-

Sheikh: Saudi Arabia haijaharibu maeneo ya historia

Imefafanuliwa kuwa maeneo takribani yote yaliyobeba historia ya Uislamu nchini Saudi Arabia tangu enzi za Mtume Muhammad [rehema za Allah na amani zimshukie] na hata baada ya kufariki kwake, bado yanatunzwa na kulindwa tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu.

Ufafanuzi huo umetolewa na Sheikh Haruna Jumanne Kapama katika mahojiano maalumu na gazeti imaan, akijibu tuhuma kuwa, Saudi Arabia imekuwa ikiharibu maeneo ya historia ya Uislamu.

Sheikh Haruna, maarufu pia kama Abu Hafswa, mwenye uzoefu wa kuhudumu katika kusafirisha mahujaji kwa miaka 12 sasa, anasema ametembelea maeneo takribani mengi ya kihistoria na kukuta bado yapo, bali yameboreshwa.

Ukweli na usahihi hakuna sehemu ambayo inagusa dini yetu ambayo Saudi Arabia imebadilisha, ila kuna maeneo yamefanyiwa maboresho ambayo ni muhimu kuhakikisha maeneo hayo hayaharibiki kabisa au kupotea,” alisema Sheikh Kapama.

Sheikh Kapama aliyataja baadhi ya maeneo muhimu ya historia ya Uislamu ambayo yapo mpaka sasa miongoni mwayo ni Bustani ya Saqīfah Banī Sā’idah, mahali ambapo Swahaba Abubakar alichaguliwa kuwa Khalifa wa kwanza baada ya Mtume Muhammad kufariki.

Maeneo mengine aliyoyataja ni soko la Madina ambalo Mtume ndio alikuwa akifanyia biashara zote na misafara, na pia misikiti kadhaa kama Masjidil Alghamama, Masjidil Abubakar Sidiq, Masjidil Ali, Masjidil Umar, Masjidil Othman. Misikiti yote hiyo, ambayo baadhi Mtume alikuwa akiswali Swala ya Idd, bado ipo mpaka sasa.

Sheikh Kapama aliongeza kuwa, baadhi ya misikiti hiyo haiswaliwi ila bado imehifadhiwa kwa ajili ya kumbukumbu muhimu kwa Waislamu. Akitolea mfano wa juhudi za utunzaji wa historia kupitia Masjidil Ijaba, Sheikh Kapama alisema, hoteli karibu zote zilizokuwa karibu zimevunjwa lakini msikiti huu umebakia. Masjidil Ijaba ni msikiti ambao Mtume aliomba mambo matatu, mawili yakakataliwa, moja likakubaliwa.

Msikiti mwingine ni Masjid Abuzar Ghifari, sehemu ambayo Mtume, akiwa katika Swala, alipewa ujumbe na Malaika Jibril kutoka kwa Allah Aliyetukuka kuwa, atakayemsalia Mtume; Mwenyezi Mungu naye atambariki na kumshushia rehema zake. Sheikh Kapama alisema, licha ya majengo yaliyozunguka msikiti huo kuvunjwa, msikiti huo umeachwa.

Hata hivyo Sheikh Kapama alisema kuwa yapo baadhi ya maeneo ambayo imekuwa vigumu kwa mahujaji kufika kwa sababu ya umbali na sababu za kidini ila hayajaharibiwa kama inavyodaiwa.

Yapo maeneo ambayo tunaona shida kupeleka Mahujaji kwa sababu tu hatuwezi kufika. Kwa mfano, kisima cha yule Myahudi Rummat al Giffari, ambaye alikuwa akitesa watu wa Madina kwa kukifunga siku ya Ijumaa jioni kwenda Jumamosi kwa sababu ya Sabato ambayo alikuwa akiitikadi yeye,” alisema Sheikh Kapama.

Sheikh Kapama alisema, kisima hicho bado kipo lakini sasa hivi wameweka uzio kwa sababu baadhi ya mahujaji waliokuwa wanaenda kule, walikuwa na itikadi za kishirikiana ikiwemo kuchukua michanga.

Abuu Hafswa aliongeza kuwa, hata yale maeneo ya kihistoria ambayo yalichipuka baada ya kufariki Mtume Muhammad bado yapo mpaka sasa. Akitoa mfano, Sheikh Kapama aliitaja Ikulu ya Abdillah bin Zubeir aliyetawala miaka kadhaa baada ya Mtume Muhammad kufariki, eneo ambalo lipo mpaka sasa katika mji wa Madina.

Kwa mujibu wa Sheikh Kapama, wale wanaosema kuwa Saudi Arabia imeharibu maeneo ya kihistoria wanafanya hivyo ikiwa ni sehemu ya propaganda chafu dhidi ya taifa hilo.

Kwa hiyo ukimsikia mtu anasema nchi ya Saudi Arabia inaharibu maeneo ya kihistoria, hizo ni propaganda tu zisizokuwa na msingi wowote na zinazopaswa kupuuzwa.”

Aliongeza: “Mimi naamini Saudi Arabia ni nchi iliyolinda vyanzo vya kihistoria tena kwa gharama, ulinzi na kila kitu. Kajaribu kuupanda Mlima Uhud hivi sasa uone kama hautashushwa na wanajeshi. Kwa hivyo, haya ni maneno ya uongo ambayo Watanzania wanatakiwa wayapuuze.”

Aidha Sheikh Kapama aliwaasa Waislamu ambao hawajaenda kuhiji kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuwafikisha huko ili kupata ladha halisi ya dini yao ya Uislamu. “Tunashajiisha watu watekeleze ibada hii ya Hijja kwa sababu ukitekeleza ibada hii unakuwa umetekeleza nguzo ya tano, lakini inakuwa umepata bahati ya kufika kwenye yale maeneo ya kihistoria ambayo ndio kuna chemchem na chimbuko la dini yetu,” alisema Sheikh Kapama. Sheikh Kapama aliongeza:

Hii [Hijja na kutembelea maeneo matukufu] inazidisha yakini kwa kiasi kikubwa sana katika moyo wa Muislamu mbele yake Allah Sub’hanahu Wata’ala.”

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close