-

Mji wa Jerusalem ni Milki ya Nani?

Sehemu ya Kwanza

Historia ya mji wa Baytul Muqaddas au Yerusalemu kwa Kiswahili, Jerusalemu kwa Kiingereza ni mji wenye kuvuta hisia  za waumini wa dini kuu tatu ulimwenguni yaani Waislamu, Wakristo na Wayahud. Historia ya mji huu ni historia ngumu kuliko mji wowote ule duniani tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Wanahistoria wanaeleza kwamba mji wa Yerusalemu umeangamizwa kabisa mara tatu, umezingirwa na majeshi ya maadui mara ishirini na tatu, umeshambuliwa mara hamsini na mbili na umetekwa mara arobaini na nne.

Swali la kujiuliza, ni kwa nini hali iwe hivi kwa mji wa Yerusalem? Ni nani mmiliki wa mji wa Yerusalemu? Umiliki wake anaupata kwa misingi gani? Kuwa wa kwanza kusihi pale, kupewa Mwenyezi Mungu, kupewa na Umoja wa mataifa au kuwa mbabe kuwazidi wengine?

Tukijaribu kulitatua tatizo la mji wa Yerusalemu na Palestina kwa ujumla kwa kuangalia nani alikuwa wa kwanza kufika pale tutakumbana na kikwazo kwani kwa mujibu wa historia watu wa kwanza kufika Palestina walikuwa ni Wafoeniki au Phoenicians kwa kiingereza.

Hawa ni watu waliotoka pwani ya mashariki ya bahari Nyekundu yaani Red Sea. Hawa ndio waliotajwa katika vitabu vya kale na vile vya kidini kama Wakaanani au The Canaanites. Hawa Wakaanani ndio wenyeji wa asili wa Palestina.

Ardhi ya Kaanani ndiyo Palestina?

Palestina ikajulikana katika historia ya kale kama ardhi ya Kaanani kutokana na watu hawa Wafoeniki na wakajenga mji katika chemchem iitwayo Gihon karibu na ulipo mji wa Yerusalemu hivi sasa kati ya mwaka 4500–3500 kabla ya kuzaliwa nabii Isa (Yesu).

Baada ya Wafoeniki,  wakahamia katika ardhi hii ya Palestina watu wengine waitwao Wafilisti au Phillistines kwa Kiingereza kati ya mwaka 3500-3000. Watu hawa wametajwa katika Kitabu cha Joshua 13:3 na Samueli 6:17 kwamba waliishi katika eneo la miji ya Gaza, Ashkelon, Ashdod, Ekron na Gath.

Kiuhakika ni kutokana na wa Filisti ndiyo eneo hilo likapewa jina Palestina na Warumi walipoliteka eneo hili mwaka 63 kabla ya kuzaliwa nabii Isa. Warumi waliliita eneo hili Caesaria Palestina ambalo kwa Kiingereza ni Palestine.

Kutokana na historia hii, ni wazi basi wakazi wa asili wa eneo hili ni Wafoeiniki na baadaye Wapalestina. Hawa Wafilisti walitokea eneo la Levant au Shamu ambayo ni eneo ilipo hivi leo Syria, Lebanon, Jordan na Palestina yenyewe. Kwa hiyo lugha yao ilikuwa Kifilisti, moja ya matawi ya lugha ya Kiarabu.

Waisraeli walifikaje Palestina?

Tunapozungumza Waisraeli tunamaanisha wana wa Israeli. Na huyu Israeli ndiye huyo Yakub au Yakobo (Jacob) aliyetajwa katiak Taurati, Injili na Qur’an. Ama kuhusu Waisraeli walifikaje Palestina na kwa hiyo Yerusalemu, inabidi turudi nyuma hadi kwa nabii Ibrahimu (Amani iwe juu yake na mitume wote wa Allah).

