-

Mji wa Jerusalem ni Milki ya Nani? 2

Sehemu ya Pili
(Sehemu ya kwanza – Bonyeza Hapa) 

Utangulizi

Katika toleo lililopita tuliuliza swali la kujiuliza, ni kwa nini hali iwe hivi kwa mji wa Yerusalem? Ni nani mmiliki wa mji wa Yerusalemu? Umiliki wake anaupata kwa misingi gani? Kuwa wa kwanza kusihi pale, kupewa na Mwenyezi Mungu, kupewa na Umoja wa mataifa au kuwa mbabe kuwazidi wengine?

Tulielezea historia ya mji huo na hata asili ya jina la  Jerusalemu na watu gani walikuwa wenyeji wa asili ya hao na Waisraeli walifikaje Palestina. Tuliona pia kwamba inapotajwa Palestina Waisraeli ni ‘watu wa kuja’ kwani babu yao nabii Ibrahimu alihamia Palestina akitokea Mesopotamia (Iraq) ya leo.

Mbali na hayo tuliona pia kwamba Mwenyezi Mungu aliwaokoa Waisraeli kutoka utumwani Misri na kuwafanyia mambo makubwa. Kisha tukamalizia kwa kuuliza swali, je kwa maelezo haya ambapo Waisraeli katika ardhi ya Palestina na mji wa Yerusalemu ni ‘watu wa kuja’ chambilecho Waswahili na kwamba walipewa ardhi na Mwenyezi Mungu basi ardhi yote ya Palestina ni mali yao?

Madai ya Waisraeli kumiliki ardhi Palestina

Kwa kuwa tumeona kwamba Waisareli katika ardhi ya Palestina ni watu wa kuja na kwamba kulikuwa na wenyeweji wa asili wakiishi katika ardhi hiyo maelfu ya miaka kabla ya ujio wa Ibrahimu Muebrania kutoka Mesopotamia, je Waisraeli wanategemea nini?

Madai pekee ya Waisraeli kuhusu kumiliki ardhi ya Palestina na mji wa Yerusalemu ni kwamba wao walipewa ardhi hiyo takatifu na Mwenyezi Mungu kwa ahadi aliyomwahidi nabii Ibrahimu na pia aliyomwahidi nabii Musa alipowatoa Waisraeli utumwani Misri.

Je ni kweli Waisraeli waliahidiwa ardhi ya Palestina? Jibu ni ndiyo kwa mujibu wa vitabu vitakatifu Taurati, Injili, Zaburi na hata Qur’an.

Qur’an inasema ni kweli Waisraeli baada ya kutoka utumwani Misri waliahidiwa “nchi ya ahadi” ambayo ni ardhi takatifu. Katika Qur’an tunasoma

“(Nabii Musa akasema), enyi watu wangu ingieni ardhi takatifu ambayo Allah amekuandikieni na wala msikengeuke mkarudi nyuma mkajakuwa wenye kupata hasara. (Qur’an 5:20)

Katika kumbukumbu la Taurati 34:4 nako tunasoma maneno haya Mwenyezi Mungu akimwambia Musa,

Na Yehova akamwambia: “Hii ndiyo nchi ambayo nilimwapia Abrahamu, Isaka na Yakobo, na kusema, ‘Nitaupa uzao wako.’ Nimekufanya uione kwa macho yako mwenyewe, kwa maana wewe hutavuka kuingia huko.”

Kwa hiyo hakuna utata kwamba Wana wa Israeli wlaiahidiwa ardhi takatifu ambayo ndiyo hiyo Yerusalemu na maeneo ya pambizoni mwake siyo ardhi yote ya Palestina. Lakini ni kwa nini Waisraeli wakapewa na Allah ardhi ya watu wengine?

Ni kwa sababu ni wao ndio watu pekee zama hizo waliokuwa wakimjua Mungu wa kweli (Allah) na wakimwabudu katika ardhi hiyo ingwa mara nyingi walikuwa watu wakorofi na wasiomtii Allah ipasavyo.

Ndiyo wana wa Israeli waliahidiwa ardhi takatifu ya Yerusalemu, sasa ahadi hiyo maana yake wao ndio wamiliki wa nchi na mji huo milele? Je umiliki huo haukuwa na masharti? Je waliyatimiza masharti hayo? Na kama hawakuyatimiza, je umiliki wao bado uko pale pale?

Ni wazi kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ilikuwa na masharti. Maana yake ni kwamba umilki wa Waisraeli wa ardhi hiyo waliyoahidiwa ni wakati ule tu wakiwa wanatimiza masharti ya ahadi. Je ni masharti gani hayo walipewa na Mwenyezi Mungu?

Katika Kumbukumbu la Torati 26:16-19 tunasoma masharti waliyopewa Waisraeli ambayo pasina kuyatekeleza haya umiliki wa ardhi takatifu unakwisha na ardhi kupewa watu wengine kama alivyokuja kusema Masihi Isa mwana  wa Mariyamu (Yesu).

“Siku ya leo Yehova Mungu wako anakuamuru utekeleze masharti haya na sheria hizi. Ni lazima uzishike na kuzitekeleza kwa moyo wako wote na nafsi yako yote.  Leo Yehova amewatangazia kwamba atakuwa Mungu wenu mnapotembea katika njia zake na kushika masharti yake, amri zake, na sheria zake, na mnaposikiliza sauti yake.”

