-

Mipaka ya kuchukiana baina ya Waislamu

Kupendana na kuchukiana kwa ajili ya Allah [Al-walaa wal-baraa]

Mpenzi msomaji, mlango wa kupendana na kuchukiana kwa ajili ya Allah (Al-walaa Wal-baraa) haujaishia kwa Waislamu na makafiri tu bali uko baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe. Ikiwa Muislamu ndani yake ana imani na maasia, basi atapendwa kutokana na imani yake na kuchukiwa kutokana na maasia yake. Hii iko hata katika maisha halisi, mtu anaweza kukerwa na ladha chungu ya dawa, lakini wakati huohuo akaipenda dawa hiyo kwa kuwa ndani yake kuna ponyo au shifaa ya ugonjwa wake.

Sheikh Muhammad Saleh Al-Uthaimeen amesema baadhi ya Waislamu, kwa kutokujua, wanamchukia Muislamu mwenye kufanya maasia kuliko wanavyomchukia kafiri; nalo ni jambo la ajabu linalogeuza uhakika wa mambo. Kafiri ni adui wa Allah, Mtume na adui wa Waislamu. Allah Mwenyewe kaelekeza kafiri achukiwe wala asipendwe. Allah anasema: “Enyi mlioamini! Msifanye adui wangu na adui wenu kuwa marafiki wa ndani mkiwapa mapenzi, na hali wamekwishakufuru yaliyokujieni ya haki. Wanamfukuza Mtume pamoja nanyi kwa sababu mmemuamini Allah Mola wenu. Mnapotoka kwa ajili ya jihad katika njia yangu na kutafuta radhi zangu mnawapa siri kwa mapenzi, na hali Mimi najua zaidi yale mnayoyaficha na yale mnayoyadhihirisha. Na yeyote atakayefanya hivyo miongoni mwenu, basi kwa yakini amepotea njia ya sawa.” (Qur’an 60: 1).

Hebu angalia Allah anavyosema ndani ya Qur’an juu ya mtu aliyemfanyia ndugu yake dhambi kubwa ya kuua: “. . . na anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa ihsani. Hiyo ni tahafifu kutoka kwa Mola wenu na rahma. Na atakayevuka mipaka baada ya hapo basi atapata adhabu iumizayo.” (Qur’an, 2:178).

Huyu ni mtu mwenye imani aliyemuua Muumini kimakosa. Allah kamjaalia kuwa ni ndugu wa aliyeuliwa, pamoja na kuwa kumuua Muumini kwa bahati mbaya ni katika dhambi kubwa sana. Vilevile, Allah akasema: “Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu, na timizeni haki haki. Hakika Allah anapenda wanaotimiza haki.” (Qur’an, 49: 9).

Allah hakuyatoa makundi mawili ya Waislamu yenye kupigana katika imani wala undugu wa kiimani. Bado yangalimo kwenye Imani na undugu. Ikiwa kumhama mtu kuna maslahi au kuna kuondosha mafsada (mfano kemeo kwa muasi katika maasia yake); basi hapo, kumhama kunakuwa ni jambo sio tu linalofaa bali linalotakikana na kupendekezwa pia kisheria. Na katika hili, mtu apime ukubwa wa maasia ambayo yanasababisha kumhama mtu.

 

Na wala usikodolee macho yako kwa yale tuliyowastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao. Hayo ni mapambo ya uhai wa dunia tu, ili tuwajaribu kwayo. Na riziki ya Mola wako ni bora zaidi na ni yenye kudumu zaidi.” [Qur’an, 20:131]

Mfano wa hili ni kisa mashuhuri cha Swahaba

Ka’abu bin Maalik na jamaa zake wawili ambao walibaki wasiende vitani. Mtume aliamrisha wahamwe na akakataza wasisemeshwe, na hivyo watu wakawatenga hadi ilifikia aliingia kwake mtoto wa ami yake Abuu Qatadah (Allah amridhie). Huyu alikuwa mtu aliyempenda Ka’abu bin Maalik sana lakini alimsalimia na wala wala hakumuitikia. Hivyo, kuwahama watu hawa watatu kulikuwa na maslahi mapana zaidi ya kuwafanya warejee kwa Allah na kutubia toba ya kweli.

Huu ulikuwa ni mtihani mkubwa kwao kwani maslahi ya kuwahama yalikuwa na faida zaidi kuliko wasingesusiwa. Ama siku hizi, kuwasusia na kuwahama watu wanaofanya maasia sio tu hakuwazidishii ila ukorofi bali pia kunawaongezea kasi ya maasia yao na kuwafanya wawakimbie zaidi Waumini na wanazuoni. Hii maana yake ni kuwa, kuwahama na kuwasusisa hakuna faida.

Inaweza kusemwa, kumhama mtu na kumsusia ni dawa inayotumika panapokuwa na uwezekano wa kuwa tiba. Ama panapokuwa hakuna uwezekano wa kuwa tiba au ikionekana kuwa itazidishwa maradhi na hivyo kumuangamiza mgonjwa, hakuna sababu ya kumhama na kumsusia. Hali za kumhama mtu kwa ujumla wake ni tatu. Kukiwa na uhakika kuwa maslahi yapo katika kumsusia au kumhama mtu huyu, hapo kumhama linakuwa ni jambo linalotakikana.

Pili, ikiwa ni kinyume chake, yaani kumhama na kumsusia kuna mafsada na madhara zaidi kuliko kutokumhama na kumsusia, hapo inakatazwa kumhama au kumsusia mtu. Hali ya tatu, ikiwa ni pale inapokuwa haifahamiki yako wapi maslahi zaidi kati ya kumhama na kumsusia mtu au la. Kilicho bora ni kutokumhama kutokana na kauli ya Mtume kuwa, haifai kwa Muislamu kumhama ndugu yake Muislamu zaidi ya siku tatu. ..

Itaendelea…

Tags
Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close