Nabii Ibrahim ni Muebrania yaani uzao wa Eber. Huyu Eber alikuwa akiishi eneo la Mesopotamia (Iraq) na maana yake “mtu anayeishi kuvuka mto”. Waebrania ni katika kizazi cha Sam (Shem) mtoto wa nabii Nuhu ambaye kizazi chake kiliishi kati ya mito miwili ya Yufrati na Tigris.

Nabii Ibrahimu alipookoka kuchomwa moto na Mfalme Nimrod (Namrudha) kwa kukataa kuabudia miungu masanamu alikimbilia eneo la Palestina kama ilivyokuja katika Qur’an Suurat Mu’minuun aya ya 71:

“Na tukamuokoa yeye na Lutu kwenda kwenye ardhi ambayo tumeibariki kwa ajili ya Walimwengu”.

Ardhi iliyobarikiwa ni ardhi ya Yerusalem na pambizoni mwake kama ilivyokuja tena katiak Qur’an Suura ya 17 aya ya 1 Allah aliposema “ Ametukuka yule ambaye aliyempeleka mja wake (Mtume Muhammad) kutoka Msikiti Mtukufu (wa Makka) hadi Msikiti wa Mbali tuliobariki pambizoni mwake ili tumuoneshe miongoni mwa miujiza yetu hakika yeye ni Mwenye Kusikia na Mwenye Kuona kila kitu”.

Katika Qur’an ziko aya nyingi zinazotaja utakatifu wa mji wa Yerusalemu na nchi nzima ya Palestina na katika Biblia ziko takriban aya kumi na mbili pia zenye kutaja utakatifu wa ardhi hii ya Palestina. Kwa Mfano Kitabu cha Zakaria 2:12 pameandikwa

“The LORD will posses Judah as His portion in the holy land, and will again choose Jerusalem”.

Tafsiri isiyo rasmi ni kwamba

“Na Bwana Mungu atamfanya Yuda kama sehemu yake katika ardhi takatifu na ataiteua tena Yerusalemu”.

Na katika Ezekiel 48:14 pameandikwa

“Zaidi ya hayo au kutenga chaguo hili la hawatouza au kubadili sehemu yoyote ya ardhi teule kwani ni takatifu kwa Bwana Mungu”.

Kwa hiyo hapana ubishi kwamba kwa mujibu wa Uislamu, Ukristu na Uyahudi ardhi ya Yerusalemu na eneo lote pembeni yake ni ardhi takatifu kiasi cha Musa kuamriwa avue viatu vyake kuuenzi utakatifu wa ardhi hiyo.

Katika Qur’an Sura ya 20 aya ya 12 Allah anasema

“Hakika mimi ni Mola wake basi vua viatu vyako hakika wewe uko katika uwanda mtakatifu”. Na katika Matendo 7:33 pameandikwa “Lakini Bwana Mungu akamwambia ‘vua viatu vyako kutoka miguuni mwako kwa sababu sehemu uliyosimama juu yake ni ardhi takatifu”.

Baada ya kufika ardhi takatifu, Ibrahimu na mkewe walisafiri kwenda Misri na huko yakamkuta yaliyomkuta akalazimika kurudi Yerusalemu akiwa amepewa kijakazi Agar (Haajirah). Akiwa Yerusalem, wakati huo hakuna Waisraeli (Wayahudi), Ibrahimu akamzaa Ismaili (Ishmael) na kijakazi wake.

Nabii Ibrahimu akaamriwa na Allah asafiri na kijakazi huyo na mwanaye Ismaili kwenda Paran (Makka) na akamuacha huko kisha yeye akarejea Palestina ikawa anakuja kuwatembelea mara kwa mara kuwajulia hali. Baadaye Ibrahimu na mwanye wakaziinua kuta za Msikiti Mtakatifu wa Makka.

Ni katika kizazi cha Ismaili ndipo alipokuja kuzaliwa Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) nabii wa mwisho wa Mwenyezi Mungu kwa walimwengu, nabii ambaye kama ilivyosema Qur’an ametajwa katika Taurati, Injili na Zaburi.

