-

Kuthamini marafiki wa mzazi baada ya kufa kwake

Abdullah bin Diynaar (Allah amridhie) amesimulia kuwa Abdullahi bin Umar (Allah amridhie) alikutana na bedui katika njia ya kuelekea Makka. Abdullah bin Umar alimsalimia (bedui huyo) kisha akampandisha kwenye punda wake na kumzawadia kilemba alichokuwa amekivaa.

Watu wakasema kumwambia Abdullah bin Umar : “Allah akufanye mwema. Hao ni mabedui wanaoridhika na mepesi.” Abdillahi bin Umar akasema: “Baba yake (bedui huyu) alikuwa rafiki mkubwa wa Umar bin Khattwab. Nimemsikia Mjumbe wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema: “Hakika wema mkubwa kabisa ni mtu kuunga undugu na vipenzi wa baba yake.” [Muslim].

Katika riwaya nyingine ya Ibn Diynaar amesimulia kuwa Abdillahi alipokuwa akichoka kupanda ngamia wakati akielekea Makka alikuwa anapumzika, kisha (huinua kichwa chake juu) na kukikaza kwa kilemba.

Wakati mmoja Abdillahi alipokuwa juu ya punda wake, alipita bedui mmoja akamuuliza: “Je, wewe ni mtoto wa fulani?” Akajibu: “Ndiyo.” Abdillahi bin Umar akamzawadia bedui huyo punda, kisha akamwambia: “Mpande (punda) huyu.” Pia alimzawadia kilemba na kumwambia: “Kifunge kichwani mwako.”

Baadhi ya marafiki zake wakasema: “Allah akusamehe (Ewe Abdillahi). Umempa bedui huyu punda uliyekuwa ukimtumia kwa safari zako na kilemba ulichokuwa ukifunikia kichwa chako!?”

Abdillahi bin Umar akasema: “Hakika nimemsikia Mjumbe wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema, ‘Wema mkubwa kabisa ni mtu kuunga undugu na vipenzi wa baba yake baada ya kufa baba yake.’” [Muslim].

Mafunzo ya tukio

Tukio hili limefungamana na amri ya kuwafanyia wema marafiki wa wazazi (baba na mama). Jambo hili, kisharia linazingatiwa kuwa ni sehemu ya kuwafanyia wema wazazi wawili, kama ilivyoelezwa katika hadith ya Abu Usayd Malik bin Rabi’ a (Allah amridhie).

Swahaba huyo amehadithia kuwa walipokuwa wamekaa na Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani imshukie) alikuja mtu kutoka ukoo wa Salima, akasema:

“Ewe Mtume wa Allah! Je, kumebakia wema wa kuwatendea wazazi wangu baada ya kufa kwao?” Mtume akasema: “Ndiyo! (Unatakiwa) uwaombee dua, uwatakie msamaha, utekeleze ahadi zao baada ya kufa kwao, uunge kizazi ambacho hakiungiki ila kwa sababu yao na kuwakirimu marafiki zao.” [Abu Daud].

Ni wajibu wetu kuwaombea dua wazazi wakati wa uhai wao na baada ya kufa. Ajabu ni kwamba, Waislamu wengi wamekuwa wakitumia gharama kubwa kununua chakula kwa ajili ya wageni wanaowaalika kuhudhuria shughuli za dua.

Kufanya hivyo ni kupotosha wajibu huu ambao kimsingi unapaswa kutekelezwa na watoto wa marehemu mara kwa mara. Kualika watu kwa lengo la kumsomea Qur’an maiti ni mojawapo ya masuala sugu yaliyoota mizizi ndani ya jamii zetu.

Jambo hili linakinzana na mafundisho ya Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) aliyesema:

“Atakapokufa mwanadamu matendo yake yote hukatika ila kwa mambo matatu: Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye kunufaisha au mtoto mwema atakayemuombea dua (mzazi wake).” [Muslim].

Kwa hivyo, tunapaswa kuwaombea dua wazazi wetu mara kwa mara, na si kusubiri msimu fulani au mwisho wa mwaka ndiyo tuwaombee dua. Waislamu tunatakiwa kuiacha ibada ya kuwaombea dua wazazi katika uhalisia wake. Hili ni jambo lililo ndani ya uwezo wa kila mtu anayejibidiisha na ibada.

Hata hivyo, wapo baadhi yetu ambao aidha kwa uzembe, dharau au kutofahamu umuhimu wa kuwaombea dua wazazi, wamekuwa wakipuuza ibada hii.

Kutekeleza usia wa wazazi

Ni wajibu kwa watoto kutekeleza usia na ahadi walizoziweka wazazi wao. Endapo wosia utakuwa na kipengele chenye madhara kwa baadhi ya watu ama jambo lililoharamishwa na dini, ni lazima ubadilishwe kwani sharia imekatazwa kutekeleza wosia wa namna hii. Ukamilifu wa wema ni kusahihisha jambo lolote la kisharia ambalo wazazi walilikosea.

Kuwakirimu marafiki wa wazazi

Miongoni mwa mambo muhimu ambayo mtoto anapaswa kumfanyia mzazi wake ni kuwatendea wema na ukarimu ndugu na marafiki wa wazazi wake. Katika hali na mazingira yoyote yale, watoto hawapaswi kuvunja uhusiano na marafiki wa wazazi wao, bali wanatakiwa waamiliane nao kwa wema na kuepuka kuwavunjia heshima na kuwatolea maneno makali. Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya familia hukumbwa na migogoro mikubwa pindi mtu anapofariki. Matokeo yake watu wanachukiana na kufanyiana uadui wao kwa wao kwa sababu ya mali. Aghalabu mtu anapofariki, ndugu hujikuta katika migogoro ya kugombania mali, jambo ambalo hupelekea mpasuko kati ya watoto wa marehemu na ndugu wengine.

Mtume ni kiigizo chema

Mama Aisha (Allah amridhie) amesema: “Sijamuonea wivu yeyote miongoni mwa wake wa Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) kama nilivyomuonea wivu Khadija (Allah amridhie) ilhali sijawahi kumuona. Lakini Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) alikuwa akimtaja sana Khadija, na mara nyingine alikuwa akichinja mbuzi, akimkata vipande na kuwapelekea marafiki wa Khadija. Mara nyingine nilimwambia: “Kana kwamba hakuna (mwanamke) duniani ila Khadija.”

 Akaniambia: “(Khadija) alikuwa kadha wa kadha, amenizalia watoto.” [Bukhari na Muslim]. Funzo mojawapo tunalolipata kutokana na hadith hii ni kuwa katika utamaduni wa Kiislamu ndugu na marafiki wa wazazi wana hadhi na nafasi kubwa, hivyo ni wajibu wetu kuwajali, kuwathamini na kuwatendea wema.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close