-

Kampeni ya Hijja yazinduliwa rasmi nchini

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa kushirikiana na taasisi nyingine 17 za hapa nchini zilizoruhusiwa kusafirisha mahujaji wamezindua kampeni ya kuhamasisha Waislamu kwenda Hijja nchini Saudi Arabia mwaka 1440 Hijiriya (2019).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika Hotel ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Shirikisho la Vikundi vya Hijja (Biiitha) hapa nchini, Sheikh Mussa Hemed, amesema idadi ya wanaohudhuria Hijja hapa nchini bado ni ndogo na hivyo kuna umuhimu wa kuhamasisha watu waende kwa wingi. Pia Sheikh Hemed alisema, kampeni hiyo itafanyika nchi nzima na kuwaomba Waislamu washirikiane kuiwezesha.

Kiutaratibu, Tanzania hupewa nafasi 25,000 hadi 30,000 za mahujaji lakini waendaji huwa kati ya 2,500 na 4,000. Sababu mbalimbali za hali hiyo zimekuwa zikitolewa zikiwemo za kiuchumi na muamko hafifu. Sheikh Hemed alisema taasisi 17 zilizokidhi vigezo vya awali mpaka sasa bado zinatakiwa kukamilisha taratibu zingine za malipo ya ada ya taasisi na ada kwa kila anayenda Hijja. Sheikh Hemed alisema kwamba, taasisi zitakazoshindwa kukamilisha taratibu hizo zitaondolewa katika orodha huku akibainisha kuwa mwisho wa kufanya hivyo ni Aprili 10 mwaka huu.
Kuhusu mwisho wa kufunga mikataba ya nyumba huko Makka na Madina, Sheikh Hemed alisema kuwa Saudi Arabia imeweka mwisho wa kufanya hivyo kuwa ni Mei 5 mwaka huu sawa na Shaabani 29, 1440.

Aidha, alisema ili kuondoa usumbufu wanaokutana nao mahujaji wakati wa kuchukua alama za vidole (fingerprints) wanapowasili nchini Saudi Arabia, Hemed alisema zoezi hilo kwa sasa litafanyika hapa nchini kabla ya safari.

Orodha ya taasisi 17

Taasisi hizo zilizokidhi vigezo vya awali ni Alhusna Hajj Trust, Masjid Adil, Shamsul Maarifa Kheir, Peace Travel and tours Ltd, Jamarat Hajj and umra Traveller Ltd na Dalali Islamic center Hajj and umra. Zingine ni Tanzania Muslim Hajj Trust, Zam Zam centre Hajj and Umra, Kitengo cha Hijja cha Bakwata, Ibn Taiyimiyya Salafi Foundition Hajj and Umra na Ahlul Daawa Hajj Travelling Agency na Labbaik Travel and Tours Ltd. Pia M2 Travel Company Ltd, TCDO, Aljazirah International Hajj Trust, Albushir Tours Ltd na Alkhaibar Hajj and Umra CO.

Naye Imamu Mkuu wa msikiti wa Manyema jijini Dar es Salaam, Sheikh Hemed Jongo ameziasa taasisi za Hijja kutochafuana kwa lengo la kupata mahujaji. “Tunapofanya kampeni yetu isiambatane na taasisi moja kuibughudha taasisi nyingine. Kampeni ilenge kuonesha mema ambayo taasisi hiyo inayoweza kumfanyia mhusika,” alisema Sheikh Jongo.

Taasisi kujipanga

Nao wahusika wa baadhi ya taasisi hizo akiwemo mratibu wa taasisi ya Dalali Islamic Center Hajj and Umra, Sheikh Abdillah Mborya alisema, taasisi yake imejipanga vema kuwahudumia mahujaji. Sheikh Mborya ambaye taasisi yake ni ya kwanza kuanzishwa mkoani Dodoma alisema watahakikisha wanakamilisha taratibu zote. Pia, alitangaza kuwa, gharama zao kwa hujaji mmoja ni dola 4,500.

Kauli ya Uhamiaji

Naye Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji, Godfrey Sylvanus Muria ambaye alimuwakilisha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini Dkt. Anna Peter Makakala, amezitaka taasisi zote zitakazosafirisha mahujaji kuhakikisha zinapeleka majina na picha za wasimamizi wao katika ofisi ya Uhamiaji. Muria alisema, lengo la kufanya hivyo ni kuondoa usumbufu kwa mahujaji kwani baadhi ya taasisi zimekuwa na wasimamizi wengi wakati wa safari kiasi cha kuleta usumbufu kwa wateja wao.

Pia aliwatolea wito wale wenye lengo la kwenda Hijja mwaka huu na hawana hati ya kutafuta hati hizo mapema ili kuondokana na usumbufu hapo baadae.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close