-

Kwanini baadhi ya dua hazijibiwi?

Moja ya mambo yanayowashangaza kama siyo kuwatatanisha watu wengi, ni suala la kukubaliwa dua tunazomuomba Allah. Watu wanahoji ni kwa nini Allah anasema: “Niombeni nitakuitikieni.” (Qur’an, 40:60), lakini hawajibiwi maombi yao.

Watu wanaulizana: “Allah ametuahidi kukubali maombi yetu, sasa mbona hilo hatulishuhudii? Hivi ni kwanini tunamuomba sana Mwenyezi Mungu lakini tunaambulia patupu?”

Pamoja na kusoma kwa bidii, wanafunzi humuomba sana Mwenyezi Mungu ili awawezeshe kufaulu vizuri mitihani yao. Hata hivyo, wapo baadhi ya watu wanaodhani kwamba si lazima mtu akubaliwe dua/ maombi ya kile alichokiumba kwani kufanya maombi ni katika mila na desturi za mababu na si jambo linalohusiana na ibada. Katika kutetea hoja yao, watu hao wanasema iweje mtoto aliyedhulumiwa anajipinda kuomba dua ndani ya mwezi wa Ramadhan, ambao mfungaji akiomba dua hujibiwa pasina kipingamizi, lakini Allah Ta’ala hajibu dua yake huku madhalimu wakiendelea kuishi maisha ‘mazuri’ yasiyo na kero.

Wakati mwingine mtu anaweza kujitumbukiza kwenye shari kwa kuomba jambo zuri akidhani kuwa lina kheri kwake

Mtoto anaweza kujiuliza ni kwanini nimeomba dua mara nyingi lakini sijibiwi Hapo ndipo anapoanza kujenga dhana ndani ya nafsi yake kwamba mtu anapomuelekea Allah kwa maombi si lazima kujibiwa, hivyo anaanza kupunguza morali ya kumtegemea Allah.

Sharti ya kukubaliwa dua
Jambo la kumfahamisha mtoto wako na watu wengine wenye fikra kama hizo ni kwamba, baadhi ya dua ambazo waja huziomba hukosa majibu kwa sababu maalumu. Sanjari na hivyo, pia unatakiwa umjuze mwanao sharti za kukubaliwa dua kama zilivyoainishwa na wanazuoni. Kadhalika, mfahamishe mwanao Hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) inayosema: “Enyi watu! Hakika Allah ni mwema, hakubali ila kilichokuwa chema.” Pia, mwanao ajue kuwa, Allah amewaamuru Waumini kama alivyowaamuru Mitume, akasema: “Enyi mlioamini! Kuleni vizuri tulivyokuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.” [Qur’an, 2:172].

Kisha, Mtume akataja kisa cha msafiri aliyepigwa na vumbi akawa ni mwenye kuinua mikono yake juu lakini chakula, kinywaji, mavazi – vyote ni vya haramu. Basi, ikahojiwa, ni kwa namna gani atajibiwa dua yake huyu? Ni vigumu mno dua ya mtu huyu kujibiwa.

Tuachane na mtu huyu anayeishi kwa kutegemea chumo la haramu kwani tumeshajua sababu ya yeye kuchukiwa na kutokukubaliwa maombi yake. Swali la msingi ni: Je, kwanini baadhi ya dua (maombi) ya watu wema wenye kushikamana na sharia za Allah hazijibiwi? Katika ufafanuzi wake juu ya suala hili, Imam Ibnu al–Jawziy (Allah amrehemu) amesema: “Jua kuwa Allah ‘Azza Wajllah’ hakatai maombi ya Waumini bali wakati mwingine huchelewesha maombi yao kwa kuzingatia maslahi yao. Na hutokea mtu akaomba kitu au jambo lisilokuwa na maslahi wala tija kwake, hivyo Allah humpa mbadala wa kile alichokiomba. Allah anasema, ‘Sema, Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye katika waja wake.’” [Qur’an, 34:39].

Lakini pia huenda mja akacheleweshewa maombi ya kile alichokiumba hadi Siku ya Kiyama. Hivyo basi, Muumini anatakiwa asiache kumuomba Allah kwa sababu ya kutokukubaliwa dua yake. Muislamu afahamu kuwa, hakuna bahati mbaya katika dua ambayo anamuomba Allah. Allah amethibitisha hilo pale alipomzungumzia Nabii wake Zakariya: “Akasema, ‘Mola wangu Mlezi! Mifupa yangu imedhoofika, na kichwa kinameremeta kwa mvi; wala, Mola wangu Mlezi, sikuwa mwenye bahati mbaya kwa kukuomba Wewe.” (Qur’an, 19:4).

Hii ina maana, dua ni sehemu ya ibada, hivyo Muislamu anapomuelekea Mola wake kwa maombi hapaswi kukata tamaa juu ya matokeo ya kile anachokiomba kwani Allah amejaalia kila kitu na wakati wake, wala haupitikii, na kipimo hakivuki. Na hakika si vinginevyo, Allah hukubali dua za waja wema.

