-

MAISHA YA MASWAHABA: Salmaan al-Faarisy, Maisha yake baada ya kusilimu

Kutokana na maelezo yaliyotangulia tunajifunza kwamba Salmaan alisilimu mwaka wa kwanza Hijriya mara tu baada ya Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] kuwasili Madina. Kuanzia hapo aliishi na Mtume na inasemekana alikuwa muachwa huru wake, kwa maana Mtume alimlipia gharama za kumkomboa. Na pia Salmaan anatajwa kuwa ni katika watu aliyowapa hadhi yakuwa mtu wa nyumbani mwake [Ahlu bayti]. Mtume alimpenda sana Salmaan.

Salmaan hakuhudhuria vita vya Badri na Uhud kwa sababu ya kuwa mtumwa lakini alihudhuria vita vya Khandaq na alitoa mchango mkubwa katika kuwahami Waislamu na adui wao. Na baada ya hapo alihudhuria vita mbali mbali pamoja na Mtume ikiwemo mkataba wa Hudaibiya na Fat-hu Makka.

Nafasi yake kielimu

Shauku ya Salmaan ya kujifunza masuala ya kidini haikuishia kwa wanazuoni wakati wa safari yake ya kuisaka dini ya haki mwanzoni, bali aliendelea kuwa mtafiti mahiri wa mambo ya sheria za Uislamu na misingi yake mbele ya Mtume huku akioanisha na uelewa alioupata safarini mwake.

Salmaan alijibidiisha mpaka akawa mmoja wa waliopokea hadithi nyingi kutoka kwa Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] na kuzisimulia kwa wengine. Pia, alikuwa ni miongoni mwa waliopata ufahamu wa kina juu ya Uislamu. Zaidi ya hayo, Salmaan alizingatiwa kuwa, ni mmoja wa watoa fatwa katika masuala mengi na walisoma kwake wengi miongoni mwa Maswahaba wenzake akiwemo Anas bin Malik Ibn Abbas na wengineo.

Pia walisoma kwake katika Matabii kama vile Ilkima bin Qais Annakhaii na Abdullah bin Wadia. Kwa hiyo Salmaan alikuwa ni chem chem ya maarifa watu wakiteka hapo hususan baada ya Mtume kuondoka.

Salmaan na Abu Dardaa

Katika kujenga umoja wa Waislamu kama msingi muhimu wa kusimamisha serikali ya Kiislamu, Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] alipanga udugu baina ya Muhajirina na Answar. Kila muhajiri alimuunganisha na Answar awe mwenyeji wake na waishi kama ndugu. Licha ya kuja riwaya nyingi zilizo tofauti katika kubainisha nani alikuwa ndugu wa Salmaan [mwenda nyuma ya haki] katika Maanswar, lakini mashuhuri zaidi ni kwamba mwenyeji wake alikuwa Abuu Dardaa [Allah awaridhie] ambaye alisifikana sana kwa wingi wa ibada na zuhdi [kuipa mgongo dunia].

Muongozo wa Salmaan nyumbani kwa Abu Dardaa

Siku moja Salmaan alitembelea nyumbani kwa rafiki yake wakati hayupo, Salmaan alimkuta Mama Dardaa akiwa mchakavu. Kwa maana nyengine hakuwa na ishara ya kuwa kama mke wa mtu. Alimuuliza: “Una nini?” Akamjibu: “Ndugu yako Abuu Dardaa hana haja nasi, [yeye na ibada zake tu].”

Abuu Dardaa aliporudi alimtaarishia mgeni wake chakula na kumwambia: “Tafadhali kula, mimi nimefunga.” Akasema: “Hapana, sili mpaka tule pamoja.” Ulipofika usiku baada ya swala ya Isha, Abuu Dardaa alisimama kutaka kuswali [swala za usiku]. Salmaan akamwambia: “Nenda kalale kwanza.” Akaenda kulala.

