-

Muntada Aid watembelea TIF

Uongozi wa taasisi ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu, Muntada Aid, umetembelea Makao Makuu ya The Islamic Foundation (TIF) mjini Morogoro pamoja na vitengo mbali mbali vya taasisi hiyo.

Katika ziara hiyo ya kujenga urafiki na ushirikiano kati ya Muntada Aid na TIF, ujumbe wa Muntada Aid ulipokelewa na mwenyeji wao Mwenyekiti wa TIF Aref Nahdi. Ujumbe huo ulikuwa wa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Sheikh Hamid Azad aliyeongozana na Meneja wa Mradi wa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto wadogo ujulikanao kama Little Hearts, Ndugu Kabir Miah.

Akizungumza katika Ofisi za Makao Makuu ya TIF, Sheikh Hamid alisema amefurahia sana kutembelea Makao Makuu ya TIF na kwamba anataraji ushirikiano unaokusudiwa kujengwa kati ya Muntada Aid na TIF utaleta mafanikio makubwa katika nyanja za huduma kwa jamii.

“Tunataraji kufanya kazi na TIF siku zijazo na tunaamini kutapatikana tija kubwa kwa ushirikiano kati ya TIF na Muntada Aid katika kuwahudumia watu”, alisema shekh Hamid.

Naye Meneja wa Mradi wa Little Hearts, alisema kwamba mradi huo ulitambulishwa rasmi kwa bunge la Uingereza mwaka 2012 na hadi sasa madaktari kutoka Muntada Aid wameshafanya operesheni za moyo kwa watoto wadogo 1,700 duniani kote.

“Tumeshafanya operesheni mara tatu nchini Tanzania na malengo yetu ya sasa ni kuwapatia huduma ya matibabu ya moyo watoto 82 na tumeshawahudumia watoto wadogo zaidi ya 260 nchini Tanzania na tutakuja tena na tena Tanzania mpaka pale watanzania watapokasema sasa basi”, alisema Kabir.

Akizungumzia huduma za Muntada Aid, sheikh Hamid alisema wao hujishughulisha na miradi ya huduma za elimu, afya, maji safi, usafi wa mazingira, huduma za dharura kwa waathirika wa majanga mbali mbali ya asili na pia kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani wa nchi wanazofanya nazo kazi.

This is Abdul, he had an open heart operation. He is doing so well that he is being taken out of Intensive Care

Aidha Sheikh Hamid alisema hawatoi tu huduma ya matibabu ya moyo kwa watoto wadogo halafu wakaondoka bali pamoja na utoaji huo wa huduma, Muntada Aid hutoa mafunzo kwa wataalamu madaktari wa magonjwa ya moyo katika nchi hizo ili waweze kuchukua ujuzi huo na kuutumia katika kuwahudumia wagonjwa.

Katika ziara ya sasa ya madaktari hao jumla ya operesheni 82 zimefanyika katika kituo cha maradhi ya moyo cha Jakaya Mrisho Kikwete kilichoko Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Dhy Nureyn Foundation.

Kwa mujibu wa Sheikh Hamid, operesheni moja waifanyayo wao kwa kutumia vifaa maalum pasina kupasua kifua cha mgonjwa ingefanyika nje ya nchi ingegharimu dola za Kimarekani $10,000- $15,000 hivyo kufanya  matababu ya safari hii ambapo wagonjwa 82 wametibiwa kuokoa dola Milioni Moja na Laki Mbili sawa na Shilingi Bilioni 2.64 za kitanzania.

“Fedha hizi zilizookolewa zinaweza kutumiwa na serikali ya Tanzania kuboresha huduma za sekta yake ya afya na hivyo kuwanufaisha watanzania wengi zaidi. Muntada Aid inafurahi kuwa mdau wa serikali ya Tanzania katika kuwahudumia watanzania kupitia mradi wake wa Little Heart”, aliongeza Sheikh Hamid.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa Muntada Aid alisema lengo lao la muda mrefu ni kuwajengea uwezo madaktari wa Tanzania na pia kuondoa tatizo la msingi la ukosefu wa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha ili nchi zinazoendelea ziweze kujitegemea katika huduma za afya na huduma nyingine za kijamii.

Kauli dira ya Muntada Aid ni “Serving humanity to build a better and peaceful world” yaani kuwahudumia wanadamu ili kujenga ulimwengu bora na wenye amani.

Nae Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi, aliwashukuru Muntada Aid kwa ujio wao kuitembelea TIF na kwamba uongozi wa Muntada Aid ulimpigia simu kutaka kuitembelea TIF nae akawasiliana nao kuifanikisha ziara hii.

Aliwashukuru Muntada Aid kwa mambo makubwa wanayoyafanya nchini Tanzania na kwamba TIF inafurahia huduma zao nchini. Aidha, Mwenyekiti Nahdi alisema

“wamekuja kufanya matibabu ya moyo na sisi TIF tunataraji kufanya matibabu ya moyo mwezi Machi 2018 kwa kushirikiana na taasisi ya Sharjah Charity International ya UAE”.

At just 11 months old Glory is being assessed today for her life saving heart operation, by our volunteer medical team in Tanzania. Each year thousands of children are born with congenital heart disease. Through Muntada Aid Little Hearts Project, we have saved thousands of little hearts.

Mwenyekiti huyo aliuahidi uongozi wa Muntada Aid kwamba hawatajutia kushirikiana na TIF katika miradi yao kwa kuwa ushirikiano huo utakuwa wa uaminifu mkubwa  na watafurahia ushirikiano huo.

Kabla ya kuondoka mjini Morogoro, uongozi huo wa Muntada pia ulitembelea shule za Forest Hill Secondary School na Imaan English Medium Pre & Primary Schools  zilizoko mjini Morogoro ambazo zinamilikiwa na TIF pamoja na Kituo cha yatima.

Viongozi wengine wa TIF walioulaki ujumbe huo wa Muntada Aid ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TIF, Sheikh Ibrahim Twaha Ibrahim, Katibu Mkuu wa TIF, sheikh Muhammad Issa, Mkurugenzi wa Idara ya Da’wah, Sheikh Islamil R. Kundya, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Fedha, Mussa Buluki na Mkurugenzi wa Miradi F, sheikh Umar Mohamed na watendaji wa TV na Radio Imaan.

Ujumbe huo wa Muntada Aid uliondoka mjini Morogoro kurejea jijini Dar es Salaam siku hiyo ya Jumamosi kuendelea na shughuli zake huku ukiacha nyuma matumaini makubwa ya ushirikiano kati ya taasisi hizi mbili za utoaji huduma za kijamii kwa manufaa ya watanzania wote.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close