-

Tawheed yawafunda mahujaji watarajiwa

Taasisi ya Tawheed Development Network imeanza kutoa mafunzo kwa mahujaji watarajiwa ili kuwapa ufahamu wa ndani wa ibada ya hijja kabla ya kwenda huko Saudi Arabia

Akiongea katika Semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es swalaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Hijja wa Taasisi hiyo ya Tawheed, Mhandisi Mussa Natty, amesema kuwa, wamekuwa wakitoa semina karibia kila wiki ili mahujaji wapate elimu ya hijja ya kutosha.

Mhandisi Natty alisema wanatoa mafunzo hayo kwa muda mrefu ili mahujaji hao watarajiwa wakienda Saudi Arabia wasipate tabu sana ya kutekeleza ibada hiyo. “Siye tunafanya semina nyingi kwa mahujaji wetu, na huwa tunafanya hivyo karibia kila wiki, na kutokana na hali hiyo ndiyo maana mahujaji wetu huwa hawapati tabu wakiwa huko Makka,” alisema mhandisi Natty.

Pia Mhandisi huyo alisema kuwa semina zinazotolewa na Tawheed si kwa ajili ya mahujaji wa taasisi hiyo bali mtu yoyote anaetarajiwa kwenda hijja anaruhusiwa kuhudhuria. Mhandisi Natty alisema kuwa semina hizo zinatolewa pia katika mikoa mingine huku akitoa wito kwa mahujaji hao watarajiwa kuhakikisha wanapata elimu ya kutosha ya ibada za hijja.

Profesa Assad

Naye muanzilishi wa taasisi hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, Profesa Mussa Assad amesema kuwa, taasisi hiyo inaendesha mambo yake kwa kuzingatia sheria za Kiislamu na ndiyo maana mambo yao yanakwenda vema.

“Siye tunafanya baishara na Mwenyezi Mungu, na ndiyo maana tunakikisha kila anayeenda hijja anajua mambo ya huko vizuri, na tunafanikiwa katika hilo,” alisema Prof. Assad.

Naye Mgeni rasmi katika semina hiyo, Meneja wa Shirika la Misaada Afrika (A.R.O), Samy Mohamed Elazeb, amewahimiza Waislamu kupupia ibada ya hijja akisema nguzo hiyo inapaswa kutiliwa mkazo kama nguzo zingine. “Waislamu lazima tujue ibada ya hijja ni muhimu kama zilivyo ibada zingine, hivyo hatuna budi kutumia kila kidogo tunachopata kwa ajili ya kupata uwezo wa kwenda Hijja,” alisema Meneja huyo.

Nao baadhi ya mahujaji watarajiwa wamesema semina hizo zimesaidia kuwapa elimu kubwa na wanaimani watatekeleza ibada yao wakiwa na ufahamu sahihi wa jinsi inavyofanywa ibada hiyo.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close