-

Idil Adh’ha ni siku ya Ibada, tuisherehekee kwa Ikhlas

“Allaahu Akbar Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Laa Ilaha Illa Allah Allaahu Akbar, Allaahu Akbar Walillahil Hamdu..” 

Hivyo ndivyo watakavyokuwa wakitamka mahujaji wote na Waislamu wengine katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania katika sherehe ya Idil Adh’ha (Idd ya kuchinja au Idd kubwa kama tulivyozoea kuiita) inayotarajiwa kufanyika ‘Insha Allah’ siku chache zijazo.

Mafundisho ya Uislamu yanatuambia kuwa Idd ni siku ya kula na kunywa pamoja na kumdhukuru (kumtaja) Allah. Pia, Idd ni siku ya kuwatembelea ndugu, jamaa, marafiki na watu wenye mahitaji maalumu kama vile wenye ulemavu, wafungwa, mafukara na maskini kwa kuwapa misaada mbalimbali, zaka na hata sadaka ili wasijione madhalili, wanyonge, wapweke na wenye huzuni katika siku hii ya furaha.

Hakika, siku za Idd katika Uislamu ni siku za furaha mno kwa yule mwenye nia njema, na si kwa aliyekusudia kujifaharisha na kujionesha katika macho ya watu.

Licha ya ukweli kwamba Idd ni alama tukufu katika alama za Uislamu, baadhi yetu tumekuwa tukipuuzia na hadi kufikia hatua ya kutanguliza na kufadhilisha sikukuu za kizushi kuliko sikukuu hii ambayo ni sunna ya Mtume (rehema na amani ya Allah ziwe juu yake). Allah Mtukufu anasema: “Ndiyo hivyo! Na anayetukuza ibada za Allah, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.” [Qur’an, 22:32].

Anayetaka kujua tabia za umma huu, basi afuatilie sikukuu zake. Katika Uislamu, sikukuu ni ibada kwa sababu zimefungamana na ibada. Ndani ya sikukuu, zinadhihiri tabia njema katika tabia za Kiislamu ambazo Muislamu anapaswa kujipamba nazo hasa kwa yule anayefahamu maana halisi ya sikukuu katika Uislamu.

Tuepuke maneno na matendo machafu Katika Uislamu, sikukuu ni siku ya kufurahi pamoja, ni siku ya kuliwazana kusaidiana na kufarijiana kwa hali na mali. Sikukuu ambapo hutawala hisia za undugu wa Kiislamu, mshikamano, upendo na huruma. 

Idd katika Uislamu ni kujitakasa na udanganyifu pamoja na vitimbi vya shetani. Idd ni kumtii Allah na kumtakasa katika ibada zake, pia ni furaha katika neema mbalimbali za kidunia ambazo Allah ametuneemesha na kutupa kwa hisani yake, ikiwamo kula na kunywa pamoja na kuvaa vizuri. Yote hayo yakifanyika katika misingi inayomridhisha Allah.

Lakini yatupasa tukumbuke kuwa, Idd si kufuata matamanio ya nafsi na ladha ya mambo ya haramu, kujikusanya katika fukwe za bahari wanamume kwa wanawake pamoja katika mandhari zilizoharamishwa katika Uislamu.

Idd si kuacha mambo ya wajibu na kukimbilia mambo ya hovyo, na ya ufisadi katika ardhi, si kuvuka mipaka na kusahau wajibu wa kumshukuru Mola Mlezi wa viumbe wote

Idd katika Uislamu si kujifaharisha kwa mavazi mapya, na kutembea kwa maringo katika mgongo wa ardhi kwa majivuno na kiburi. Idd si mikusanyiko ya vijana na watu wazima wakiimba muziki na kusherehekea kwa vilevi na ngoma za aina mbalimbali. Idd ni msimu wa kutabasamu kwa watu wenye shida na matatizo.

Hivyo, ni wajibu wetu Waislamu kuitumia ipasavyo sikukuu ya Idil Adh’ha kwa kumcha Allah na kamwe tusiigeuze kuwa ni siku ya kumuasi Muumba wetu. Pia, tusisahau kutekeleza ndani yake mambo ya wajibu kama vile ibada na mengineyo.

Kadhalika, tusighafilike tukaingia katika mambo maovu, tusifanye matokeo ya sikukuu hii yakawa ni kumkasirisha Allah na kustahiki ghadhabu zake.

Idd ni siku ya ibada, toba na furaha, kwa hiyo tudhihirishe tabia njema ili watu wauone Uislamu katika kilele chake cha tabia njema. Tusiwasahau wenye machungu katika siku hii, tujitahidi kuyaondoa yale yanayowezekana, na yasiyokuwa katika uwezo wa kibinadamu tumuombe Allah kwa hisani yake awahurumie waathirika – wakiwemo wagonjwa, wafungwa, maskini, wenye ulemavu na kadhalika. Wote hawa wanahitaji furaha katika Idd.

Tunafurahi na kushukuru Allah kutuneemesha kwakutufanyatuwe katika Uislamu: “Leo nimekukamiliishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.” [Qur’an, 5:3].

Kwa hiyo, haifai na ni haramu Muislamu kujifananisha na wasiokuwa Waislamu katika kusherehekea sikukuu ya Idd. Uislamu unamtaka Muislamu awe na haiba ya peke yake ambayo inatofautiana na watu wa mila nyingine kama ilivyo pia kuwa, kuwafikiana nao katika mambo yao ni katika uzushi na ni katika mambo ya haramu.

Katika mambo yanayothibitisha utume wa Mtume Muhammad (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) ni kuendelea kuthibiti yale aliyoyaelezea kwa umma wake kuwa yatatokea.

Miongoni mwa mambo hayo ni kauli ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Mtafuata mwenendo wa wale waliokuwepo kabla yenu, shubiri kwa shubiri, dhiraa kwa dhiraa, hata kama wangeingia katika tundu la yuri kenge mtawafuata.” Tukasema: “Ewe Mjumbe wa Allah ni Mayahudi na Manaswara?” Akasema: “Ni kina nani basi?” Akasema: “Hakitosimama Kiyama mpaka umma wangu uchukue yale waliyoyachukuwa umma ziliizopita.” [Bukhari]. Yote haya ni tahadhari kutoka kwa Mtume juu yetu illi tusijifananishe na makafiri katika sikukuu zao kwa sababu kujifananisha nao ni uovu na upotovu

 

Show More

Related Articles

Back to top button
Close