-

Kikao cha TIF Volunteers chafana

Wajipanga kongamano la Misk ya Roho 2018

Jumapili iliyopita ya tarehe 12 mwezi wa nane ilikuwa ni ya kipekee kwa volunteers wa taasisi ya The Islamic Foundation baada ya kufanya kikao cha kwanza cha kimkakati kuelekea kongamano la pili la Afrika Mashariki lijulikano kama Misk ya Roho 2018.

Kikao hicho kilichowakutanisha pamoja volunteers wa zamani na wapya wa TIF kilifanyika katika mgahawa wa Delhi Darbar, Upanga jijini Dar Es Salaam kilipendezeshwa na uwepo wa mkurugenzi wa matukio wa taasisi ya The Islamic Foundation Tajmohamed Abbas.

Lengo kuu la kikao hicho ilikuwa ni kupeana taarifa kuhusu ujio wa kongamano la pili la Afrika Mashariki (Misk ya Roho 2018), lakini sambamba na hilo pia kukumbushana nafasi na wajibu wa Volunteers katika dini yetu ya kiislam kwa mujibu wa Quran na Sunnah.

Miongoni mwa faida zilizopatikana katika kikao hicho ni kukutana, kufahamiana, kujenga urafiki na udugu kwa volunteers wa zamani wa taasisi na volunteers wapya ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo walikuja kuonesha nia ya kujitolea kwa mara ya kwanza katika taasisi hii.

Akizungumza katika kikao hicho mkurugenzi wa matukio wa TIF Tajmohamed alisema “Kupata mwitikio mkubwa kiasi hiki hasa wengi wenu mkiwa vijana na ile hali ya kuonesha moyo wa kujitolea katika taasisi yetu na dini kwa ujumla ni matumaini makubwa kwetu kuwa tunayoyafanya yanaonekana na yanakubalika na jamii.” Pia alikumbushia kauli mbiu ya Taasisi isemayo “Tumeahidi, Tumetimiza na Allah ni Shahidi”

Mzungumzaji wa kwanza katika ratiba ya asubuhi ya kikao hicho, Limbanga Mohamed aliwasilisha historia fupi ya taasisi ya The Islamic Foundation na shughuli zinazofanywa na taasisi ili vijana hao wa kujitolea wapate kuifahamu taasisi hii kiundani pamoja na mpangilio wake wa mgawangyo wa majukumu katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi.

Kwa upande wake mzungumzaji wa pili wa kikao hicho, Niyazhan Ibrahim yeye alijikita katika kuwajenga kifikra volunteers kwa kuwapa misingi, kanuni, sera na mbinu za kujitolea katika dini ya Allah katika misingi inayokubalika kisheria.

Huku pia akitumia fursa hiyo kuwanasihi vijana hao kuitumia nafasi waliyoipata pamoja na ujana wao vyema kwani hizo ni neema za Allah (s.w.t) ambazo baadae watakuja kuulizwa walizitumia vipi. Aliendelea kuwakumbusha na kuwabainishia baadhi ya sheria mbalimbali ambazo taasisi imeziweka ili kuchunga misingi ya imani yetu.

Mzungumzaji wa tatu katika ratiba ya asubuhi Ramadhan Maulid alipata fursa adhimu ya kuangazia baadhi ya shughuli za kidini na kijamii ambazo volunteers wamezifanya kwa kipindi cha mwaka mmoja, pia alipata nafasi ya kuchambua mwenendo wa shughuli hizo ili kuonesha mafanikio, changamoto na malengo ya baadae.

Shughuli zilizofanywa na TIF Boys ni kama vile zoezi la kusafisha misikiti kila mwezi, ugawaji wa tende na maji katika viunga vya jiji la Dar Es Salaam ndani ya mwezi wa Ramadhan, Safari ya upandaji mlima Uluguru.

Kwa upande wa TIF Girls wao walifanya mikutano ya mara kwa mara ndani ya mwezi wa Ramadhan kwa ajili ya darsa, iftaar na kufahamiana, pia shughuli za halaqah mbalimbali.

Katika ratiba ya mchana, mzungumzaji Niyaz Ibrahim alijikita katika kufanya tathmini ya makongamano yaliyopita na kuwaonesha mafanikio waliyoyapata, changamoto na kinachotarajiwa katika makongamano yajayo.

Mwisho kabisa alitumia fursa hiyo kuwapa mikakati ambayo viongozi wameipanga katika kuhakikisha kongamno lijalo la pili la Afrika Mashariki linafanikiwa.

Mwisho wa kikao hicho volunteers hao walipata wasaa wa kupata chakula cha mchana kwa pamoja kabla ya kutawanyika kwa ajili ya utelekezaji wa majukumu yanayowakabili katika maandalizi ya kongamano lijalo.

Kwa upande wao volunteers wapya waliokuja kwenye kikao hicho walitoa mrejesho kuwa wanashukuru kupata fursa hiyo adhimu ya kutumikia dini yao na kuupeleka mbele uislamu, pia wamefurahi kupokelewa kwa bashasha na ndugu zao na kuahidi kushirikiana nao katika kazi kubwa iliyo mbeleni.

Show More

Limbanga M. Limbanga

Ni mhandisi wa Umeme na Elekroniki. Pamoja na shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa katika uhandisi pia anatumia muda wake katika kujitolea kuandika,kuhariri na kutafsiri makala mbalimbali, ni mmoja kati ya vijana wa kujitolea katika taasisi ya TIF katika masuala ya kidini na kijamii. Anapendelea kuielemisha jamii na kutumia ujuzi wake kunufaisha wengine.

Related Articles

Back to top button
Close