-1. Habari1. TIF News

Sharjah, TIF zafanikisha matibabu ya moyo

Wagonjwa 21, milioni 700 zaokolewa

Jumuiya ya Sharjah Charity International kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imefanikiwa kuwafanyia upasuaji wa moyo jumla ya watoto 17 na watu wazima wanne katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuokoa kiasi cha Shilingi za Kitanzania zaidi ya milioni 700.

Upasuaji huo ulifanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 20 hadi 22 mwaka huu chini ya uratibu wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) yenye makao yake makuu mkoani Morogoro, ambapo mwisho wa zoezi hilo, Mwenyekiti wake, Aref Nahdi, aliishukuru serikali kwa kuruhusu kuingiza vifaa vya tiba na matibabu hayo bila kodi na pia kwa kuwaunga mkono.

Matibabu hayo yalitolewa bure kwa walengwa kwa msaada wa madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Al-Qassimi iliyopo katika jiji la Sharjah katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Katika siku tatu za matibabu hayo yaliyoendeshwa na madak.tari bingwa watatu, wawili wa upasuaji na mmoja wa usingizi; siku ya kwanza wagonjwa nane walipatiwa matibabu, siku ya pili tisa na siku ya tatu wanne.

Madaktari wageni waliohusika na matibabu hayo ni pamoja na Dkt. Ahmed Al Kamali kutoka UAE, Dkt. Mahmoud Abdulatif Al-soufy kutoka nchini Syria na Dkt. Suresh Kailasam Sivamurthy kutoka India ambao wote wanafanya kazi UAE. Madaktari hao ambao pia walishirikiana na madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete waliweza kuwatibu moyo wagonjwa 21 bila kufungua kifua kupitia teknolojia ya ‘Cardiac catheterization’ ambapo mgonjwa hutobolewa mishipa maalumu iliyopo mapajani na kuzibwa matundu ya moyo kupitia kifaa maalumu.

Kwa mujibu wa Dkt. Naiz Majani, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto katika taasisi
ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI), zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Kambi hii imewahudumia watoto wadogo na watu wazima ambao walizaliwa na matatizo ya moyo lakini walishindwa kutibiwa wakati walipokuwa wadogo. Mdogo kuliko wote ana umri wa miezi minne na mkubwa ana miaka 49.”alidokeza Dkt. Naiz.

Kauli ya wageni kutoka Sharjah

Kwa upande wake, kiongozi wa jopo la madaktari hao bingwa kutoka Jumuiya ya Sharjah Charity International, Dkt. Ahmed Al Kamali amesema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kufika tena Tanzania na kuwahudumia watoto wenye matatizo ya moyo.

Tunafurahi kuwa sehemu ya juhudi ya kuwasaidia watoto wa Kitanzania wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo. Tumekuja hapa tukiwa kama ndugu, marafiki na watu wa karibu kwa lengo moja la kuwasaidia wototo wetu hawa,”alisema.

Aidha, Dkt. Al Kamali aliishukuru Serikali ya Tanzania, Ubalozi wa UAE hapa nchini pamoja na Taasisi ya The Islamic Foundation kwa kufanikisha zoezi hilo. Hii ni mara ya tatu kwa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) kuleta madaktari bingwa hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma
za upasuaji moyo kwa watoto.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, TIF kwa kushirikiana na taasisi ya Sharjah Charity wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji jumla ya watoto 50 na watu wazima wanne. Kauli za madaktari, JKCI Dkt. Bashir Nyangasa, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), amewashukuru madaktari hao kutoka Sharjah kwa imani kubwa walioionesha katika kuwahudumia wagonjwa wa moyo kwa technolojia hiyo mpya ya isiyohusisha upasuaji.

Namshukuru Allah, na nipende tu kuishukuru taasisi ya Sharjah Charity International na The Islamic Foundation kwa imani yao na huduma yao walioionesha kwa Watanzania,” aliongeza kusema Dkt. Nyangasa.

Dkt. Nyangasa, ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu hospitalini hapo alisema kuwa ujio wa madaktari wa moyo hapa nchini, umeleta mapinduzi makubwa na yenye tija katika sekta ya afya kwani wamekuwa wakiisaidia JKCI kutoa huduma za upasuaji moyo kwa mafanikio makubwa.

Kwa upande wake, Dkt. Naiz Majani amesema huduma ya upasuaji moyo watoto katika taasisi hiyo imezidi kuimarika tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 2015 ambapo hadi sasa wameweza kutibu jumla ya watoto 370. “Ujio wa madaktari kutoka Sharjah una manufaa makubwa kwani katika miaka mitatu iliyopita, huduma ya upasuaji mdogo wa moyo haikuwa ikitolewa hapa Tanzania, hivyo watoto wote waliohitaji kupatiwa huduma hiyo walikuwa wakisafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu,” alibainisha Dkt. Naiz na kuongeza:

“Kupitia kambi mbalimbali za matibabu ya moyo, mwaka huu wa 2018 tumeweza kuwafanyia upasuaji watoto 39 huku watoto wengine zaidi ya 100 wakisubiri kufanyiwa upasuaji mdogo,” alifafanua daktari huyo.

Akitoa mchanganuo wa gharama halisi ambazo taifa lingeingia kama huduma hiyo ingetakiwa malipo, matibabu ya kuziba vitundu kwa watu 16 yangegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 30 hadi 35 kwa mtu mmoja. Kwa mujibu wa Dkt. Naiz, hadi sasa kuna zaidi ya wagonjwa 450 wanaosubiri kufanyiwa upasuaji ambapo kati yao zaidi ya 125 wanahitaji kufanyiwa upasuaji mdogo wa bila kufungua kifua.

Kuhusu mafanikio, Dkt. Naiz alisema kwa sasa JKCI ina uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji moyo na mwishoni mwa mwaka huu itaanza kutoa huduma ya upasuaji mdogo yenyewe. Dkt. Naiz aliendelea: “Uwezo wa madaktari wa ndani umeendelea kukua siku hadi siku tofauti na awali ambapo idadi ya madaktari wanaokuja kutoka nje walikuwa wengi. Tunategemea ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo tutaanza kutoa huduma hii wenyewe baada ya vifaa vyetu kufika.”

Kauli za Mwenyekiti wa TIF akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhudumia wagonjwa hao wa moyo, Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi aliishukuru serikali kwa kuruhusu kuingizwa nchini vifaa tiba vya matibabu hayo bila ushuru. Nahdi pia aliishukuru serikali na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kuiunga mkono The Islamic Foundation huku akiahidi kuendelea kuleta madaktari bingwa wa moyo kutoka UAE ili kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa kwenda kutibiwa nje.

Tunamshukuru sana Rais Magufuli na serikali yake kwa ujumla kwa kutuunga mkono katika hili. Kitu kingine ambacho tumeshauriana na madaktari wa JKCI ni kuhusu kuleta timu nyingi za madaktari kuliko timu hizi, na ni mategemeo yetu Allah atatuwezesha,” aliongeza kusema Nahdi.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close