-

Namna corona ilivyobadili Ramadhan ya mwaka huu

Kufuatia ulimwengu kukabiliwa na ugonjwa wa corona, tofauti zimeanza kudhihiri katika Ramadhan ya mwaka huu ukilinganisha na namna mfungo huu ulivyozoeleka miaka iliyopita.

Tofauti hizo zimeonekana sio tu hapa nyumbani Tanzania, bali pia katika nchi za jirani na hata kimataifa kwa viwango vinavyopishana.

Makka, Madina

Hivi sasa, nchini Saudi Arabia, Waumini hawaruhusiwi kushiriki katika ibada za sala, ikiwemo sala ya sunna maalumu ya tarawehe katika Misikiti Miwili Mitukufu yaani ule wa Makka, Masjidil Haram na ule wa Madina, Masjidi Nnabawi.

Picha za mnato na video kutoka mji huo zinaonesha maeneo mbalimbali ya msikiti huo yakiwa matupu, kinyume kabisa na kawaida ya hali inavyokuwa katika kipindi cha Ramadhan.

Kwa sasa, sala za tarawehe zinazosaliwa katika misikiti hiyo zinahusisha viongozi wa misikiti hiyo na watumishi tu. Pia, tarawehe inasaliwa rakaa 11 (pamoja na swala ya Sunna ya Witri), huku dua ya Qunut nayo ikifupishwa na kulenga zaidi katika kumuomba Mwenyezi Mungu aiondolee dunia balaa la maradhi ya corona.

Itikaf, ibada ya kukaa msikitini kwa lengo la kumuabudu Mwenyezi Mungu tu hususan katika siku 10 za mwisho za mwezi Mtukufu wa Ramadhan nayo mwaka huu haipo kwa sababu hakuna Waumini kutoka katika jamii za miji hiyo au wageni wanaoingia msikitini humo.

Takwimu zinaonesha kuwa, kwa kawaida, katika miaka ya nyuma, zaidi ya Waumini 100,000 wamekuwa wakikaa itikaf katika misikiti hiyo miwili katika siku 10 za mwisho za mwezi wa Ramadhan. Pia, kwa kawaida, misikiti hiyo miwili mitukufu inavutia mamilioni ya Waumini katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan – kama inavyokuwa katika miezi ya ibada ya faradhi ya hijja.

Sababu inayofanya Waumini wengi waelekee Makka kipindi cha Ramadhan ni ukweli kwamba, ibada katika misikiti hiyo zina malipo makubwa katika kipindi hiki, kwani Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema fadhila za ibada ya Umra ndani ya mwezi wa Ramadhan inalingana na ujira wa hijja.

Tanzania

Kwa hapa Tanzania, utofauti wa Ramadhan kati ya mwaka huu na miaka iliyopita ulianza kujionesha tangu wakati tukikaribia kuupokea mfungo huu mtukufu, ambapo kinyume na ilivyozoeleka mwaka huu hakukuwa na shughuli na matukio ya kuupokea mwezi.

Kwa kawaida, miaka ya nyuma, kumeshuhudiwa taasisi kadhaa zikiandaa matukio makubwa ya kujadili mambo ya Kiislamu katika muktadha wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mwaka huu, kipindi cha mwezi Shaaban ambapo mengi ya matukio hayo kwa kawaida hufanyika; kulikuwa tayari na tahadhari dhidi ya corona sio tu nchini Tanzania, mataifa mengine ya Afrika ya Mashariki na dunia kwa ujumla yalishakuwa kwenye hali ya tahadhari ya maradhi ya corona, na hivyo matukio ya aina hiyo, kwa sehemu kubwa, yalishazuiwa.

Sala za mita moja – moja

Huenda hii ni mara ya kwanza katika historia ambapo Waislamu wamelazimika kusali huku kila mmoja akiwa umbali wa mita moja kutoka kwa mwenzake – ikiwa ni sehemu ya tahadhari dhidi ya kuenea kwa maradhi ya homa ya mapafu ya corona.