Nabii ibrahimu akapate mtoto mwingine aitwaye Is-haka kwa mkewe Sarai (Sarah) na Is-haka akamzaa Yaqubu (Yakobo) ambaye ndiye aitwaye Israeli na kizazi chake ndicho kinachoitwa Wana wa Israili.

Hawa Wana wa Israili miongoni mwao walitokea mitume na manabii wengi sana kuliko ilivyotokea kwa kizazi chochote kile na hivyo kuwa taifa teule la Mwenyezi Mungu kama ilivyotajwa katika Qur’an na vitabu vya Allah vilivyoitangulia Qur’an.

Waisraeili wakawa wakazi wa mji wa Jerusalemu katika Palestina mpaka ilipofika zama za nabii Yaqubu mwanaye Yusuf ambaye pia ni nabii wa Allah alipokuwa waziri katika utawala wa Misri, wakahama kutoka Palestina kwenda Misri.

Baada ya kukaa utumwani Misri kwa karne kadhaa Mwenyezi Mungu akamuinua Musa na nduguye Haruna kama mitume wake kwa Wana wa Israeli na akawatendea mambo makubwa ikiwemo kuwakoa kutoka utumwani na kuwashindisha juu ya majeshi ya Wafilisti waliokuwa wakikaa katika mji wa Yerusalemu.

Allah anasema katika Qur’an, Suura ya 5 aya ya 21

“(Musa) akasema enyi watu wangu ingieni ardhi takatifu ambayo Allah amewapa na wala msikengeuke mkawa wenye kupata hasara”.

Wana wa Israeli wakakataa kuingia katika ardhi hiyo.

Agano la Kale Kumbukumbu la Taurati 1:26 limeelezea kukataa huku kwa Wana wa Israeli kwa maneno haya;

“Watu wale wana nguvu na ni warefu kuliko sisi na miji yao ni mikubwa na ina ngome madhubuti zilizoinuliwa juu”.

Hatimaye nabii Musa alifariki Wana wa Israeli wakitangatanga jangwani kwa miaka arobaini na hawakuingia Jerusalemu hadi Daudi akiwa kijana mdogo alipomuua Goliati (Goliath) na kulishinda jeshi la Wafilisti.

Kwa maelezo haya, tunaona kwamba Wana wa Israeli wanazalika katika mji wa Yerusalemu ambao nabii Ibrahimu aliahidiwa na Allah na nabii Musa aliamriwa tena waingie baada ya kutoka utumwani Misri.

Swali linabaki, je kwa maelezo haya ambapo Waisraeli katika ardhi ya Palestina na mji wa Yerusalemu ni ‘watu wa kuja’ chambilecho Waswahili na kwamba alipewa ardhi na Mwenyezi Mungu basi ardhi yote ya Palestina ni mali yao?

Kweli waliahidiwa na wakapewa ardhi takatifu ya Yerusalemu, sasa hili maana yake ni kwamba wao ndio wamiliki wa mji huo milele? Je umiliki huo haukuwa na masharti? Je waliyatimiza masharti hayo? Na kama hawakuyatimiza, je umiliki wao bado uko pale pale?

(Itaendelea In Shaa Allah…)

Tags
Show More

SHEIKH MUHAMMAD ISSA

Ni mtu mwenye wadhifa katika mashirika mbalimbali nchini Tanzania kwanzia ngazi ya elimu, Kiuchumi, vyombo vya habar na mashirika ya kislam.Ni katibu mkuu wa Islamic Foundation, katibu msaidizi wa chama cha BASUTA, mwenyekiti wa bodi ya uaminifu katika Muslim development board Shinyanga, mchambuzi wa siasa na jamii katika chombo cha BBC swahili, mtangazaji wa Tv, radio na mwandishi wa vitabu vingi vya dini hususan vya fedha za Uislam Tanzania. Ana Umri wa miaka 53 na watoto 13 Mashallah.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close