Ogopa dua ya aliyedhulumiwa
Imam Bukhari amenukuu maneno ya Umar bin Khattwab aliyomuambia mmoja wa watawala (magavana) wake, akasema: “Ogopa dua ya mtu aliyedhulumiwa, hakika dua yake hukubaliwa.” [Bukhari na Muslim]. Katika kufafanua Hadithi hii, mwanazuoni Ahmad bin Ismail amesema: “Wakati mwingine mtu hujiuliza, ‘Ni watu wangapi wanauawa bila sababu wala hatia huku muuaji akiendelea kuishi bila ya usumbufu, bughudha wala kero licha ya kuombewa mabaya kila siku?’”

Jibu la swali hili lipo katika Hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) inayosema: “Hakuna mtu aombaye dua ila hukubaliwa dua yake – aidha ataharakishiwa maombi yake hapa duniani au atawekewa akiba ya maombi yake huko Akhera, au atafutiwa dhambi zake kwa kiasi cha dua aliyoiomba kwa sharti mbili; maombi yenyewe yasiwe ni katika mambo ya madhambi au kuvunja undugu au yasiwe ya kuharakisha ajibiwe maombi yake.”

Maswahaba wakauliza: “Ewe Mjumbe wa Allah ni namna gani mtu anaharakisha kujibiwa maombi?” Akasema: “Ni muombaji kusema, ‘Nimemuomba Mola wangu lakini sijakubaliwa.’” (Tirmidhiy, na Sheikh Al–bani amesema ni Hadithi sahihi).

Tunafahamu kwamba kuhifadhiwa akiba ya maombi Siku ya Kiyama ni jambo zuri, wakati tunajua kuwa kupona maradhi, kufutiwa madhambi na kuepushiwa madhara kwa wanyonge ni mambo matatu makubwa ambayo ni muhimu kwa mwanadamu? Kama ni hivyo, kwa nini Allah anawakosesha baadhi ya watu kheri za duniani?

Jawabu la swali hili ni kama ifutavyo. Kupona maradhi kunaweza kuwa ni kheri kwa mtu kuliko jambo lile alilokusudia kulipata. Zaidi ni kwamba, Allah humpa mja kitu chema atakacho kwa kuzingatia maslahi na tija ya kitu hicho. Na yeyote atakayeruzukiwa jambo jema na Allah basi anakuwa amepewa kheri nyingi kwa vile atayaendesha vyema mambo ya Dunia na Akhera.

Imam Bukhari na Muslim wamenukuu Hadithi kutoka kwa Ataa bin Abuu Rabah (Allah amridhie), ambaye amesema: “Siku moja nilikuwa na Ibnu Abbas akaniambia, ‘Nikuoneshe mwanamke miongoni mwa wanawake wa peponi?’ Atwaa akamjibu, ‘Ndiyo nionyeshe.’ Akasema, ‘Ni huyu mwanamke mweusi, ambaye alimjia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akamuambia, ‘Mimi nina maradhi ya kifafa na kila kinaponishika nguo zangu hukaribia kuvuka, basi niombee kwa Allah (nipone).’ Mtume akamuambia, ‘Kama ukipenda, unaweza kuvumilia maradhi yako na utaingia peponi, na kama ukitaka nitamuomba Allah Aliyetukuka atakuponya.’ Yule mwanamke akasema, ‘Nitavumilia maradhi yangu.’ Kisha akamuambia Mtume, ‘Lakini huwa nakashifika (nakaa uchi), basi niombee kwa Allah nisikashifike.’”

Katika Hadithi hii tumeona jinsi mwanamke yule akifanya uamuzi wa busara kwa kuridhia kuishi na maradhi ya kifafa ili Siku ya Kiyama apate fursa ya kuingia peponi. Na kama tulivyosema, hakuna tatizo katika upokewaji wa dua kwani Allah ametutaka tumuombe na akaahidi kuwa atatuitikia dua zetu – aidha ataturuzuku kheri za hapa duniani au kesho Akhera.

Wakati mwingine mtu anaweza kujitumbukiza kwenye shari kwa kuomba jambo zuri akidhani kuwa lina kheri kwake kama anavyosema Allah Aliyetukuka : “Na mwanadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanadamu ni mwenye pupa.” [Qur’an, 17:11].

Tunasoma katika Hadithi kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimuomba Allah mambo matatu, akakubaliwa mawili na kukataliwa moja. Mtume aliomba umma wake usiangamie kwa ukame akakubaliwa, akaomba umma wake usiangamizwe kwa gharika (tufani) akakubaliwa, lakini alipoomba umma wake uhifadhiwe na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe alikataliwa. Hii ni dalili kuwa Allah ‘Azza Wajllah’ hakatai maombi ya waja

Show More

Related Articles

Back to top button
Close