-

Nahdi awashukuru waliohudhuria, agusia mabadiliko ya Kongamano

Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation [TIF], Aref Nahdi ameonesha kufurahishwa na mahudhurio makubwa ya watu katika kongamano la pili la Misk ya Roho lililofanyika Oktoba 28 mwaka huu na kubainisha kuwa anawashukuru wote waliohudhuria.

Nahdi amesema mahudhurio hayo makubwa ni ishara kuwa Waislamu wanaipenda dini yao na hivyo kuwaomba wazidi kushiriki makongamano mengine ili kuusukuma mbele Uislamu.

Katika shukrani zake hizo pia Nahdi amewashukuru wahadhiri waliwasilisha mada akisema wameonesha uwezo wakubwa na kufanikiwa kukata kiu ya umati mkubwa uliosheheni ukumbini na shauku ya kuwasikiliza wahadhiri hao.

Wahadhiri wametia fora, ukiangalia watu ukumbini utabain hilo, kwani watu walikuwa na bashasha muda wote, hii ni ishara waliridhika na watoa mada,” alisema Nahdi.

Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi akimsikiliza sheikh Bizimana katika kongamano la Misk ya roho

Wahadhiri waliowasilisha mada katika l kongamano hilo lililovutia watu wengi ni pamoja na Sheikh Yusuf Abdi na Sheikh Jamaldin Osman kutoka Kenya, Sheikh Zuberi Bizimana [Burundi], Sheikh Ally Kajura [Rwanda] na Sheikh Muhammad Abduweli kutoka Uganda. Na kwa hapa nchini walikuwemo kina Sheikh Dourmohamed Issa, Sheikh Ally Jumanne na Sheikh Abdulrahman Mhina [Baba Kiruwasha].

Aidha Nahdi amewashukuru vijana waliojitolea katika kongamano hilo akisema wamefanya kazi kubwa sana ambayo mwenye uwezo wa kuwalipa haswaa ni Mwenyezi Mungu:

Kwa hakika vijana hawa wakujitolea wamefanya kazi kubwa sana, kila mtu nadhani aliyoona jinsi ukumbi ulivyonawiri, mi niseme Allah ni mbora zaidi katika malipo kwani sisi TIF hatuna cha kuwalipa.”

Aidha, alitumia jukwaa la Kongamano hilo kuwakabidhi tuzo wahadhiri wa kongamano pamoja na wadhamini kwa juhudi zao kubwa za kufanikisha kongamano hilo. Wadhamini waliyokabidhiwa tuzo ni wale wa Platinum ambao ni Asas Dairies Ltd ya Iringa, Afya pure drinking water na Azam TV.

Kwa upande wa dhahabu [Gold] ni Usangu logistics[T] Limited, Dar fresh Milk, O-GAS na Fedha (Silver) ni kampuni ya Mafuta ya ATN. Na shaba [Bronze sponsors] ni MOROBEST, Simba Oil, Cam Gas, Car Center na Carmel Floor Milk. Wengine waliyofanikisha Kongamano hilo na kuzawadiwa ni runinga ya Mahassin, Horizon TV ya Kenya na Imaging Smart.

Mabadiliko katika kongamano

Aidha Nahdi alidokeza juu ya uwezekano wa kubadili ukumbi wa kufanyia makongamano kwamba badala ya kufanyia ukumbini basi iwe kwenye viwanja vya wazi. Hatua hiyo ya Nahdi inatokana na kile anachosema ni gharama kubwa katika kuandaa kongamano linalofanyika ukumbini akitolea mfano wa kongamano la hivi karibuni la Misk ya Roho lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 130.

Makongamano haya yanagharimu sana, mfano kongamano hili tu limetugharimu zaidi ya shilingi milioni 130, hizo ni fedha nyingi, ifahamike hawa wahadhiri wanakuja kwa ndege na wanalala hoteli yenye hadhi sio hizi za kawaida,” alisema Nahdi

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close