-

Siku ya Wanawake Duniani: Uislamu umempa heshima kubwa mwanamke

Machi 8, 2019 Tanzania iliungana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambapo kwa hapa Tanzania kauli mbiu ya mwaka huu inasema: ‘Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu.’ Maadhimisho haya ya kila mwaka hutoa fursa kwa mataifa, taasisi zisizo za kiserikali na wadau wengine kupima mafanikio yaliyopatikana katika kuwaendeleza wanawake na kubainisha changamoto zilizojitokeza katika kuwawezesha na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.


“Enyi watu! Hakika sisi tumekuumbeni kutokana na mwanaume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Mbora wenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye mchamungu zaidi.” [Qur’an, 49:13]

Tangu kuasisiwa kwake mwanzoni mwa mwaka 1909, pamoja na mambo mengine, wadau na wanaharakati wa haki za binadamu na zile za wanawake wamekuwa wakipigania suala la kumkomboa mwanamke kisiasa, kiuchumi na kijamii, baadhi wakiona Uislamu ni kikwazo katika kulifikia hili. Miongoni mwa maneno yenye kasoro kubwa katika sehemu kubwa ya hotuba za wadau na wanaharakati wa haki za wanawake, ni kusemwa kwamba heshima na haki za mwanamke zimeporwa.

Dhana hii inapingana na kauli ya Mungu Muumba inayosema: “Na hakika tumewatukuza wanadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba.” [Qur’an,
17:70].

Uislamu unatambua haki za makundi mbalimbali ya watu katika jamii ambazo zinapaswa kuheshimiwa. Moja ya makundi hayo ya jamii ni wanawake. Uislamu unaagiza kumjali, kumuheshimu na kumthamini mwanamke. Tunaporejea historia ya Uislamu [Tareikh] tunaona kuwa, Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] alimkuta mwanamke kwenye jamii mbalimbali akiishi katika kudhalilishwa na mazingira duni na ya ukandamizaji. Kwa kuliona hilo, Allah Mtukufu kupitia mfumo sahihi wa maisha [Uislamu] akamuondolea mwanamke unyonge, udhalili, dhulma, uonevu na unyanyasaji.

Katika kuzungumzia uhusiano uliopo baina ya mwanaume na mwanamke, Allah Ta’ala anasema: “Enyi watu! Hakika sisi tumekuumbeni kutokana na mwanaume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Mbora wenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni aliye mchamungu zaidi.” [Qur’an, 49:13]. Hivyo, Uislamu unapinga vikali dhana ya uongo iliyokuwa imeenea sana wakati wa kuteremshwaQur’an kuwa, mwanamke ni mtu duni, anayedhalilishwa na asiye na umuhimu katika jamii.

Haki za wanawake na vazi la hijabu
Kwa miongo mingi wasomi wa elimu za kimagharibi, wanafalsafa na watetezi wa haki za wanawake wamekuwa wakilinasibisha vazi la sitara la Hijabu na kumnyima mwanamke haki na uhuru wa kuvaa. Wakitumia ujinga wa wale wasioujua Uislamu, wanaharakati wa haki za wanawake wamekuwa wakidai kuwa hukumu zote za mavazi na stara ni za uzushi uliokuja baadae na si mambo yanayoamrishwa na Qur’an.

Baadhi ya Waislamu, kwa kuathiriwa na mawazo ya kimagharibi, nao wamekuwa wakifuata mkumbo huo na kujiingiza katika madai ya haki za wanawake kuanika viwiliwili vyao, huku wakisahau kuwa kufanya hivyo ni kuhalifu hukumu za stara ya Kiislamu. Uislamu umekuja kumuongoza mwanadamu – awe mwanamume au mwanamke katika kutekeleza haki za Muumba wake, kwa kumtambua, kumuamini, kumuabudu na kumtii.

Haya yanadhihiri katika zama hizi ambazo idadi kubwa ya wanawake wa Kiislamu wanaojitambua na kujiheshimu wakiwamo mawaziri, walimu wa shule, wahadhiri wa vyuo vikuu na watendaji wengine wa serikali wanavaa vazi la stara la Hijab huku wakitoa mchango wao katika kulitumikia taifa.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close