Mara akainuka tena. Salmaan akamwambia tena: “Nenda ukalale.” Mpaka ilipobaki thuluthi ya mwisho ya usiku Salmaan alimuamsha mwenyeji wake wakaenda kuswali na kumwambia: “Hakika Mola wako ana haki juu yako, na mwili wako una haki juu yako, na mke wako ana haki juu yako, basi mpe kila mwenye haki haki yake.” Asubuhi alikwenda kwa Mtume na kumuelezea mkasa huu mzima:

Mtume (saw) akamwambia: “Salmaan amesema kweli.”

Kisa hiki Imamu Bukhari amekirejea rejea kwenye milango kadhaa katika kitabu chake. Kwa mfano, katika kitabu ‘Swaumu’ hadithi ya 1968, kitabu ‘al-Ayman’ hadithi ya 4830. Pia kimeandikwa na Imamu Muslim kitabu ‘swaumu’ hadithi ya 1159, na Imam Attirmidhy ‘Baabuz Zuhd’ hadithi ya 2413. Kisa hiki kinaonesha upeo wa fiqhi ya Salmaan [Allah amridhie] katika kuizingatia mipaka ya utendaji ibada pamoja na kuchunga haki za wengine.

Salmaan Alfarisy katika vita
vya Khandaq

Moja ya mambo yaliyompatia umaarufu mkubwa Swahaba Salmaan [Allah amridhie] ni rai yake kwa Mtume juu ya kuchimba handaki kama kinga ya Waislamu dhidi ya makafiri waliotaka kuivamia Madina.

Mnamo mwaka wa tano tangu Mtume kuhamia Madina, Waislamu walipata taarifa kwamba Makuraish wakishirikiana na Waarabu wengine, akina Banii Ghatwafan, wamepanga kuwashambulia wakiwa ndani ya mji wao.

Mtume alishauriana na Maswahaba nini la kufanya. Kwa kweli Waislamu walikuwa katika kipindi kigumu sana hususan ikizingatiwa kwamba vita hivyo vilikuwa na mchango mkubwa wa Banii Quraidha, moja ya makundi ya kiyahudi, ambao hapo awali walifunga mkataba wa amani na Waislamu lakini wakauvunja. Kwa hiyo nyoyo za Waislamu zilijaa wasiwasi.

Katika muktadha huo, ndipo Salmaan akamshauri Mtume wachimbe handaki. Sheikh Munir Muhammad Alghadhbaan amesema: “Basi Salmaan akishauri lichimbwe handaki, liizunguke Madina sehemu zisizo na milima. Salmaan
alisema:,

Ewe Mtume wa Allah, sisi [kwetu kule] Furs tukiogopa maadui [kutuvamia] tunachimba mahandaki.”

Mtume aliafiki rai hii na Waislamu wakaipenda. Mtume akaamuru handaki lichimbwe na kuwataka Waislamu wawe wavumilivu, wajitahidi na ya kwamba wakivumilia na kumcha Allah watapata ushindi. Mtume pia aliwasisitiza kuwa watiifu wakati wote wa vita.

Mbinu hii ya kivita haikuwa ikifahamika kwa Warabu, Salmaan ndiye wa kwanza kuja nayo. [Taz: ‘Fiqhu sirauk’ uk314] Dalili ya hayo ni kwamba hata maadui walipofika na kuliona shimo na kina chake walishangaa sana na hawakuweza kuliruka na kupita upande wa pili, ila wachache tu, hali iliyowaacha nje masiku kadhaa. Kwa kweli Salmaan alikuja na fikra iliyowatatulia Waislamu sehemu kubwa ya tatizo lao lile.

Kifo chake

Katika ukhalifa wa Umar, Salmaan alichaguliwa kuwa gavana huko Madaain [Iraq] na Inaaminika kuwa alikufa katika ukhalifa wa Uthmaan [Allah amridhie] mnamo mwaka wa 33 Hijriya. Allah Aliyetukuka ammiminie radhi zake Salmaan.

 

MAISHA YA MASWAHABA: Salmaan al-Faarisy (Allah amridhie)

MAISHA YA MASWAHABA: Salmaan al-Faarisy (as) -2

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close