-

Swala inahitaji maandalizi-4

Swala ya jamaa na umuhimu wake

Moja ya malengo makuu ya kujengwa na kuwepo misikiti katika maeneo wanayoishi Waislamu ni kuwakusanya ili waswali pamoja, yaani swala ya jamaa. Swala ya jamaa maana yake ni watu kujumuika na kuswali pamoja nyuma ya imamu (kiongozi) mmoja wa ibada ndio maana Mtume akasisitiza kwamba, watu watatu au wawili tu wakiishi sehemu lazima waswali jamaa, na wasipofanya hivyo, huzingatiwa kuwa wamekumbwa na ubabaishaji (wamepotoshwa) na shetani.

Maandalizi ya swala ya jamaa

Muislamu anapaswa kupata maandalizi ya kiroho ili yamsukume kupenda kuzitekeleza swala kwa jamaa. Maandalizi hayo hupatikana kwa kuijua nafasi na umuhimu wa swala ya jamaa msikitini kiasi kwamba mja aone aibu, ajisikie mpungufu na ajilaumu iwapo ataikosa. Haifai kwa Muislamu kuona kukosa jamaa kuwa jambo la kawaida kwani kwa mujibu wa Qur’an na Sunna, swala ya jamaa ni muhimu sana.

Swala ya jamaa katika Qur’an

Katika Qur’an, kuna aya kadhaa zinazoonesha kwamba, amri ya kusimamisha swala imeambatanishwa na agizo kwa Waislamu waswali kwa pamoja, yaani jamaa. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema: “Katika nyumba ambazo Allah ameamrisha yatukuzwe na humo litajwe jina lake, humtakasa humo asubuhi na jioni. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.” [Qur-an 24:36-37].

Na katika aya nyingine, Allah Aliyetukuka anasema: “Muhammad ni Mtume wa Allah na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri, wenye kuhurumiana wao kwa wao, utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja) wakitafuta fadhila za Mola wao na radhi (zake). Alama zao ziko katika nyuso zao kutokana na athari ya kusujudu (unyenyekevu). Huu ndio mfano wao katika unyenyeke Taurati na mfano katika Injili. . .” [Qur’an 48:29].

Katika aya nyinigine, Allah anasema: “Na simamisheni swala na toweni zaka na swalini pamoja na wenyekuswali.” [Qur’an, 2:43]. Kadhalika, anasema katika aya nyingine: “Na mtegemee (Mola) Mwenye nguvu, Mwingi wa rehema, ambaye hukuona ukiwa umesimama (ukiswali) na kugeuka kwako (ukirukuu na kusujudu) pamoja na wanaosujudu (walio nyuma yako).” (Qur’an, 26:217-218).

Kutokana na aya hizi, tunajifunza kwamba, misikiti ni vituo vitakatifu. Licha ya shughuli nyingi zitakiwazo kufanywa humo, lengo kuu ni kuwakusanya Waislamu na kuswali kwa pamoja. Mtu wa kwanza kupewa agizo hilo ni Mtume mwenyewe (rehema za Allah na amani zimfikie). Aidha, tumeona kuwa kuswali pamoja ndio desturi ya Waumini katika umma zote za Mitume waliopita, na wala sio tu katika umma huu. Unapoingia wakati wa swala, Waumini hao hawashughulishwi tena na kazi yoyote na hukimbilia kwenye nyumba za ibada kumtaja Mola. Wanafanya hivyo kwa sababu wanamhofu Mola wao na adhabu yake Siku ya Kiyama, lakini pia wanataraji radhi na malipo.

Umuhimu wa swala ya jamaa katika Sunna

Tukigeukia upande wa Sunna, pia tunakuta Hadithi nyingi zinazobainisha sio tu umuhimu wa kuswali misikitini, lakini pia kutaja fadhila za swala hizo zinaposwaliwa kwa jamaa. Ibn Masoud (Allah amridhie) amesema: “Ambaye anapenda kukutana na Mola wake akiwa amesalimika basi na azihifadhi swala hizi tano kila zinapoadhiniwa kwani Allah ameweka kwa Mtume wenu mienendo ya uongofu; na swala ni katika mienendo ya uongofu. Basi lau mtaswali katika majumba yenu kama afanyavyo mpuuzaji (wa swala za jamaa) mtakuwa mmeacha Sunna za Mtume wenu, na mkiacha Sunna za Mtume wenu mtapotea.

