-

Saruji ya Dangote kujenga Makao Makuu Dodoma

Na Jasmine Shamwepu

TAASISI ya Dangote inayojishughulisha na uzalishaji wa saruji kupitia kiwanda chake kilichopo mkoani Mtwara imesema itafungua kituo kikubwa cha uuzaji wa saruji mkoani Dodoma. Mbali na hilo, kampuni hiyo ina mpango wa kujenga bandari kavu ambayo itatoa huduma katika mikoa na nchi jirani kwa lengo la kuwarahisishia upatikanaji wa saruji ya uhakika. Makamu wa Rais wa kampuni hiyo, Alhaji Saada Ladan alisema hayo mjini Dodoma wakati wa mazungumzo na uongozi wa mkoa wa Dodoma kuhusiana na nia yao ya kuwekeza na kuwezesha ujenzi wa miji ya makao makuu. Amesema mji wa Abuja umetumia ramani ya Makao makuu ya nchi ya Tanzania Dodoma na unafanana katika maeneo yote na hata watafiti walioshiriki kupanga mji wa Abuja walitoka Tanzania na kusisitiza kuwa tayari wameshafungua ofisi katika mkoa wa Dodoma ambayo itashiriki kikamilifu katika usambazaji wa saruji za biashara lakini pia kuwezesha ujenzi wa makao makuu. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, alisema mazungumzo yake na uongozi wa Dangote yalienda vizuri na kwamba kampuni hiyo imeonesha utayari wa kushiriki katika mpango wa mkoa wa Dodoma wa kukarabati majengo ya shule za msingi na sekondari. Naye Meneja wa Dangote mkoa wa Dodoma Mselem Ally amesema watahakikisha saruji ya uhakika yenye ubora wa viwango mbalimbali katika mkoa wa Dodoma inapatikana.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close