-

Sheikh Kyebanja ashangazwa Watanzania kusifika kwa ushirikina

“Ndugu zangu wa kutoka Tanzania nyie ni lazima mchunge sana. Mimi nimeishi Uganda na Kenya na huko kuna waganga wengi sana wanaojisifu kuwa wao ni wachawi kutoka Tanzania. Huko kwetu Uganda unaweza kukutana na mtu akakuambia ‘mimi usinichezee, mimi ni mganga kutoka Tanzania,”.

Hayo ni maneno ya Sheikh Ibrahim Kyebanja aliyoyaongea katika kongamano la kwanza la Afrika Mashariki lililofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee hivi karibuni.

Katika hotuba yake Sheikh Kyebanja alisema, licha ya shirki kuwa ndiyo dhambi kubwa zaidi mbele ya Allah, Waislamu wengi nchini Tanzania na katika bara la Afrika wamedidimia katika ibada ya kuabudu makaburi, mizimu, kwenda kwa wachawi pamoja na kupiga ramli. Sheikh Kyebanja alisema:

“Nyumba nyingi za Waislamu zimetawaliwa na mambo ya kishirikiana, hivyo ni lazima Waislamu waonywe juu ya dhambi hiyo mbaya na kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.”

Hata hivyo Sheikh Kyebanja alikiri juu ya kuwepo kwa hali mbaya ya ushirikina katika nchi za Uganda na Kenya ambako kunatajwa kuwa na waganga wengi wa kienyeji kutoka Tanzania na huku wakijisifu kuwa wao ni mabingwa wa kuwaroga watu.

Sheikh Kyebanja alisema, changamoto kubwa iliyopo ni Waislamu wengi kutopenda kusoma dini yao na wakati huo huo wakishindwa kuwapeleka watoto wao madrasa.Kufuatia hali hiyo, Sheikh Kyebanja aliwataka Masheikh, walinganji na wazazi kutenga muda maalum kwa ajili ya kulingania dini kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuinusuru jamii na kufanya dhambi ya shirki.

“Tusiwe tunaswali na wakati mwingine tunakwenda kuyaabudu makaburi, tusiwe tunaswali saa nyingine tunakwenda kwa wachawi na wapigaji wa bao (ramli),” aliongeza Sheikh Kyebanja.

Katika hatua nyingine Muhadhiri huyo wa Dini ya Kiislamu alitoa wito kwa wanawake wa Kiislamu kumtegemea Mwenyezi Mungu pindi wanapokabiliwa na mitihani ya kimaisha.

“Akina mama muogopeni Mwenyezi Mungu katika kumshirikisha Mwenyezi Mungu na muende kuwaelimisha ndugu na jamaa zenu muwaoneshe ubaya wa shirki ili wajue ya kwamba wakifanya shirki watakaa jahannam milele na milele,” alibainisha Sheikh Kyebanja na kunukuu Aya isemayo:

“Hakika Allah hasamehi dhambi ya kushirikishwa na kitu, lakini husamehe yasiyokuwa yasiyokuwa hayo (ushirikina) kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Allah, basi bila shaka amekwishapotea upotofu ulio mbali na haki,” (Qur’an, 4:116).

Ili kufikia lengo Sheikh Kyebanja aliwataka Masheikh, Maimamu na walinganiaji kutoka nchi za Afrika Mashariki kuandaa darasa za tawhiid ndani ya misikiti yao ili iwe sababu ya Waislamu kujua Dini yao hususani katika kipengele cha kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close