mbalimbali za kimaisha ili aweze kuwa ni mfano kwa watu wa madaraja yote.

Mtume alizaliwa akiwa yatima. Akiwa mdogo, alifiwa na wazazi wake na hata walezi wake. Mtume ameishi maisha ya kimaskini akichunga mbuzi. Baada ya kupewa utume, alikuwa akipata mali ima ngawira au mali za zaka lakini hakutaka kuwa kiongozi mwenye maisha ya fahari. Kwa ujumla, Mtume alipenda kuishi maisha ya hali ya chini huku akiwatahadharisha maswahaba na umma wake kiujumla juu ya udanganyifu wa ulimwengu na starehe zake.

Hata hivyo, hii haina maana kuwa mwanadamu asiishi vizuri bali tunakatazwa maisha ya kifahari ambayo yanampelekea mtu kujisahau na kusahau kuwa mbele yake kuna maisha ambayo ni bora kuliko maisha haya. Katika tukio hili, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anatupa mfano wa ufupi wa maisha ya kidunia kwa kuyafananisha na kipindi kifupi ambacho amepumzika msafiri chini ya mti kwa ajili ya kupata kivuli kisha kuendelea na safari.

Mwanadamu anatakiwa wakati wote ajihesabu kuwa yupo safarini na ataondoka wakati wowote. Allah aliyetukuka anatuelezea pia kuhusu ufupi maisha ya kidunia na kwamba starehe zake si za kudumu, ingawa watu wanavyodanganyika nazo.

Allah amesema: “Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo na pumbao, na pambo na kujifakharisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu kali na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu,”
[Qur’an, 57:20].

Kwakuwa nafsi ya mwanadamu imeumbwa na tabia ya kuipenda dunia na kufungamana nayo, Uislamu unailea nafsi katika njia iliyosawa, malezi yatakayoifanya nafsi iweze kuyatawala matamanio yake na kujiepusha na anasa za kilimwengu. Uislamu unaielekeza nafsi kuwa maisha haya ya dunia yanayoonekana kuwa ni mazuri na yenye mvuto, ukiyafananisha na maisha ya baadae, si chochote.

Allah anayaelezea maisha ya dunia na namna watu wanavyodanganyika nayo kisha anayaelezea maisha ya akhera na namna watu wanavyoghafilika nayo, kisha anatuacha sisi wenyewe tuyapime maisha haya na tuone ni yepi yanafaa kukimbiliwa.

Lakini pia, Allah Aliyetukuka haachi kutuelekeza yale yanayostahiki kupewa kipaumbele: “Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyowekewa waliomuamini MwenyeziMungu na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu,” [Qur’an, 57:21].

Ni lazima kuwe na uwiano sawa katika maisha ya Muislamu, kimwili na kiroho. Muislamu asijinyime neema ambazo Allah amewaneemesha wanadamu katika dunia hii lakini pasi na kuchupa mipaka iliyowekwa katika sharia juu ya namna ya kuzipata na kuzitumia. Wakati huohuo, mwanadamu asisahau lengo la kuwepo kwake, yaani kumwabudu Allah Aliyetukuka. Mwanadamu ajishughulishe na mambo ya kiroho ili asije akazama katika dimbwi la starehe za kilimwengu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close