-

Imani za kishirikina zimetugeuza wanyama!

Mbeya ni miongoni mwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania inayoongoza kwa matukio ya ukatili kwa watoto hususani ubakaji na kukata sehemu mbalimbali za miili yao kama vile masikio, ulimi na hata sehemu za siri.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema kuwa, matukio hayo yanahusishwa zaidi na imani za kishirikina na hivyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kukabiliana na tatizo hilo.

Chalamila ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Jinsia lililofanyika katika kijijini cha Hatwelo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Kwa ujumla, matukio ya ubakaji kwa watoto yamekuwa yakiongezeka nchini mwaka hadi mwaka licha ya kuwepo kwa sheria kali. Takwimu za Jeshi la Polisi nchini Tanzania zinaonesha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambapo mwaka 2017 matukio yalikuwa 13,457, mwaka 2018 matukio 14,419 na mwaka 2019 matukio 15,680.

Hii inatupa picha kuwa bado kunahitajika mkakati madhubuti wa kuhakikisha sheria zinazowekwa zinapunguza matukio ya ukatili kwa watoto kama siyo kuyamaliza.

Kama alivyosema Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, matukio mengi ya ubakaji katika mkoa huo yanahusishwa zaidi na imani za kishirikina. Na hapo ndipo tunapata jibu la kwanini ushirikina ni jambo baya na lisilokubalika kidini na kijamii.

Ripoti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imebainisha kuwa wahusika wengi wanaowafanyia watoto ukatili wanatoka karibu na familia au ni ndugu wa watoto. Si nia yangu kuelekeza lawama kwa yeyote, lakini ninachosema ni kwamba ushirikiano kati ya wazazi na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama ni muhimu katika kukabiliana na vitendo hivi viovu.

Nasema haya kwa sababu, suala la utamaduni au desturi na mila ya kumaliza masuala ya ukatili kimyakimya kwa kisingizio cha kulinda heshima ya mtuhumiwa na kulinda hadhi yake linatajwa kuwa ndio chanzo cha kuongezeka kwa matukio hayo.

Hili ndilo linalowafanya wazazi wengi kushindwa kuhudhuria mahakamani kutoa ushahidi hali inayopelekea kuchelewa kwa kesi na mara nyingine kesi kufutwa.

Hivyo basi, jamii itoe ushirikiano wa kutosha katika mamlaka husika pindi wanapogundua mwanajamii anayefanya vitendo hivi bila ya kufumbia macho, ili hatua ziweze kuchukuliwa na kutoa fundisho kwa wengine wenye tabia hiyo mbaya. Wabakaji wamejenga hofu kubwa kwa wazazi na walezi juu ya mustakbali wa usalama wa watoto wao. Vitendo vya ubakaji si tu kwamba vinasababisha majeraha yasiyotibika kwa watoto, pia vinaharibu taswira nzuri ya nchi na kuongeza hofu kwa watu.

Kuongezeka kwa matukio ya ubakaji nchini kumewalazimisha wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao wadogo shule na kuwarudisha nyumbani. Haya yanafanyika, ili kila mmoja amnusuru mtoto wake na hatari ya kubakwa na kukatwa viungo.

Kiini cha tatizo

Baadhi ya waganga wa kienyeji, hupiga ramli chonganishi zinazochochea kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji kwa watoto. Baadhi ya waganga huwatuma wateja wao wanaohitaji utajiri wa haraka kuwabaka watoto na kuwakata viungo vyao vya mwili, kama njia ya kufanikisha azma zao.

Hivyo, juhudi zaidi zinahitajika katika kupambana na vitendo hivyo viovu kutokana na ukweli kuwa katika maeneo mengi ukatili dhidi ya watoto hufanywa na watu ambao wanawaona kila siku (watu wanaowazunguka).

Hakuna sababu ya kuliachia Jeshi la Polisi pekee kupambana na tatizo hili wakati wazazi wana taarifa kuhusu wahalifu, na ni wao na watoto wao ndio wahanga. Natambua kuwapo kwa hatua na juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vya dola katika kuwasaka watuhumiwa wa matukio ya ubakaji wa watoto.

Ushauri wangu kwa wazazi ni kwamba wawe tayari kudumisha ushirikiano kati yao na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini kuwapo hali isiyo ya kawaida kwa watoto wao. Kinachohitajika hapa ni polisi na wazazi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi.

Sambamba na hilo, ni wajibu wa kila mwananchi kufanya kazi ili kujipatia kipato cha halali, kwani hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha mtu kutafuta utajiri kwa njia za kishirikina. Hilo likifanyika, naamini tamaa ya watu kusaka utajiri kwa njia za kishirikina itapungua kama sio kuisha kabisa.

Hofu ya Mungu kwa wananchi ni jambo la msingi sana katika mapambano dhidi ya ubakaji. Viongozi wa dini wanapaswa wasimame kikamilifu katika kutoa mahubiri na maonyo kukemea tabia hii ambayo inachafua taswira nzuri ya nchi yetu inayosifika duniani kama kisiwa cha amani na utulivu.

Hata mwananchi asiyeamini dini yoyote, dhamiri ya moyo wake imkataze kutenda kosa la ubakaji, kwani Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an:

“…Wala msikaribie mambo machafu, yanayoonekana, na yanayofichikana…” [Qur’ an, 6:151].

Watoto wana ndoto kubwa za kufikia malengo yao kupitia elimu. Hivyo, matukio ya ubakaji ni kikwazo cha kufikia ndoto zao. Mtoto anapaswa kwenda shule bila ya kuwa na hofu yoyote ili kupokea vizuri yale yatakayofundishwa na walimu wake. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha anawaongoza watoto ili watimize ndoto zao. Wakati umefika kwa Watanzania kujitathmini na kuhakikisha kuwa watoto wanakua salama wakati wote. Tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kukomesha vitendo vya u

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close