-

Kishk: Mashindano ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee, In shaa Allah

Siku mbili kabla ya kufanyika kwa mashindano ya kuhifadhi Qur’an ya Afrika yanayoandaliwa na taasisi ya Al-Hikma Foundation, Mwenyekiti wa mashindano hayo, Sheikh Nurdin Kishk amesema yatakuwa ni ya kipekee kwani kuna makundi mapya ya washindi na zawadi vimeongezwa.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili, kuelekea mashindano hayo yatakayofanyika Jumapili ya Mei 19 katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam, Sheikh Kishk alisema, mshindi wa kwanza wa msimu huu atapatiwa shilingi milioni 20 na safari ya Hijja.

Aidha, Sheikh Kishk alisema, endapo mshindi wa kwanza atakuwa ni.Mtanzania, pia atapatiwa kiwanja katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Endapo mshindi wa kwanza atakuwa ni Mtanzania atapatiwa zawadi ya kiwanja katika eneo la Kigomboni aanze maisha. Hii ni kwa sababu sharia za nchi haziruhusu mshindi ambaye ni raia wa nje kumiliki ardhi,” alisema Sheikh Kishki.

Walimu nao kuzawadiwa

Pia Sheikh Kishk alisema, kwa mara ya kwanza katika msimu huu walimu wa washindi watatu wa juzuu 20, kila mmoja atazawadiwa kiwanja katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kwa upande wa mshindi wa kwanza wa juzuu 20, yeye atapatiwa zawadi ya kwenda Umrah nchini Saudi Arabia.

Zawadi kwa watakaohudhuria
Aidha, Sheikh Kishk alisema kuwa, mwaka huu kutakuwa na zawadi ya kwenda Umrah nchini Saudi Arabia kwa watu wanne watakaohudhuria uwanjani na kujibu maswali yatakayoulizwa kwa usahihi.

Kishk alisema washindi hao wanne watapatikana kutoka majukwaa manne yaliyomo ndani ya uwanja huo wa Taifa kwa kila jukwaa kutoa mshindi mmoja.

Rais Magufuli mgeni rasmi
Kuhusu mgeni rasmi, Sheikh Kishk alisema, anatarajiwa kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ambaye tayari ameshathibitisha kuhudhuria.

Sheikh Kishk alitaja wageni wengine wanaotarajiwa kuhudhuria kuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa Kasim Majaliwa, Mawaziri, wabunge na viongozi wengine wa Serikali.

Wageni wengine ni pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili ambaye pia ndiyo mlezi wa Al-Hikma Foundation, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete.

Ugeni kutoka nje
Kwa upande wa nje ya nchi, Sheikh Kishk alisema anatarajia kuwa Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Saudi Arabia, Dkt. Swaleh Abdul-aziz Al Shaikh atahudhuria. Dkt Swaleh ndiye aliyekuwa mgeni rasmi mwaka jana katika mashindano ya 19 ya Alhikma Foundation akimuwakilisha Imamu Mkuu wa Misikiti Mitukufu Miwili ya Makka na Madina, Sheikh Abdul Rahman Sudais.

Katika moja ya ahadi zake mwaka jana, Dkt. Al Shaik aliahidi ujenzi wa chuo kikuu cha Kiislamu hapa nchini, jambo ambalo Sheikh Kishk amesema anatumai mgeni huyo atalitolea ufafanuzi siku hiyo ya Jumapili.

Katika mashindano hayo, jumla ya washiriki 20 kutoka nchi mbalimbali
barani Afrika watashindana ambapo kwa upande wa Tanzania kutakuwa na washindi watatu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close