Hali hii ni kinyume na ilivyozoeleka, ambapo kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), maamuma wanatakiwa kutoacha nafasi baina ya mtu na mtu.

Ukilinganisha na nchi nyingine, Waislamu wa Tanzania wana nafuu kwani walau wao bado wanaruhusiwa kuendelea kwenda misikitini na kusali sio tu sala za faradhi bali hata za sunna. Katika baadhi ya nchi, kuongezeka kwa hali ya maambukizi kumepelekea misikiti kuendelea kufungwa na watu kutakiwa kusali nyumbani.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili unaonesha kuwa, hata Tanzania, licha ya ruhusa ya kusali misikitini, baadhi ya Waumini, hasa wenye maradhi sugu na wazee, wameamua kubaki nyumbani na kutekeleza sala zao zote huko, zikiwemo za faradhi na za sunna. Pia, wapo baadhi ya watu walioamua kusali nyumbani sunna ya tarawehe kwa sababu ya kutoridhishwa na haraka ya maimamu na usomwaji wa sura fupi.

Mashindano ya Qur’an

Katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan imezoeleka kuwa, kisomo cha Qur’an kupitia mashindano mbalimbali hutamalaki kila kona ya nchi. Mwaka huu mambo ni tofauti kabisa kutokana na janga la corona. Mashindano ya Qur’an hayajaonekana; na hayataonekana mwaka huu.

Kama ulikuwa ukisubiri kupata raha kama ya miaka yote ya kuwaona vijana wakisoma Qur’an na kutimiza ndoto zao za kuwa mabingwa wa kuhifadhi wa nchi, Afrika au dunia, basi jua kuwa mwaka huu hamna.

Jambo la kusikitisha ni kuwa, kabla ya kuibuka kwa corona, waendeshaji mashindano hususan yale ya kitaifa na kimatafa, walishaanza maandalizi katika ngazi za mchujo na mipango mingine ya matukio makuu ya fainali.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tanzania, Sheikh Othman Kaporo waandaaji wa mashindano ya kimataifa amesema walishakamilisha maandalizi kwa asilimia 80, ikiwamo ujenzi wa nyumba ambayo ilikuwa iwe zawadi kwa mshindi wa kitaifa wa juzuu 30. Fainali hiyo ilikuwa ifanyike jijini Dodoma.

Mashindano mengine makubwa yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu, na ambayo pia hayatakuwepo ni yale ya Afrika yanayoendeshwa na taasisi ya Al – Hikma Foundation na kufanyikia kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Mashindano haya huenda ndiyo yanayoshikilia rekodi ya mahudhurio Afrika, kama sio duniani, ambapo hujaza uwanja mzima.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Al – Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishk mpaka mashindano hayo yanatangazwa kusitishwa, maandalizi yalishakamilika kwa asilimia 90, na hivyo wamepata athari kubwa.

Moja ya kivutio kikubwa cha mashindano hayo mwaka huu, hususan kwa upande wa zawadi ukiacha fedha, ni pamoja na tiketi ya Hijja kwa mshindi; na vilevile tiketi ya Umra kwa mshindi, wazazi wake wawili na mwalimu wake.

Hamna mialiko ya futari

Kijamii, kitu ambacho kitaonekana dhahiri kupungua katika Ramadhan hii ni mialiko ya futari, ambayo kwa kawaida imekuwa ikihusisha sio tu Waislamu bali hata watu wa dini nyingine.

Tukiwa tumevuka zaidi ya wiki tangu Ramadhan ianze, kutokuwepo kwa shamrashamra za mialiko ni jambo lililo wazi. Futari katika Ramadhan hii ni suala la kifamilia zaidi kuliko kijamii. Hata misikitini, hakuna futari – yote kwa hofu ya kueneza corona.

Hata hivyo, kutokuwepo kwa aina ya ufutarishaji ya kualika watu ni fursa kwa watoaji kusaidia watu ambao ni wahitaji wa kweli na ambao baadhi yao wamepoteza kazi kutokana na corona.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close