Na leo mmemtangazia Yehova kwamba mtakuwa watu wake, mali yake ya pekee, kama alivyowaahidi, na kwamba mtashika amri zake zote na kwamba atawakweza juu ya mataifa mengine yote ambayo ameyatokeza, akiwapa sifa na umaarufu na utukufu mnapothibitisha kwamba ninyi ni taifa takatifu kwa Yehova Mungu wenu, kama alivyoahidi.”

Na katika Qur’an tunakutaka na masharti haya katika Suratul Maidha aya ya 21 “Na kwa hakika Allah alichukua ahadi kutoka kwa Wana wa Israili na tukapeleka waangalizi kumi na wawili. Na Allah akasema, hakika mimi niko pamoja nanyi. Ikiwa mtasimamisha swala na kutoa zaka na mkawaamini mitume wangu na kuwatia nguvu na mtakapomkopesha Allah kukopesha kuzuri, nitakufutieni makosa yenu”.

Kwa hiyo hadi ya Mwenyezi Mungu kwa wana Wa Israili ilikuwa na masharti bila kuyatekeleza hayo hawana haki ya kudai umiliki wa ardhi takatifu. Historia imejaa katika vitabu vya MwenyeI Mungu jinsi Waisraeli walivyokaidi amri za Mungu na kutenda ufisadi katika ardhi.

Je maandiko yote haya hayathibitishi kuwa taifa la leo la israeli ndilo wamiliki wa ardhi takatifu ya palestina na mji wa yerusalemu? Jibu ni hapana, Kwa sababu watu wasiotekeleza ahadi ya Allah, wasiotenda utakatifu na wasiokuwa watiifu kama hawa hawawezi kuwa wamiliki wa ardhi takatifu.

Kuasi kwao amri za Allah na kuvunja ahadi ndiko kulikofanya Waisraeli wanyang’anwe ardhi waliyopewa na kutawanyika duniani kote hadi waliporudishwa Palestina mwaka kuanzia mwaka 1921 -1948 kwa njama za Waingereza kupitia Umoja wa Wazayuni duniani ukiongozwa na Weismann kisha Theodore Herzl, ni kuvunja kwao ahadi ya Mungu.

Biblia inarekodi nzuri katika 1 Wafalme 14:15

“Yehova atawapiga Waisraeli kama tete linaloyumba-yumba ndani ya maji, naye atawang’oa Waisraeli kutoka katika nchi hii nzuri aliyowapa mababu zao na kuwatawanya ng’ambo ya Mto Efrati, kwa sababu walimkasirisha Yehova kwa kutengeneza masanamu ya miti”.

Katika Matendo ya Mitume Masihi Mwana wa Mariyamu anasema kuhusu uasi wa Waisraeli “Enyi wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya na ninyi ni vivyo hivyo. Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumuudhi? Na waliwaua wale waliotabiri habari za kuja yule mwenye haki ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, ‘mkamuua’.

Tanbihi: Waislamu hawaamini kuuwawa kwa nabii Masihi Isa Mwana wa Mariyamu (Yesu) kama waaminivyo Wakristo.

Qur’an nayo ikaja na habari hizi hizi za uasi wa Waisraeli ikisema

“Na kwa hakika tulimpa Musa kitabu (Torati) na tukafuatiliza baada yake kwa manabii na tukampa Isa mwana wa Mariyamu hoja za wazi wazi na kumtia nguvu kwa Roho Mtakatifu (Malaika Jibrili). Basi kila mara alipowaijilia mtume kwa yale ambayo nafsi zenu hazikuyapenda mlifanya kiburi, basi wengine mliwakadhibisha na wengine mliwaua” (2:87).

Basi je, maandiko yote haya hayathibitishi kuwa taifa la leo la israeli ndilo wamiliki wa ardhi takatifu ya Palestina na mji wa Yerusalemu na siyo Wapalestina?Jibu ni hapana kwa sababu kama tulivyoona maandiko watu wasiotekeleza ahadi ya Allah, wasiotenda utakatifu na wasiokuwa watiifu kama hawa hawawezi kuwa wamiliki wa ardhi takatifu.

Yote mawili, utakatifu wa Waisraeli na ahadi ya ardhi takatifu ni mambo yaliyokuwa na masharti tuliyoyaona na kuvunjwa kwa masharti hayo kunawanyima Waisraeli haki ya kudai kuwa wao ndio wamiliki wa ardhi takatifu ya Yerusalemu na Palestina kwa ujumla.

Hivyo ndivyo Mungu alivyowaambia Waisraeli katika kitabu cha Kutoka 19:5

“Ninyi wenyewe mmeona niliyowatendea Wamisri, ili nipate kuwachukua ninyi juu ya mabawa ya tai na kuwaleta kwangu. Na sasa ikiwa mtaitii sauti yangu kabisa na kulishika kwa kweli agano langu, ndipo hakika mtakapokuwa mali yangu ya pekee kutoka kati ya vikundi vingine vyote vya watu, kwa sababu dunia nzima ni yangu”

Kwa maneo haya Waisraeli walipoteza agano la Mungu na taifa la Israeli la Kizayuni la hivi sasa lililokalia ardhi takatifu liko pale kwa ujabari tu na kuungwa mkono na mataifa yenye nguvu. Hawana haki yoyote juu ya Yerusalemu kwani waliipoteza siku nyingi tangu walipowakataa manabii akiwemo Masihi Isa mwana wa Mariyamu.

(Itaendelea In Shaa Allah…)

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close