“Na mtu yoyote atakayejitwaharisha vizuri kisha akaelekea moja ya hii misikiti, basi huandikiwa kwa kila hatua anayoipiga wema mmoja, na hupandishwa daraja moja (ya utukufu) na kufutiwa dhambi. Na sisi tulijiona (wakati wa Mtume) kwamba mtu atakayeacha kuswali jamaa msikitini (bila udhuru wa kisheria) ni mnafiki ambaye unafiki wake unajuilikana (uko wazi). (Wakati wa Mtume) ilikuwa mtu huletwa (anajikongoja) akiwa ameshikiliwa na watu wawili mpaka anasimamishwa kwenye safu.” (Muslim).

Mtume amesema pia: “Wape habari njema watembeao katika viza (wakienda msikitini) kwamba watapata nuru kamili Siku ya Kiyama” (Ibn Majah na Ibn Khuzaima). Hii ni habari njema kwa wazichungao nyakati za swala na kutoka kwenda misikitini, sio mchana tu bali pia wakati wa kiza cha usiku. Hao wanaambiwa Akhera watapewa nuru iliyotimia. Amesema tena Mtume: “Swala ya jamaa inaizidi swala ya pweke kwa daraja 25/27.” Yaani, mtu aliyeswali swala ya jamaa ni kama ameiswali swala hiyo mara 25 ukilinganisha na mtu aliyeiswali peke yake. Licha ya faida na fadhila za swala za jamaa tulizozitaja, onyo kali limetolewa kwa Waislamu wanaume wenye tabia ya uvivu wasiohudhuria swala hizo misikitini. Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) alichukia sana kitendo cha kuacha swala ya jamaa kiasi cha kutamani kuzichoma moto nyumba za wanaume hao, kama si wanawake na watoto wanaoshi.

Baada ya kufahamu maandalizi hayo ya kiroho kwa kuujua umuhimu wa kuswali jamaa misikitini, kinachofuata ni maandalizi ya namna itakayomuhakikishia mja kuwa anazipata swala hizo na hazimpiti kiholela. Tulishagusia katika makala iliyopita jinsi na utaratibu anaotakiwa Muislamu kuufuata wakati anatoka na kuelekea msikitini hadi kuingia ndani. Hapa tunapenda kumuonesha nidhamu anayotakiwa wakati swala inakimiwa.

 

Wakati wa kukimiwa swala

Ametakiwa Muislamu kwa kila jambo analolifanya katika utekelezaji wa ibada zake msikitini awe na nidhamu ya hali ya juu ili asiharibu ujira unaotarajiwa. Kuhusiana na hili, katika Hadithi iliyopokewa na Abuu Huraira, Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema:

“Inapokimiwa swala, msiiendee kwa mbio. Iendeeni taratibu na jilazimisheni kuwa watulivu na wenye heshima. Mlipoiwahi, swalini pamoja na imamu na ilipowapiteni kamilisheni.” [Bukhari na Muslim].

Ni vyema Muislamu kukumbuka kuwa Allah ndiye mfanikishaji wa kila jambo, ndiye aliyemtoa nyumbani kwake na kumpeleka msikitini, basi hana budi kuishukuru neema hii adhimu aliyoshushiwa. Kwa hiyo, Muislamu anatakiwa aende pole pole huku akiitafakari neema hiyo ambayo wengine hawajaipata, lakini asisahau kuwa anatakiwa kuwa mtulivu pia wakati anaisogelea safu.Papara, vishindo na kelele hazitakiwi katika mazingira ya nyumba ya ibada (msikiti), nje na ndani, hususan pale ibada inapotaka kuanza na wakati wote inapoendelea.

Upangaji wa safu

Jambo jingine la kuzingatia ni suala la kuzinyoosha na kuzipanga safu vizuri. Hili ni jukumu la imamu na maamuma, ingawa imamu ndiye anayetakiwa kuwaongoza kwa kuwahimiza na kuwaamrisha. Kutokana na umuhimu wa kupanga safu, ilikuwa ni kawaida ya Mtume kabla ya kuianza swala huwapanga swahaba na kuwaambia: “Zipangeni swafu na jiwekeni sawa, kwani kuziweka sawa safu ndio kutimia kwa sala.”

Swala inahitaji maandalizi-1

Swala inahitaji maandalizi -2

Swala inahitaji maandalizi-3

 

 

 

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close