-1. Habari2. Taifa

Kamari, ulevi sumu zinazolitafuna taifa polepole

Kamari na matumizi ya mihadarati kama bangi, pombe, mirungi na ‘unga’ ni mambo yaliyoshamiri katika jamii yetu hivi sasa. Kamari na ulevi ni kama ndugu–wapo pamoja kila mahali, ingawaje bangi, mirungi na ‘unga’ huuzwa kwa kificho.

Lakini ukitaka kucheza kamari huhitaji kwenda Kasino–vituo vya kuchezea vipo kila kona, hata mitaani, kwenye vituo vikuu vya mabasi na katika viwanja vya soka.

Hata hivyo, watu wengi hupendelea kucheza kamari kupitia simu za mkononi kwa sababu huko wanatozwa kiwango kidogo cha fedha (kuanzia shilingi 500 hadi 1000) ukilinganisha na Kasino ambako mchezaji hulazimika kutoa pesa nyingi kwa wakati mmoja.

Tatizo ni kwamba wanaoshiriki michezo hiyo wanahitaji au kutamani kupata utajiri wa haraka, hivyo wanaposhindwa hushawishika kucheza tena na tena hadi kufilisika.

Si nia ya makala hii kutaja madhara yatokanayo na kamari na ulevi, lakini yafaa tuzingatie kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: “…Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet’ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shetani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuswali. Basi je, mmeacha?” (Qur’an, 5:90–91).

Aya hii inabainisha wazi kuwa aina zote za pombe na kamari ni haramu, hivyo yeyote atakayejihusisha na viwili hivyo atapata adhabu kali. Uzuri ni kwamba hata Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeitahadharisha jamii juu ya madhara ya pombe likisema, kuna hatari kubwa zaidi ya kunywa hata kiasi kidogo kwani mnywaji anakuwa katika hatari ya kupata maradhi kama saratani, kiharusi, moyo na maradhi mengine.

Hii inaonesha kuwa hakuna ‘kiasi’ cha pombe ambacho ni salama, kama ilivyothibiti katika hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) inayosema: “Kinacholevya kwa wingi wake, hata kwa uchache wake ni haramu.” (Ibnu Majah). Kadhalika, Mtume ameharamisha ulevi, michezo ya bahati nasibu, kamari ya karata, na gobairah (aina ya pombe) na akasema: “Kila ulevi ni haramu.” (Abu Daud).

Pamoja na ubainifu huo, kamari na ulevi vimeendelea kuwa sehemu ya maisha katika jamii nyingi ulimwenguni. Zamani kamari ilikuwa inachezwa katika maeneo maalumu lakini siku hizi kamari inachezwa
hadharani, vijijini mpaka mijini. Watu hutumia simu zao kucheza kamari– iwe alfajiri, alasiri au usiku wa manane. Kwa upande wa mihadarati, hali ni hiyo hiyo, vijana hawajaachwa salama.

Dawa za kulevya zimeathiri kundi kubwa la vijana wengi mitaani wakiwemo wanafunzi, hasa wa vyuo na shule za sekondari zilizopo mijini. Ukifanya utafiti mdogo utagundua kuwa, baadhi ya wanafunzi wanapokwenda shule, au wakati wa mapumziko, huchepuka pembeni na kuvuta bangi. Hali hii inawafanya wasiwe makini darasani kwani bangi huwapa jeuri ya kutowatii walimu. Chochote wanachotaka, hufanya na kama hakuna udhibiti, nidhamu ya shule hushuka.

Matokeo yake, hawafanyi vizuri katika mitihani ya taifa kwa sababu ya utoro. Hata wanapohudhuria darasani wanakuwa wapo wapo tu, badala ya kuchota elimu na maarifa, wanachota bangi kichwani. Si wanafunzi tu, pia madereva wanaoendesha malori na mabasi ya masafa marefu hutafuna mirungi huku wanaendesha wakidai kuwa wanapunguza usingizi.

Pia, katika baadhi ya maeneo hapa nchini, inaripotiwa kwamba uzalishaji wa mazao shambani umekuwa ukishuka siku hadi siku. Baadhi ya wanaume hawajishughulishi kabisa na kilimo na badala yake huamkia pombe wakidhani itawapa nguvu, kumbe ni kinyume chake. Nao vijana waliobobea kwenye uraibu wa dawa za kulevya wamekuwa wakiuza mali zao kidogo kidogo, mwishowe wanauza hata nguo zao ili wakapate ‘kete’.
Kwa kutambua haya yote, mwaka jana Tanzania ilitangaza mkakati mpya wa kupambana na uingizaji na uuzwaji wa aina mbalimbali za dawa za kulevya.

Akizungumza katika hafla ya kumuapisha Kamishna mpya wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga, Rais John Magufuli alisema serikali yake haitajihusisha na raia wa Tanzania atakayepatikana na hatia nje ya nchi ya kujihusisha na madawa ya kulevya na kama raia huyo amehukumiwa kunyongwa basi anyongwe.

Hata hivyo, bado kumekuwepo na visa kadhaa vya kukamatwa kwa Watanzania wanaojiohusisha na biashara ya ‘unga’ ndani na nje ya Tanzania. Huu ni ushahidi kuwa mikakati madhubuti bado haijawekwa kupambana na biashara hiyo haramu.

Labda viongozi wetu wachukue uamuzi kama aliyochukua Waziri wa Usalama wa Kenya, Dkt. Fred Matiang’i, aliyetangaza kuwachukulia hatua wananchi, raia wa kigeni na maafisa wa serikali wanaoendesha biashara ya kamari na mihadarati.

Katika kile kisichotarajiwa na wengi, Matiang’i alichoma mashine za kuchezeshea kamari huko Dagoretti, akisema kuwa kamari ni haramu na kamwe haitaruhusiwa nchini Kenya. Ni kwa kuchukua hatua kama
hizi tunaweza kukomesha tatizo la kamari na dawa za kulevya hapa nchini.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close