-6. Malezi

Namna ya kufikia suluhu ya ugomvi katika familia

Migogoro ni sehemu ya maisha ya wanadamu, lakini ni vile unavyokabiliana nayo ndiyo huleta tofauti. Katika maisha ya ndoa, ni kawaida kwa wawili waliooana kugombana. Hata kama wawili walioana ni Waislamu, kutokulewana hutokea tu kwa sababu mara nyingi watu hawa wanatoka katika utamaduni na malezi tofauti.

Kama nilivyosema, vile unavyokabiliana na mgogoro ndiyo huleta tofauti. Mnaweza kugombana lakini mkadhibiti ugomvi wenu na kutafuta suluhu kwa njia nzuri ili ugomvi usiwe mkubwa zaidi, na kushirikisha watu wengi. Leo ntakuletea baadhi ya nukta muhimu za namna ya kudhibiti hali ya kutokuelewana.

Muda sahihi:

Ni muhimu sana tatizo lililojitokeza lijadiliwe katika muda sahihi. Ni kosa kubwa kujadili tatizo wakati wahusika mna hasira. Acheni hasira zipungue ndiyo mjadili mambo yenu, vinginevyo kama mna jazba, hamuwezi kuelewana. Subira ni muhimu.

Wakati fulani, unaweza kujikuta unashindwa kuhimili hasira. Fuata ushauri wa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) juu ya namna ya kudhibiti hasira katika hadith iliyosimuliwa na Abu Dharr:

“Kama mmoja wenu amepatwa na hasira hali ya kuwa kasimama, basi akae. Hasira zikiondoka, vema; vinginevyo alale.”

Katika hadith nyingine iliyosimuliwa na Atiyyah as-Sa’di, Mtume ameshauri aliyepandwa na hasira akachukue udhu kwani hasira zinatokana na shetani na shetani asili yake ni moto, ambao huzimwa kwa maji. hadith zote hizi zimepokelewa na Imam Abu Dawud. Pia, katika hadith nyingine iliyopokewa na Imam Bukhari, Mtume aliwashauri Maswahaba kuwa wanapopandwa na hasira, basi waombe kinga ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka dhidi ya shetani.

Kutafuta suluhu ya tatizo hali mtu ana hasira ni jambo la hatari kwani unaweza kusema maneno ambayo yanachochea zaidi moto wa ugomvi na hatimaye ukajutia. Ni kwa kujua hasara ya kutawaliwa na hasira Mtume ndiyo maana katika hadith iliyosimuliwa na Abu Huraira, Mtume amesema:

“Mtu mwenyewe nguvu si yule anayeweza mieleka, bali ni yule anayeweza kudhibi hasira.” [Muslim].

Katika hadith nyingine pia ya Abu Huraira, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliombwa ushauri na mtu mmoja, naye akamwambia: Usiwe na hasira.” Na alipewa jibu hilo hilo hata baada ya kuuliza mara kadhaa.

Dhibiti sauti:

Kwanza haifai kuingia katika mazungumzo ya kutafuta suluhu hali umekasirika, kama tulivyoona lakini kama imetokea jazba zimepanda basi jaribu kudhibiti sauti yako. Usipaze sauti kwani hakuna tija inaweza kupatikana katika mazungumzo ambayo watu wanafokeana. Suala hapa siyo kufokeana tu lakini pia ni namna ya kuzungumza. Lugha fulani hazifai kwa mtu ambaye mnapaswa kuheshimiana .

Kwa uzoefu wangu, lugha mbaya zisizo na stara zinaondosha mjadala kutoka kwenye suala lenyewe linahitaji suluhu na kuhamia kwenye maumivu ya kutusiwa.

Acha dhana mbaya:

Dhana mbaya imekatazwa. Kama utadhani, basi iwe dhana nzuri. Hakuna kitu kinaleta shida katika familia kuliko kudhaniana vibaya. Hutokea, mathalan, mke amemuona mume anaongea na mtu mwingine; naye mke akaamini kabisa kuwa kuna jambo baya liliendelea, kumbe sivyo kabisa!

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi…”. Naye Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Epuka dhana, kwani dhana ni uongo mkubwa…” [Bukhari, Muslim].

Sikilizaneni:

Hiyo nukta iliyopita ya kutodhaniana vibaya inaenda sambamba na nukta ya kusilikizana. Huenda umeona jambo, basi siyo mbaya ukampa nafasi mwenzako ya kutoa maelezo kuhusu jambo hilo, ka nini liko hivyo. Mara nyingi tu imetokea watu kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa ambazo hazijamilima.

Ijulikane pia kwamba, hata kwenye hukumu za dini imetajwa kuwa haifai kumuhumu mtu bila kumsikiliza. Katika hili hebu rejea kisa cha Nabii Daud na mwanawe Suleiman katika Surat al – Anbiya, kisa ambacho kinahimiza kusikiliza upande wa pili katika mgogoro.

Usilikimbie tatizo:

Wakati mwingine, watu hulikimbia tatizo na badala yake kuishia kujadili dalili za tatizo. Hebu jadilianeni kwa uwazi kuliko kufichaficha. Wakati fulani mwanamume hakai nyumbani kwa sababu, labda kuna jambo la kero linatokea. Hata hivyo, wanapojadiliana na mkewe, hasemi tatizo halisi labda ili kuhofia kuumiza hisia za mwenzake. Hii haifai. Likabilini tatizo moja kwa moja kwani hata Waswahili husema, mficha uchi hazai.

Tulieni katika mada husika:

Jambo jingine muhimu ni kujadili suala husika na kulimaliza kuliko kuhama hama na kuingiza mambo yasiyokuwepo au mambo yaliyopita. Hili ni tatizo kubwa ambao hupelekea kutopatikana suluhu ya migogoro majumbani. Utasikia, na siku ile ulifanya hivi… na siku ile … na siku ilee. Jambo hili si jema.

 Heshiminianeni:

Jiulize kwa nini mnatatua tatizo? Ni kwa sababu mnataka kutafuta suluhu ambayo itawawezesha kuendelea kuishi na kutafuta radhi za Allah Azza Wajalla. Kama hivyo ndivyo, heshimianeni kwani baada ya yote, mnaendelea kuwa pamoja kujenga familia yenu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close